Na Janeth Raphael - MichuziTv


Watanzania kutoka makundi mbalimbali wanatarajiwa kukutana Novemba 7 mwaka huu katika Tanzania National Prayer Breakfast (TNB), jukwaa linalolenga kuliombea taifa, kuimarisha umoja na mshikamano pamoja na kujadili masuala yanayohusu uongozi, maadili, utumishi wa umma na maendeleo ya nchi.

Tanzania National Prayer Breakfast inalenga kuwaunganisha Watanzania bila kujali tofauti zao za kidini, kisiasa au kijamii, kwa kuwapa nafasi viongozi, vijana, wanawake na makundi mbalimbali kukutana, kuombea taifa na kujadili namna ya kujenga Tanzania yenye maadili, umoja na watu wanaoshirikiana.

Mwenyekiti wa Tanzania National Prayer Breakfast, Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye, amesema jukwaa hilo ni muhimu katika kuwaunganisha Watanzania na kutoa nafasi kwa viongozi wa kitaifa kuzungumza kuhusu masuala mbalimbali yanayolihusu taifa, akisisitiza kuwa umoja wa kitaifa ni wajibu wa kila Mtanzania na unapaswa kukumbushwa mara kwa mara.

“Lengo letu ni kuendelea pamoja, taifa moja na watu wamoja. Ni wajibu wetu kukumbushana kama taifa umuhimu wa kuwa kitu kimoja,” amesema Sumaye.

Amesema mwaka huu wamekusudia kufanya tukio hilo kwa kiwango kikubwa zaidi ili Watanzania wengi watambue umuhimu wa jukwaa hilo na Serikali pamoja na Bunge kulitambua kama sehemu muhimu ya kuimarisha umoja, maadili na mshikamano wa taifa.

Kwa mujibu wa Sumaye, Tanzania National Prayer Breakfast si jukwaa la dini moja wala kundi fulani, bali linawakutanisha watu wa dini mbalimbali, vyama mbalimbali na makundi tofauti kwa lengo la kuliombea taifa na kujenga misingi ya kuendelea kuwa taifa moja lenye watu wanaoshirikiana na kuheshimiana.

Amesema maandalizi ya tukio hilo yataanza Novemba 5 kwa semina, huku Novemba 6 kukiwa na mjumuiko maalumu wa wanawake, ambao amesema wamekuwa wakibaki nyuma katika kushiriki katika majukwaa ya aina hiyo. Vijana nao watapewa nafasi katika programu hiyo kutokana na umuhimu wao katika ujenzi wa taifa, huku wakilenga kuwajenga katika maadili, uongozi bora na uwajibikaji.

Amesema kilele cha shughuli hizo kitakuwa Novemba 7, siku ambayo itafanyika Tanzania National Prayer Breakfast na ambapo wanatarajia mgeni rasmi kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Pia wanatarajia kushiriki wageni kutoka mataifa mbalimbali, wakiwamo wawakilishi wa mabunge, mahakama, mashirika ya kimataifa, vijana na wanawake kutoka maeneo ya mijini na vijijini.

Sumaye amesema ushiriki wa watu kutoka ndani na nje ya Tanzania unaonyesha kuwa Tanzania National Prayer Breakfast ni programu yenye mtazamo mpana inayolenga kuunganisha watu kupitia uongozi wa maadili, maombi na ushirikiano. Amesema jukwaa hilo linashirikisha wadau mbalimbali wakiwamo KLNT, Kingdom Leadership, Tanzania World Vision pamoja na kikundi cha waombaji wa wabunge, ambao wamekuwa sehemu ya maandalizi ya tukio hilo.

Aidha, amesema wanataka Tanzania National Prayer Breakfast iwe sehemu inayotambulika zaidi kitaifa na kuendelea kutumika kama jukwaa la kuimarisha umoja na mshikamano wa taifa, huku wakitarajia Serikali na Bunge kuona umuhimu wa kulibeba na kuliendeleza katika miaka ijayo. Amesema iwapo Bunge litaridhia, mwakani wanataka suala hilo lipewe nafasi kubwa zaidi kwa sababu jambo linalolenga kuwaunganisha Watanzania halipaswi kuishia njiani wala kukosa kuendelezwa.

Kwa upande wake, Katibu wa Tanzania National Prayer Breakfast, L. Isack Mpatwa, amesema jambo la msingi ni kuhakikisha kunakuwa na mkakati madhubuti wa kuwakutanisha watu kutoka makundi mbalimbali ili kujenga umoja na mshikamano wa kitaifa.

Mpatwa amesema jukwaa hilo linapaswa kuendelea kuwa eneo la kukumbushana kuhusu maadili, uongozi bora na wajibu wa kila mmoja katika kulijenga taifa, akisisitiza kuwa lengo si kwa kundi moja pekee bali dini zote na vyama vyote vinapaswa kuwa sehemu ya juhudi hizo kwa kuwa Tanzania ni ya watu wote.

Amesema Tanzania National Prayer Breakfast ni sehemu ya programu pana ya uongozi wa maadili, utumishi wa umma na maombi jumuishi inayolenga kuwaunganisha viongozi na wananchi katika kujenga taifa lenye umoja na mshikamano.

Kwa mujibu wa Mpatwa, kupitia mikutano hiyo Watanzania wanapata nafasi ya kukutana, kuombea nchi yao na kukumbushana umuhimu wa kuendelea kushirikiana katika kulinda umoja na amani ya taifa, huku Tanzania National Prayer Breakfast ikiendelea kulenga kuwa jukwaa linalowakutanisha Watanzania wa makundi mbalimbali katika kujenga taifa lenye maadili, mshikamano na mwelekeo wa pamoja.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...