Naibu  Waziri wa Kilimo, David Silinde (Mb) ameipongeza Wakala wa Taifa ya Huduma za Ugani (NAESA) kwa kazi zinazofanywa kusaidia Wizara ya Kilimo kutekeleza majukumu yake, huku akifurahishwa na teknolojia ya uchakataji wa mpunga kwa kutumia mvuke inayosaidia kupata mchele wenye ubora na kupunguza kuvunjika kwa punje wakati wa kusaga.

Silinde ametoa pongezi hizo Oktoba 12, 2026, alipotembelea banda la NAESA katika maadhimisho ya kitaifa ya kuelekea Siku ya Chakula Duniani, yaliyofanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari Usagara, jijini Tanga, ambapo alijionea teknolojia mbalimbali zinazolenga kuongeza thamani ya mazao na kuboresha uzalishaji wa chakula.

Amesema kuanzishwa kwa NAESA kuna umuhimu mkubwa katika kusaidia utekelezaji wa majukumu ya Wizara ya Kilimo, hususan kuratibu na kusimamia  huduma za ugani nchini na kuhakikisha wakulima wanapata elimu, teknolojia na ushauri wa kitaalamu unaoweza kuongeza tija katika uzalishaji.

Akizungumzia teknolojia ya uchakataji wa mpunga kwa kutumia mvuke (parboiling), Silinde amefurahishwa na namna mfumo huo unavyosaidia kuimarisha punje za mchele na kupunguza kuvunjika kwake wakati wa kusaga, hatua inayoweza kumwezesha mkulima kuongeza thamani ya mazao yake na kupata manufaa zaidi kiuchumi.

Katika hatua nyingine, ameitaka NAESA kuimarisha usimamizi wa huduma za ugani nchini na kuwasilisha taarifa kwa Wizara ya Kilimo kila wiki kuhusu mwenendo wa shughuli za kilimo katika maeneo mbalimbali, ili kubaini changamoto zinazowakabili wakulima na kuwezesha hatua za haraka kulingana na mahitaji halisi ya maeneo husika.

Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Sehemu ya Masoko na Uongezaji Thamani ya Mazao wa NAESA, Bi. Esther Mwaisango, amesema taasisi hiyo imeanzishwa kwa mujibu wa sheria na wamejipanga kuhakikisha wanaongeza tija kwenye uzalishaji ili upatikanaji wa chakula uwe mzuri.

Aidha Mwaisango amesema  NAESA imeshiriki maadhimisho hayo kuonyesha teknolojia mbalimbali za usindikaji wa mazao na kuwafahamisha wananchi namna zinavyoweza kutumika kuongeza thamani ya mazao ya kilimo.

Aidha Bi. Mwaisango amesema NAESA inaendelea kuandaa mafunzo kwa maafisa ugani katika halmashauri mbalimbali kuhusu tafsiri ya taarifa za mvua na namna ya kuzitumia kutoa ushauri sahihi kwa wakulima.

Akielezea teknolojia ya uchakataji wa mpunga kwa kutumia mvuke, Mkufunzi kutoka Chuo cha Uhaulishaji Teknolojia za Kilimo (MATI Ilonga), Kilosa mkoani Morogoro, Bw. Hamis Abdalah Ramadhani, amesema mfumo huo unahusisha kuloweka mpunga kabla ya kuupitisha kwenye mchakato wa mvuke, unaosaidia kuimarisha punje na kupunguza kuvunjika wakati wa kusaga.









Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...