Na Janeth Raphael - MichuziTv

Tanzania inatarajiwa kuwa kitovu cha mijadala kuhusu maendeleo ya vyama vya ushirika wa akiba na mikopo barani Afrika kupitia Kongamano la 26 la Vyama vya Ushirika wa Akiba na Mikopo Afrika (SACCA Congress 2026), litakalofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Oktoba 11 hadi 16, 2026, katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC).

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma leo ,Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo, amesema kongamano hilo linatarajiwa kuwakutanisha zaidi ya washiriki 1,000 kutoka nchi zaidi ya 40 za Afrika na maeneo mengine duniani, likilenga kuimarisha ushirikiano na kubadilishana uzoefu katika sekta ya ushirika wa kifedha.

Amesema Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa kongamano hilo lenye kaulimbiu isemayo “Building Trust, Driving Transformation: The Future of Financial Cooperatives in Africa”, inayosisitiza kujenga uaminifu na kuleta mabadiliko katika mustakabali wa vyama vya ushirika wa kifedha barani Afrika.

Kwa mujibu wa Chongolo, kongamano hilo litaiwezesha Tanzania kujifunza mbinu bora za uendeshaji wa SACCOS, kuimarisha uwezo wa taasisi hizo na kufungua fursa mpya za uwekezaji. Ameeleza kuwa huduma za kifedha kupitia SACCOS zina nafasi muhimu katika kuwawezesha wakulima, vijana, wanawake na wafanyabiashara wadogo kupata huduma zinazoweza kuchochea shughuli zao za kiuchumi.

Aidha, amesema Tanzania itanufaika na fursa za kutangaza utalii, utamaduni na mazingira ya uwekezaji kwa wageni watakaohudhuria kongamano hilo, hatua inayoweza kuongeza mwamko wa washiriki kuhusu vivutio na fursa zilizopo nchini.

Kwa upande wake, Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania, Dkt. Benson Ndiege, amesema maandalizi ya kongamano hilo yanaipa Tanzania nafasi ya kuimarisha uhusiano na wadau wa kimataifa, kuvutia uwekezaji na kujifunza uzoefu wa nchi nyingine katika kuendeleza vyama vya ushirika.

Dkt. Ndiege amesema zaidi ya washiriki 600 wanatarajiwa kutoka nje ya Tanzania, jambo litakaloongeza fursa za kibiashara na kutoa mchango kwa sekta ya utalii kupitia matumizi ya huduma za hoteli, usafiri na biashara nyingine wakati wa kongamano hilo.

Ameongeza kuwa wageni hao watapata nafasi ya kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii, vikiwemo vilivyopo Dar es Salaam, Morogoro, Ngorongoro na Zanzibar, hali inayotarajiwa kuchochea shughuli za kiuchumi na kuitangaza Tanzania kimataifa.

Amesema kongamano hilo pia litatoa fursa ya kujengeana uwezo kwa vyama vya ushirika nchini kupitia mijadala na mafunzo kuhusu utawala bora, usimamizi wa vyama na mikakati ya kuimarisha maendeleo ya SACCOS. Vilevile, Tanzania itapata jukwaa la kuonesha mafanikio iliyoyapata katika sekta ya ushirika na kujifunza maeneo yanayohitaji maboresho.

Kwa mujibu wa Dkt. Ndiege, Tanzania kupewa nafasi ya kuandaa kongamano hilo ni ishara ya kutambulika kwa maendeleo ya sekta ya ushirika nchini na nafasi yake katika majukwaa ya kimataifa.

Waziri Chongolo ametoa wito kwa wadau wa vyama vya ushirika, washiriki kutoka Afrika na sehemu nyingine duniani kushiriki kongamano hilo, akieleza kuwa litakuwa jukwaa muhimu la kujenga mitandao ya ushirikiano, kukuza uwekezaji, kutangaza utalii na kuimarisha mchango wa SACCOS katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii.




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...