MAMLAKA ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) inaadhimisha Wiki ya Huduma kwa Wateja kuanzia tarehe 5 hadi 9 Oktoba 2026, kwa kusikiliza na kuhudumia wateja, kupokea maoni na kutoa ufafanuzi kuhusu huduma zake. Shughuli hizo zinafanyika wiki hii yote katika Makao Makuu, ofisi za Kanda ya Pwani, Kanda ya Kati, Kanda ya Ziwa, Kanda ya Kaskazini, Nyanda za Juu Kusini na Ofisi ya Zanzibar, kwa lengo la kuimarisha ubora wa huduma na mahusiano.
Maadhimisho yalianza kwa watumishi kupewa mafunzo ya huduma kwa mteja. Akiwasilisha mada, Juma Fimbo alisisitiza umuhimu wa usikivu na kujituma katika utoaji wa huduma. “Huduma bora kwa mteja inaanza na kumsikiliza, kuelewa mahitaji yake na kuchukua hatua kwa wakati. Kauli mbiu ya ‘The Extra Mile’ inatukumbusha kujituma zaidi katika kumsaidia mteja, kumpa taarifa sahihi na kuhakikisha anapata huduma kwa heshima na ufanisi na kumfutilia baada ya kutoa huduma husika,” alisema Fimbo.
Bw. Fimbo pia alisisitiza kuwa mwajiri wetu ni mteja tunayempatia huduma na TCAA ni mwakilishi tu wa mwajiri wetu.
TCAA itaendelea kutoa huduma bora hata baada ya maadhimisho haya, kwa kuimarisha usikivu na mwitikio kwa mahitaji ya wateja. Katika kutekeleza dhamira hiyo, Mamlaka ilianzisha Dawati la Huduma kwa Wateja linalopokea maswali, maoni na malalamiko, pamoja na kutoa taarifa na mwongozo kuhusu huduma zake. Dawati hilo linafikiwa kupitia WhatsApp +255 771 564 070, simu ya bure 0800 110 193, au barua pepe helpdesk@tcaa.go.tz na dawatilahuduma@tcaa.go.tz.
Aidha, ujio wa huduma za Mamlaka ya Usafiri wa Anga kupitia mfumo wa CASP (Civil Aviation Services Portal) unaimarisha upatikanaji wa huduma kidijitali. Kupitia portal.tcaa.go.tz, wateja wanaweza kuwasilisha maombi, kupakia nyaraka, kufanya malipo na kufuatilia hatua za maombi yao, hatua inayorahisisha upatikanaji wa huduma na kuokoa muda.





Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...