Na Mwandishi wetu Dodoma
Wanawake katika Jeshi la Magereza wametakiwa kuongeza ujuzi, maarifa na uwezo wa kutumia teknolojia za kidijitali ili kuendana na mabadiliko ya kiutendaji na kuongeza nafasi yao katika uongozi pamoja na majukumu ya kitaaluma ndani ya Jeshi hilo.
Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhandisi Maryprisca Mahundi, Septemba 7, 2026, jijini Dodoma, wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Mtandao wa Wanawake wa Jeshi la Magereza Tanzania (TPSWNet) 2026.
Mhandisi Mahundi amesema dunia ya sasa inahitaji watumishi wenye uwezo wa kujifunza na kubadilika kulingana na maendeleo ya teknolojia, akisisitiza kuwa wanawake wanapaswa kutumia fursa zinazotokana na mabadiliko ya kidijitali katika kuboresha utendaji wao wa kazi na huduma zinazotolewa na Jeshi la Magereza.
Amesema uwezeshaji wa wanawake hauishii katika kuwapa nafasi, bali unapaswa kwenda sambamba na kuwaandaa kwa elimu, ujuzi na uwezo wa kushindana kwa haki katika nafasi mbalimbali za uongozi na kitaaluma.
“Nawahimiza wanawake wa Jeshi la Magereza kujiamini, kuongeza elimu na ujuzi na kujiandaa kwa ushindani wa haki katika nafasi za uongozi na kitaaluma. Katika dunia ya sasa, watumishi wanapaswa kuendelea kujifunza na kutumia teknolojia katika kuboresha huduma,” amesema Mhe. Mahundi.
Kwa mtazamo huo, Naibu Waziri amesema wanawake wa Jeshi la Magereza wana nafasi muhimu ya kuwa sehemu ya mageuzi yanayoendelea katika sekta ya urekebishaji wa wafungwa, huku wakitakiwa kutumia uwezo na uzoefu wao kuchangia katika kujenga Jeshi linalokwenda sambamba na mahitaji ya wakati.
Kwa upande wake, Kamishna wa Divisheni ya Sheria na Uendeshaji wa Magereza, CP Nicodemus Menyiansumba Tenga, amesema mafanikio yaliyofikiwa na wanawake wanaoshika nafasi mbalimbali ndani ya Jeshi hilo ni ushahidi wa uwezo wao na yanapaswa kuwa chachu kwa wanawake wengine kujituma na kuwania nafasi za uongozi na kitaaluma.
Akisoma taarifa ya Mtandao wa Wanawake wa Jeshi la Magereza Tanzania, Kamishna wa Huduma za Urekebishaji Jeshi la Magereza, CP Amina Jumanne Kavirondo, amesema TPSWNet imeendelea kuwa jukwaa muhimu la kuwawezesha wanawake, kukuza usawa wa kijinsia na kujenga mazingira rafiki ya kazi kwa watumishi wanawake.
Amesema mtandao huo pia unalenga kuhakikisha wanawake wanapata uwakilishi katika maeneo mbalimbali ndani na nje ya Jeshi pale inapowezekana, huku ukiendelea kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika majukumu ya urekebishaji wa wafungwa pamoja na masuala ya ulinzi na usalama.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mchango wa wanawake katika urekebishaji wa wafungwa unaonekana pia kupitia shughuli mbalimbali za kuwapatia wafungwa ujuzi na kuwaandaa kurejea katika jamii wakiwa na uwezo wa kuendesha maisha yenye tija.
Mkutano huo pia unajadili namna ya kuimarisha uwezo wa wanawake katika uongozi, kujitambua na kufanya maamuzi, sambamba na kubadilishana uzoefu na ujuzi wa kitaifa, kikanda na kimataifa kuhusu urekebishaji wa wafungwa.
Mbali na masuala ya uongozi na utendaji, washiriki wanajadili pia malezi, maendeleo ya awali ya mtoto, wajibu wa kijamii, uwezeshaji wa kiuchumi, maadili, afya na matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii.
Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Mtandao wa Wanawake wa Jeshi la Magereza Tanzania 2026 unafanyika jijini Dodoma kuanzia Septemba 7 hadi 9, 2026, ukiwakutanisha wanawake wa Jeshi la Magereza pamoja na wadau mbalimbali.
Mkutano huo umebeba kaulimbiu “Wanawake Mahiri, Jeshi la Magereza la Kisasa, na Taifa lenye Ustawi kuelekea Dira 2050.”






.jpeg)

.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...