Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Abdi Mahamoud Abdi, amesema kuelekea maadhimisho ya miaka 50 ya kuzaliwa kwa CCM, chama hicho kinatarajia kuandaa shamrashamra mbalimbali zitakazoambatana na matukio ya kuimarisha na kuendeleza uhai wa chama.

Abdi amesema miongoni mwa shughuli zitakazofanyika ni pamoja na kufungua matawi mapya ya CCM, ofisi za chama za mikoa na wilaya, pamoja na kuendelea na ziara za kukagua uhai wa chama katika maeneo mbalimbali nchini.

Amesema hayo wakati akiendelea na ziara ya kukagua uhai wa CCM ndani ya Jimbo la Bumbwini, ambapo ametembelea Tawi la CCM Fujoni, Mkoa wa Kaskazini Unguja.

“Tunapoelekea kutimiza miaka 50 ya CCM, kutakuwa na shamrashamra mbalimbali. Tutafungua matawi mapya, ofisi za CCM za mikoa na wilaya, pamoja na kuendelea kukagua uhai wa chama,” amesema Abdi.

Kwa upande wake, Mnadhimu wa Wawakilishi wa CCM, Machano Othman Said, amewapongeza wanachama wa chama hicho katika Jimbo la Bumbwini kwa uzalendo wao na kuendelea kukiunga mkono CCM pamoja na kuamini katika utekelezaji wa Ilani ya chama.

Katika ziara hiyo, Abdi ametembelea na kukagua uhai wa CCM katika matawi mbalimbali ndani ya Jimbo la Bumbwini, yakiwemo Kiongwe Kidogo, Zingwezingwe, Mangapwani A, Mangapwani B, Kiwambamvua na Mkadini.

Ziara hiyo ni sehemu ya jitihada za CCM za kuimarisha uhai wa chama, kusikiliza changamoto za wanachama na kuhakikisha shughuli za chama zinaendelea kutekelezwa kwa ufanisi katika ngazi za matawi.



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...