-TEKNOLOJIA, UBUNIFU KUTUMIKA KUPUNGUZA GHARAMA ZA USAFIRISHAJI

Na Ashura Mohamed – Arusha

WATAALAMU wa usafirishaji, ununuzi na mnyororo wa ugavi kutoka ndani na nje ya Afrika wamekutana jijini Arusha kujadili namna teknolojia na ubunifu unavyoweza kutumika kupunguza gharama za usafirishaji na kuimarisha mchango wa sekta hiyo katika uchumi.

Akizungumza wakati akimwakilisha Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, katika Mkutano wa Nane wa Afrika wa Usimamizi wa Uendeshaji na Mnyororo wa Ugavi (ACOSCM), Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile, amesema uboreshaji wa miundombinu ya usafirishaji ni muhimu katika kupunguza gharama za usafirishaji nchini.

Amesema sekta ya usafirishaji ni mhimili muhimu wa uchumi kwa kuwa inaunganisha wazalishaji na masoko, kuwezesha biashara na kuchochea shughuli za kiuchumi.

Kwa mujibu wa Kihenzile, sekta ya usafirishaji nchini ilizalisha dola za Marekani bilioni 2.7 mwaka 2025, sawa na asilimia 15.6 ya mauzo ya nje ya Tanzania, ikilinganishwa na dola bilioni 2.2 mwaka 2024.

“Serikali yetu inaendelea kuboresha miundombinu ya usafirishaji nchini kwa sababu sekta hii ni muhimu kwa wakulima, wavuvi na wajasiriamali. Gharama za usafirishaji zinapopungua, mnufaika wa mwisho ni mwananchi, kwa kuwa gharama za kusafirisha bidhaa zake hupungua,” amesema Kihenzile.

Aidha, amewataka washiriki wa mkutano huo kujikita katika kujadili suluhisho la changamoto zinazokabili sekta ya usafirishaji, ikiwamo namna vijana na makundi mengine yanavyoweza kushiriki na kunufaika na fursa zinazotokana na miradi mbalimbali ya miundombinu, ikiwamo Reli ya Kisasa (SGR).

Kwa upande wake, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe anayeshughulikia Taaluma, Prof. Hawa Tundui, amesema mkutano huo umewakutanisha wataalamu takribani 200 kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika pamoja na mabara ya Ulaya na Asia.

Amesema mjadala mkuu umejikita katika namna ya kutumia ubunifu na teknolojia katika masuala ya usafirishaji, ununuzi na mnyororo wa ugavi ili kupunguza gharama na kuongeza ufanisi.

“Mada kubwa ni namna bora ya kutumia ubunifu na teknolojia katika masuala ya usafirishaji, ununuzi na ugavi. Tumewakutanisha wadau mbalimbali, wakiwemo watafiti na wataalamu kutoka Afrika, Ulaya na Asia, ili kuangalia namna ubunifu na teknolojia unavyoweza kuleta mchango katika serikali zetu na kusaidia kupunguza gharama za usafirishaji,” amesema Prof. Tundui.

Amesema lengo la mkutano huo ni kufikia maazimio ya pamoja yatakayosaidia kuhakikisha sekta ya uchukuzi inakuwa na ufanisi na kuleta unafuu katika mnyororo mzima wa usafirishaji.

Mkutano huo umeandaliwa na Chuo Kikuu cha Mzumbe kwa kushirikiana na Khune Foundation Tanzania.







Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...