
Na Oscar Assenga, Tanga
BANDARI ya Tanga imevuka lengo la kuhudumia shehena kwa mwaka wa fedha 2025/2026 baada ya kuhudumia tani milioni 2.179 dhidi ya lengo la tani milioni 1.65, ikiwa ni ongezeko kubwa ikilinganishwa na tani milioni 1.3 zilizohudumiwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Aidha, bandari hiyo imepunguza muda wa meli kusubiri huduma kutoka wastani wa siku 10 hadi 20 katika mwaka uliopita wa fedha hadi kati ya siku sifuri na tano katika miezi mitatu ya mwanzo ya mwaka mpya wa fedha.
Meneja wa Bandari ya Tanga, Salehe Mbega, alisema hayo alipokuwa akizungumza wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Mteja, akieleza kuwa mafanikio hayo yametokana na maboresho yaliyofanyika katika utoaji wa huduma.
Alisema maboresho hayo hayajalenga kuongeza idadi ya meli pekee, bali pia yameongeza uwezo wa bandari kushughulikia shehena kwa ufanisi.
Kwa mujibu wa Mbega, mojawapo ya changamoto kubwa iliyokuwa ikiikabili bandari hiyo ni meli kukaa nje ya bandari kwa muda mrefu zikisubiri kuingia gati, hali iliyosababisha malalamiko ya wateja kuhusu kuchelewa kwa mizigo yao.

“Katika mwaka uliopita nilikuwa napokea simu nyingi sana za wateja wakilalamika kwamba meli zimekaa muda mrefu zikisubiri kuingia nangani au magari yao yamefika lakini mizigo haijapakiwa. Kwa miezi hii mitatu tangu kuanza mwaka huu wa fedha, simu hizo zimepungua sana,” alisema.
Alisema uongozi wa bandari ulifanya tathmini kubaini maeneo yaliyokuwa yakisababisha ucheleweshaji na kuyafanyia maboresho, hatua ambayo imeanza kuleta matokeo chanya katika utoaji wa huduma.

Mbega alibainisha kuwa katika kipindi cha Julai hadi Septemba 2026, zaidi ya asilimia 70 ya meli zilizohudumiwa katika bandari hiyo zilianza kupata huduma bila kusubiri, huku muda wa kusubiri kwa ujumla ukipungua hadi kati ya siku sifuri na tano.
Aliongeza kuwa maboresho hayo yameambatana na kupungua kwa muda ambao meli hutumia zikiwa gati, ambapo nyingi sasa huhudumiwa ndani ya siku tatu hadi tano, na katika baadhi ya mazingira muda huo unaweza kufikia siku saba.
Kwa upande wa meli za mafuta, alisema muda wa kusubiri nao umepungua, huku baadhi ya meli zikiingia katika eneo la kuhudumiwa ndani ya chini ya siku mbili kabla ya kukamilisha shughuli zake na kuondoka.
Akizungumzia utendaji wa bandari hiyo, Mbega alisema katika mwaka wa fedha 2025/2026 ilihudumia meli 166 dhidi ya lengo la meli 163, ikilinganishwa na meli 150 zilizohudumiwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Alisema mafanikio hayo yanatoa matumaini ya kufanya vizuri zaidi katika mwaka wa fedha unaoendelea, akisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), kampuni za meli, mawakala wa forodha, wateja na taasisi nyingine zinazohusika na shughuli za bandari.
“Tumeshanza kwenda extra mile kwa vitendo. Ufanisi huu hauji kwa sababu ya TPA pekee, bali ni matokeo ya ushirikiano wa wadau wote. Tunaamini tukiendelea kushirikiana, tutafanya vizuri zaidi kuliko mwaka uliopita,” alisema.
Hata hivyo, Mbega alisema bado kuna meli zinazolazimika kusubiri nje ya bandari kabla ya kuingia, lakini muda wa kusubiri umepungua ikilinganishwa na ilivyokuwa awali.
Alizitaka kampuni na wadau wengine kuendelea kutumia huduma za Bandari ya Tanga na kutoa mrejesho wanapokutana na changamoto, akieleza kuwa TPA itaendelea kuboresha huduma ili kuhakikisha meli na shehena zinahudumiwa kwa wakati.
Naye Meneja wa Seafront Shipping katika Bandari ya Tanga, Amri Sufiani Kagembe, alisema kampuni hiyo imeshuhudia maboresho ya huduma za bandari, akibainisha kuwa kupungua kwa changamoto zilizokuwapo awali kumeongeza ufanisi katika kuhudumia meli na wateja.
Alisema Seafront imeendelea kuhudumia idadi kubwa ya meli katika bandari hiyo, jambo alilolitaja kuwa ishara ya imani waliyonayo katika huduma zinazotolewa.

“Tunathamini sana ‘extra mile’ inayofanywa katika Bandari ya Tanga kwa vitendo. Tunaamini huduma bora kwa mteja si kwa sababu tu ni wajibu wetu, bali kwa sababu mteja anastahili huduma bora zaidi. Hapa Tanga, tunaona hilo likitekelezwa kwa vitendo,” alisema Kagembe.
Kwa upande wake, Meneja wa CHICASA ICDV, Sofia Mfinanga, alisema wanajivunia huduma wanazopata katika Bandari ya Tanga, akieleza kuwa maboresho hayo yamechangia kuongezeka kwa wateja wanaotumia huduma za kituo hicho cha kuhifadhi na kushughulikia makontena pamoja na shughuli za biashara kwa ujumla.
“Tunajivunia sana huduma tunazozipata hapa Tanga chini ya uongozi wa Meneja wa Bandari, Salehe, na timu yake. Pia tunajivunia jinsi tunavyopata wateja na kuona ongezeko la shughuli. Tunawakaribisha wadau kutumia huduma za Bandari ya Tanga kwa sababu huduma zake ziko vizuri,” alisema Mfinanga.


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...