Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Ndugu Abdi Mahamoud Abdi, amesema chama hicho kitaendelea kuwasimamia viongozi wa majimbo kuhakikisha wanatekeleza Ilani ya CCM kwa vitendo na kuwaletea maendeleo wananchi.

Ndugu Abdi ameyasema hayo Oktoba 7, 2026, wakati akiendelea na ziara ya kukagua uhai wa CCM kuanzia ngazi ya matawi katika Jimbo la Pangawe, Zanzibar, pamoja na kusikiliza changamoto zinazowakabili wanachama na kutafuta namna ya kuzitatua.

Amesema CCM ina mpango wa kuhakikisha wanachama wake wanawezeshwa kiuchumi, ikiwemo kuwawezesha kupata mitaji itakayowasaidia kuanzisha na kuendeleza shughuli mbalimbali za biashara na kujikwamua kiuchumi.

Aidha, amewataka viongozi wa CCM katika majimbo kuwa karibu na wanachama, kusikiliza changamoto zao na kuzifanyia kazi kwa wakati, akisisitiza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kuimarisha uhai na mshikamano wa chama.

Kwa upande wake, Mnadhimu wa Wawakilishi wa CCM Zanzibar, Ndugu Machano Othman Said, amesema wanachama wa CCM katika Jimbo la Pangawe wana dhamana kubwa ya kuendeleza umoja na mshikamano ili kuhakikisha chama kinaendelea kusonga mbele.

Ndugu Machano amewahimiza wanachama kuachana na makundi ndani ya chama na badala yake kujenga umoja, mshikamano na ushirikiano kwa maslahi ya CCM na wananchi kwa ujumla.

Aidha, amewataka wanachama kuendelea kulipa ada za uanachama kwa wakati, akieleza kuwa ada hizo ni muhimu katika kuimarisha shughuli za chama na kuhakikisha CCM inaendelea kutekeleza majukumu yake kwa maslahi ya wanachama na taifa kwa ujumla.

Katika ziara hiyo, Ndugu Abdi ametembelea matawi mbalimbali ya CCM ndani ya Jimbo la Pangawe, yakiwemo Tawi la CCM Pangawe, Tawi la CCM Pangawe Bondeni na Tawi la CCM Muembe Majogoo, ambako amepata fursa ya kuzungumza na wanachama na kusikiliza changamoto zinazowakabili.

Mbali na kutembelea matawi, Ndugu Abdi pia amewatembelea na kuwajulia hali Wazee wa CCM, akiwemo Ndugu Kassima Haji Ameir nyumbani kwake Pangawe na Ndugu Daudi Mussa Daudi nyumbani kwake Pangawe Bondeni.

Ziara hiyo imeelezwa kuwa sehemu ya kuendeleza utamaduni wa CCM wa kuwajali na kuwaheshimu wazee, pamoja na kuimarisha mshikamano na uhusiano kati ya viongozi na wanachama wa chama.












Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...