Mwamvua Mwinyi, Kibiti

MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti, mkoani Pwani, Ramadhan Kimara, amewataka mafundi na wasimamizi wa miradi ya maendeleo kuhakikisha kazi zinakamilika kwa wakati, kwa kuzingatia mikataba na matumizi sahihi ya vifaa vya ujenzi.

Kimara ametoa maelekezo hayo Oktoba 12, 2026, wakati akikagua ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Mkupuka yenye thamani ya Sh milioni 528, iliyopo katika Kijiji cha Mkupuka wilayani Kibiti.

Akiwa katika eneo la mradi huo, Kimara amezungumza na fundi pamoja na msimamizi wa ghala la vifaa vya ujenzi, akiwataka kuhakikisha vifaa vinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na kazi inakamilika ndani ya muda uliowekwa kwenye mkataba.

Aidha, amemtaka Mhandisi wa mradi kutembelea eneo la ujenzi mara kwa mara ili kufuatilia maendeleo ya kazi na kushughulikia changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa utekelezaji.

“Mjulisheni Mhandisi wa mradi ahakikishe muda wote anafika katika eneo la ujenzi ili kusiwe na changamoto zozote katika ujenzi huu,” amesisitiza Kimara.

Katika ziara hiyo, Kimara pia ametembelea Kijiji cha Nyamisati, Kata ya Salale, ambako amekagua Kiwanda cha Samaki kwa lengo la kujionea hali ya miundombinu iliyopo na kubaini changamoto zinazokikabili.

Ukaguzi wa kiwanda hicho ulilenga kutathmini hali yake na kubaini maeneo yanayohitaji kufanyiwa kazi ili kuwezesha shughuli za uzalishaji kuanza au kuimarishwa.

Hatua hiyo inalenga kuongeza mapato ya Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti, kukuza uwekezaji na kuchochea shughuli za kiuchumi zitakazochangia maendeleo ya wilaya hiyo.









Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...