Maonesho ya Siku ya Chakula Duniani yanayofanyika kitaifa jijini Tanga yanatoa fursa kwa wakulima kupata elimu kuhusu matumizi sahihi ya mbolea, ubora wa pembejeo hizo na upatikanaji wa mbolea za ruzuku ili kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao na kuimarisha usalama wa chakula nchini.
Akizungumza Oktoba 11, 2026, jijini Tanga, Afisa Mdhibiti Ubora Mwandamizi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Stephano Mfugale, amesema matumizi ya mbolea yenye ubora na kuzingatia kanuni sahihi ni miongoni mwa mambo muhimu yanayochangia uzalishaji wenye tija.
Mfugale amesema TFRA inaendelea kutoa elimu kwa wakulima kuhusu uchaguzi wa mbolea sahihi, matumizi yake katika sehemu inayofaa na kwa wakati unaotakiwa kulingana na mahitaji ya mazao, hatua inayosaidia kuongeza uzalishaji na kuboresha upatikanaji wa chakula.
Aidha, amewahimiza wakulima na wadau mbalimbali kutembelea banda la TFRA katika maonesho hayo yanayofanyika katika Viwanja vya Usagara, jijini Tanga, ili kupata elimu kuhusu ubora wa mbolea, matumizi yake na fursa za biashara katika mnyororo wa thamani wa mbolea.
Kwa upande wake, Khatibu Kileka, Msimamizi wa Mbolea za Ruzuku wa TFRA Mkoa wa Tanga, amewakaribisha wakulima kutembelea banda hilo ili kupata maelekezo kuhusu upatikanaji wa mbolea za ruzuku na taratibu za kujisajili katika mfumo unaotumika kupata huduma hiyo.
Kileka amesema maonesho hayo pia ni fursa kwa wafanyabiashara, wazalishaji na wadau wengine wa sekta ya mbolea kupata ushauri kuhusu shughuli zao na taratibu za usajili wa bidhaa, huku akisisitiza umuhimu wa ushiriki wao katika kuboresha upatikanaji wa pembejeo na kuongeza tija katika uzalishaji wa chakula nchini.
Maonesho ya siku ya Chakula Duniani yanafanyika kwa muda wa siku 7, kuanzia Oktoba 10, 2026, na kilele chake ni Oktoba 16, 2026, kwenye viwanja vya shule ya sekondari Usagara, chini ya kauli mbiu isemayo "Ubunifu wa Leo, Lishe ya Kesho, Kuelekea Dira 2050".


.jpeg)

.jpeg)
.jpeg)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...