Na Seif Mangwangi, Michuzi TV, Arusha
WASANII nchini wametakiwa kubadili mtazamo na kuanza kuzitazama kazi zao za sanaa kama biashara kwa kuzirasimisha, kusajili majina ya biashara na kulinda miliki bunifu ili kuongeza fursa za kukuza shughuli zao na ushindani katika soko.
Wito huo umetolewa na Msaidizi wa Msajili Mkuu, Mkurugenzi wa Miliki Bunifu kutoka Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Nassoro Mtavu, aliyewahimiza wasanii kutumia fursa zinazopatikana kupitia usajili na ulinzi wa kazi zao.
Mtavu ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na wadau wa sanaa katika Tamasha la Arusha Artisan Festival linaloendelea katika viwanja vya General Tyre, Njiro jijini Arusha.
Amesema BRELA imejipanga kuwasaidia wasanii kuelewa taratibu za usajili wa biashara pamoja na masuala ya majina ya biashara, alama za biashara na miliki bunifu yanayoweza kuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya sekta ya sanaa.
Amesema ushiriki wa BRELA katika tamasha hilo unalenga kutoa elimu kwa wasanii na wafanyabiashara kuhusu umuhimu wa kurasimisha shughuli zao na kuhakikisha wanafanya biashara kwa kuzingatia matakwa ya sheria.
“Maonyesho haya yamekuwa fursa muhimu kwa wasanii na wafanyabiashara kupata elimu kuhusu namna ya kuendesha na kukuza shughuli zao kwa kuzingatia taratibu za kisheria,” amesema Mtavu.
Amesema wasanii wanapaswa kutumia nafasi hiyo kuuliza maswali na kueleza changamoto zinazowakabili katika shughuli zao ili kupata majibu na ushauri kutoka kwa wataalamu wa BRELA.
Kwa mujibu wa Mtavu, baadhi ya changamoto zinazowakabili wasanii zinaweza kutatuliwa iwapo wataongeza uelewa kuhusu usajili wa biashara, majina ya biashara, alama za biashara pamoja na namna ya kulinda miliki bunifu.
Amesema usajili wa shughuli za sanaa unaweza kuwasaidia wasanii kuwa na utambulisho rasmi wa kibiashara na hivyo kuongeza uwezo wao wa kutumia fursa mbalimbali zinazopatikana kwa wafanyabiashara waliosajiliwa.
Aidha, amesema ulinzi wa miliki bunifu ni muhimu kwa wasanii kwa kuwa kazi zao zinaweza kuwa na thamani kubwa kiuchumi na hivyo zinahitaji kulindwa dhidi ya matumizi yasiyoruhusiwa.
Mtavu amewataka wasanii kutumia mafunzo na huduma zinazotolewa na BRELA kama sehemu ya kujenga msingi imara wa biashara zao badala ya kutegemea kipaji pekee katika kuendesha shughuli zao.
Amesema msanii anayelinda kazi yake, anasajili shughuli zake na kuzingatia taratibu za kisheria ana nafasi kubwa ya kukuza thamani ya kazi zake na kufikia masoko mapana zaidi.
Ameongeza kuwa wasanii wanapaswa kutumia majukwaa kama Tamasha la Arusha Artisan Festival si kwa ajili ya kuuza na kutangaza kazi zao pekee, bali pia kujifunza namna ya kuzifanya kazi hizo kuwa biashara endelevu.
Amesema BRELA itaendelea kushirikiana na wadau wa sanaa kutoa elimu na kuwasaidia kuelewa huduma zinazotolewa na taasisi hiyo ili waweze kutumia ipasavyo fursa zilizopo.
Mtavu amewahimiza wasanii wengine ambao bado hawajar formalisha shughuli zao kuchukua hatua kwa kuanza mchakato wa usajili na kupata uelewa kuhusu namna bora ya kulinda kazi zao.
Amesema hatua hiyo itasaidia kujenga sekta ya sanaa yenye wasanii wanaoweza kutumia ubunifu wao kama chanzo cha ajira, kipato na biashara endelevu nchini.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...