Na Mwandishi Wetu.

Rome, Italia. Tarehe 4 Oktoba 2026: Taasisi ya CRDB Bank Foundation imeendelea kujiimarisha kama daraja muhimu la mitaji ya kimataifa na jamii ambazo hazijafikiwa ipasavyo na huduma za fedha, baada ya kushiriki mkutano unaojadili Ufadhili Mseto wa Miradi yaani Blended Finance Working Group (BFWG) ulioandaliwa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) kujadili namna ya kuongeza upatikanaji wa fedha kwa wananchi na biashara za vijijini. 

Akishiriki mkutano huo uliowajumuisha wadau wengine ukiwamo Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD), Benki ya Dunia, Benki ya Maendeleo ya Ujasiriamali ya Uholanzi (FMO), Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP), pamoja na wadau wa maendeleo, taasisi za fedha na wataalamu wa sekta mbalimbali, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa amesema mikakati ya pamoja inahitajika kuwafikia wananchi wenye uhitaji wa mitaji nafuu ili nao washiriki kuujenga uchumi wa mataifa yao.

Akizungumza pembezoni mwa mkutano huo, Tully amesema CRDB Bank Foundation ipo katika nafasi ya kipekee ya kuunganisha rasilimali za kimataifa na fursa zilizopo katika jamii kwa sababu ya uelewa wake wa kina kuhusu mahitaji ya wananchi wa vijijini pamoja na dhamira yake ya muda mrefu ya kukuza ujumuishaji wa kiuchumi.

"Upatikanaji wa fedha bado ni moja ya changamoto kubwa kwa jamii za vijijini na biashara ndogondogo. Kupitia uzoefu wetu chini ya Programu ya iMBEJU Kilimo, tumedhihirisha kuwa ushirikiano sahihi na mifumo bunifu ya ufadhili, inaweza kurahisisha namna kuwafikia wananchi ambao mara nyingi huonekana kutofikika na huduma za kifedha na kuwasaidia kuwa washiriki wenye tija katika uchumi," amesema.

Majadiliano ya mkutano huo yalijikita katika kutafuta majibu ya swali muhimu kuhusu namna ya kuhamasisha na kuelekeza mitaji zaidi kwa jamii, wakulima na biashara zinazohitaji fedha ili kukuza shughuli zao za kiuchumi hivyo kutoa fursa kwa washiriki kubadilishana uzoefu kuhusu mchango wa mifumo ya ufadhili mseto (blended finance), dhamana za mikopo, na nafasi ya taasisi imara za fedha katika kuvutia uwekezaji mkubwa zaidi kwenye sekta za kilimo na maendeleo ya biashara za vijijini.

Majadiliano hayo pia yalisisitiza umuhimu wa kuziba pengo lililopo kati ya wawekezaji wa kimataifa na jamii nyingi ambazo bado zimeendelea kubaki nje ya mifumo rasmi ya fedha.

Kwa CRDB Bank Foundation, ushiriki katika mikutano ya BFWG umetoa jukwaa muhimu la kushirikisha uzoefu wa Tanzania katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kimkakati unaoweza kuleta vyanzo vipya vya mitaji karibu zaidi na wajasiriamali wa vijijini, wakulima na biashara zinazomilikiwa na jamii.

Zaidi ya hayo, Foundation inaendelea kuonyesha dhamira yake ya kuziba mapengo ya upatikanaji wa huduma muhimu za maendeleo kama inavyofanya sasa kupitia programu ya iMBEJU Nuru, inayotekelezwa kwa ushirikiano na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa kutoa ruzuku za gharama za kuunganishiwa umeme kwa jamii za vijijini ambazo zina changamoto ya upatikanaji wa huduma hiyo muhimu.
Kupitia mipango kama hii, CRDB Bank Foundation inaendelea kuhimiza matumizi ya mifumo bunifu ya ufadhili inayounganisha mitaji kutoka sekta ya umma, sekta binafsi na taasisi za maendeleo ili kupunguza vihatarishi vya uwekezaji, kuongeza upatikanaji wa huduma muhimu na kuweka msingi thabiti wa ukuaji wa uchumi shirikishi.

Kwa kushirikiana na taasisi za maendeleo za kimataifa na wadau wa kifedha, Foundation inalenga kuharakisha upatikanaji wa fedha kwa miradi na biashara zinazochochea ajira, kuimarisha uhakika wa chakula na kujenga uchumi imara na endelevu katika maeneo ya vijijini.

Ushiriki wa CRDB Bank Foundation katika mkutano huo wa Rome ni sehemu ya utekelezaji wa dira ya kuchochea maendeleo jumuishi kwa kuunganisha mitaji na fursa zilizopo katika jamii. Wakati majadiliano ya kimataifa kuhusu maendeleo jumuishi na ufadhili endelevu yakiendelea, CRDB Bank Foundation inaendelea kuelekeza nguvu zake katika kubadili ushirikiano kuwa miradi inayotekelezeka, na miradi hiyo kuwa matokeo halisi yanayogusa maisha ya mamilioni ya wananchi wa vijijini nchini Tanzania na kwingineko.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...