Na Mwandishi Wetu, Masasi

Msimu wa Korosho 2026/2027 umezinduliwa rasmi wilayani Masasi, huku viongozi wa Vyama vya Ushirika vya Msingi (AMCOS) wakitakiwa kuwa waadilifu na kutohujumu zao hilo, kwa kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watakaobainika kufanya hivyo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa msimu huo kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Masasi, Emmanuel Shilatu, amesema Serikali haitamvumilia mtu yeyote atakayehujumu zao la korosho au kufanya vitendo vinavyoweza kuwarudisha nyuma wakulima.

Shilatu ameyasema hayo katika kikao cha uzinduzi wa msimu wa Korosho 2026/2027 kilichowakutanisha wadau mbalimbali wa zao hilo.

Amesema wakulima wa korosho wanamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi zake za kuhakikisha zao hilo linapewa heshima na kuendelea kuwa na mchango mkubwa katika uchumi wa nchi.


“Serikali haitamvumilia mtu yeyote atakayefanya mzaha au kujaribu kuhujumu kazi nzuri iliyofanywa na Rais Samia kwa kutaka kulihujumu zao la korosho kwa namna yoyote ile. Hatua kali zitachukuliwa dhidi yake, ikiwemo adhabu ya kifungo,” amesema Shilatu.

Kwa upande wake, Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Mtwara, Robert Nsunza, amewataka makarani wanaohusika katika shughuli za ununuzi wa korosho kuhakikisha wanatumia mizani ya kidijitali, kuzingatia ubora wa zao na kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu.

Naye Kiongozi wa Chama Kikuu cha Ushirika cha MAMCU, Biadia Matipa, amesema chama hicho kimejipanga kikamilifu kuhakikisha msimu wa Korosho 2026/2027 unakwenda vizuri.

Matipa amesema maandalizi yote yamekamilika na ameahidi kuhakikisha wakulima wanalipwa fedha zao kwa wakati, akieleza kuwa lengo ni kuhakikisha malipo yanafanyika ndani ya siku saba tangu kufanyika kwa mnada.

Kwa upande wao, viongozi wa AMCOS wameahidi kufanya kazi kwa uadilifu na kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa weledi ili msimu wa Korosho 2026/2027 uwe na tija kwa wakulima na wadau wote wa zao hilo.




Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...