Na Janeth Raphael -MichuziTv -Bungeni Dodoma
SERIKALI imesema imekamilisha mapitio ya Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana ya Mwaka 2007 na kwamba Toleo la Mwaka 2024 tayari linaendelea kutekelezwa nchini.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Zainab Katiba, kwa niaba ya Waziri wa Maendeleo ya Vijana, wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Timida Mpoki Fyandamo, aliyetaka kujua ni lini Serikali itapitia upya Sera ya Maendeleo ya Vijana ya Mwaka 2007.
Naibu Waziri amesema kabla ya kufanya mapitio hayo, Serikali ilifanya tathmini ya utekelezaji wa sera hiyo mwaka 2022 kwa lengo la kubaini mafanikio yaliyopatikana, changamoto, mapungufu pamoja na masuala mapya yaliyojitokeza katika maendeleo ya vijana.
Amesema matokeo ya tathmini hiyo, pamoja na maoni ya wadau mbalimbali, yalitumika katika kuandaa Toleo la Mwaka 2024 la Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana.
Kwa mujibu wa Serikali, sera hiyo iliidhinishwa na Baraza la Mawaziri Aprili 25, 2024 na kuzinduliwa rasmi jijini Dodoma Agosti 12, 2024.
Amesisitiza kuwa Serikali kwa sasa haipo katika hatua ya kupanga kufanya mapitio ya sera hiyo, kwa kuwa zoezi hilo tayari limekamilika na Toleo la Mwaka 2024 linaendelea kutekelezwa.
Aidha, Serikali imeandaa Mkakati wa Utekelezaji wa Sera hiyo kwa kipindi cha mwaka 2024 hadi 2034, unaoainisha afua zitakazotekelezwa, matokeo yanayotarajiwa, viashiria vya utekelezaji, muda wa utekelezaji pamoja na majukumu ya wadau mbalimbali.
Serikali imesema itaendelea kuratibu, kufuatilia na kutathmini utekelezaji wa sera hiyo ili kuhakikisha changamoto na mahitaji ya vijana yanabainika na kushughulikiwa kwa wakati.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...