Na Seif Mangwangi, Michuzi TV, Arusha


BINTI mdogo wa Kitanzania, Elizabeth Milaho(22), ameweka historia baada ya kupata nafasi ya kuwasilisha mada kuhusu afya ya akili mbele ya wajumbe wa Mkutano wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), akitoa wito kwa Serikali na watunga sera kuwashirikisha vijana katika utengenezaji wa sera na sheria zinazolenga kukabiliana na changamoto za afya ya akili.

Elizabeth, ambaye ni mratibu wa programu katika taasisi ya Akili Tulivu yenye makao yake makuu Jijini Dar es salaam, amesema ushiriki wa vijana katika mchakato wa utungaji wa sera ni muhimu kwa kuwa wao ni miongoni mwa makundi yanayoathirika kwa kiasi kikubwa na changamoto mbalimbali za afya ya akili.

Akizungumza na wajumbe wa mkutano huo, Elizabeth amesema afya ya akili si suala linalowaathiri vijana pekee, bali linaweza kuathiri familia, uchumi na jamii kwa ujumla, hivyo linahitaji kushughulikiwa kuanzia ngazi ya chini hadi kitaifa.

Elizabeth amesema kutokana na hali hiyo, Serikali inapaswa kuweka mazingira yatakayowawezesha vijana kushiriki kikamilifu katika majadiliano na utengenezaji wa sera zinazohusu afya ya akili.

“Tunatengeneza sera ambazo zitawasaidia vijana, lakini vijana nao wanapaswa kuwa miongoni mwa washiriki wa suala zima la utengenezaji wa sheria zetu,” amesema.

Amesema vijana wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo shinikizo la kiuchumi, matatizo ya kifamilia na mazingira wanayoishi, mambo ambayo yanaweza kuwa na athari katika afya yao ya akili.

Ameongeza kuwa maendeleo ya teknolojia za kidijitali yameleta changamoto nyingine, kwa kuwa vijana ni miongoni mwa watumiaji wakubwa wa teknolojia hizo na hukutana na mazingira mbalimbali yanayoweza kuathiri ustawi wao wa kisaikolojia.

Elizabeth amesema taasisi ya Akili Tulivu ilianzishwa Tanzania kwa lengo la kuwasaidia vijana kukabiliana na changamoto za afya ya akili, huku mpango huo ukiendelea kupanuka na kufikia maeneo mbalimbali duniani.

“Akili Tulivu inatoa jukwaa salama na lenye faragha linalowawezesha vijana kueleza changamoto wanazopitia na kutafuta msaada unaohitajika kwa kutumia Kiswahili au Kiingereza,” amesema

Amesema fursa ya kuwasilisha mada hiyo katika Mkutano wa IPU imemuwezesha kufikisha ujumbe wa vijana mbele ya viongozi na wawakilishi wa mabunge kutoka mataifa mbalimbali duniani.

Kwa mujibu wa Elizabeth, viongozi hao wana nafasi muhimu katika kutengeneza sera na sheria, hivyo ni muhimu wao kuelewa changamoto halisi zinazowakabili vijana katika masuala ya afya ya akili.

Amesema ujumbe uliowasilishwa kupitia Akili Tulivu umepokelewa vyema, huku akieleza matumaini kwamba hatua zaidi zitachukuliwa kuweka mazingira bora ya kushughulikia changamoto za afya ya akili kabla hazijawa kubwa na kusababisha madhara zaidi katika jamii.

Elizabeth amesema sababu kubwa ya kuanza na vijana ni kwamba kundi hilo ndilo linalotarajiwa kuwa viongozi, watunga sera na waamuzi wa masuala mbalimbali ya nchi katika siku zijazo.

“Tunategemea vijana hawa baadaye kuwa viongozi, kutengeneza sera na kuwa watu watakaokuwa wanaongoza nchi yetu. Kwa hiyo tunahitaji kuanza kuwasaidia mapema,” amesema.

Amewataka vijana kutokuwa na hofu ya kuzungumza kuhusu changamoto wanazopitia, akisisitiza umuhimu wa kutafuta watu sahihi wa kuwaeleza pale wanapokabiliwa na changamoto za afya ya akili.

Amesema vijana wanapaswa kutumia fursa zilizopo katika shule, vyuo vikuu na ngazi nyingine za jamii kuzungumzia changamoto zinazowakabili, ili kujenga jamii inayotambua afya ya akili kama sehemu muhimu ya maendeleo ya kizazi cha sasa na kijacho.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...