Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) nchini Tanzania limesema maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani mwaka huu yataweka mkazo katika kutambua na kuenzi mchango wa mwanamke mkulima katika uzalishaji wa chakula, biashara ya kilimo na kuboresha lishe katika kaya.

Akizungumza na Waandishi wa habari Oktoba 13, 2026, Jijini Tanga, Jane Mstagati, Mtaalamu wa Masuala ya Jinsia kutoka FAO Tanzania, mara baada ya Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Prof. Peter Msofe, kutembelea Banda la Umoja wa Taifa, amesema mwanamke ana nafasi kubwa katika kuhakikisha chakula kinapatikana na kuandaliwa nyumbani, huku akishiriki kwa kiwango kikubwa katika shughuli za uzalishaji mashambani.

Amesema maadhimisho hayo yanalenga kutambua wanawake wanaofanya vizuri katika kilimo, kwa kuzingatia mchango wao katika kuzalisha chakula cha kutosha kwa familia na jamii, kushiriki katika biashara ya kilimo pamoja na ufugaji wa mifugo inayozalisha maziwa na mayai.

Mstagati amesema FAO kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo na Mkoa wa Tanga, ilitumia vigezo mbalimbali kuwapata wanawake vinara wa kilimo, ikiwemo uzalishaji wa mboga mboga za aina mbalimbali na matumizi ya mbolea za asili zinazolenga kupunguza madhara yanayoweza kusababishwa na matumizi ya kemikali.

Amesema kabla ya kilele cha maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani, Oktoba 16, 2026, kutakuwa na hafla ya kuwatambua na kuwapongeza wanawake vinara wa kilimo Oktoba 15, mwaka huu, jijini Tanga, ambapo tuzo zitatolewa kwa wanawake waliofanya vizuri katika sekta hiyo.

Wanawake hao wanajumuisha wanaojihusisha na kilimo cha mboga mboga, ufugaji wa ng’ombe, kuku na mbuzi, pamoja na shughuli nyingine katika mnyororo wa thamani wa kilimo.

Ameeleza kuwa mmoja wa wanawake watakaotambuliwa atashiriki katika mdahalo utakaolenga kujadili changamoto na fursa zilizopo katika kilimo, mchango wa ubunifu katika kuboresha upatikanaji wa chakula na lishe, pamoja na namna wanaume na Serikali wanavyoweza kumuunga mkono mwanamke mkulima.

Amesisitiza kuwa upatikanaji wa chakula cha kutosha pekee hautoshi kuhakikisha lishe bora, kwani maandalizi ya chakula, mgawanyo wa rasilimali na maamuzi ndani ya kaya pia vina mchango mkubwa katika hali ya lishe ya familia.





Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...