MPANDA, KATAVI
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo imesema haitakaa kimya kuzungumzia mafanikio yanayopatikana katika miradi ya umwagiliaji nchini, ikieleza kuwa imejiridhisha na kazi kubwa inayofanywa na Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuendeleza sekta ya kilimo.
Kamati hiyo imesema uwekezaji mkubwa unaofanywa katika miradi ya umwagiliaji umeanza kuleta mabadiliko kwa wakulima na kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao.
Akizungumza mkoani Katavi wakati wa ziara ya siku tano ya Kamati hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, ambaye pia ni Mbunge wa Njombe Mjini, Mhe. Deodatus Philip Mwanyika, amesema wamejionea kazi kubwa inayofanyika katika Mradi wa Umwagiliaji Mwamkulu.
“Ukweli usemwe na hatutakubali kukaa kimya na kufunga midomo. Miradi hii, kwa kazi kubwa iliyofanywa na Rais Dkt. Samia, ni lazima ionekane na mahali panapofanya vizuri, maneno ni lazima yawepo,” amesema Mwanyika.
Amesema kwa muda mrefu kaulimbiu imekuwa ikisema kilimo ni uti wa mgongo wa Taifa, lakini Serikali ya Awamu ya Sita imeanza kuifanya kauli hiyo ionekane kwa vitendo kupitia uwekezaji katika miundombinu ya umwagiliaji.
“Kilimo kilikuwepo tangu wakati huo na kauli mbiu ilikuwa Kilimo ni Uti wa Mgongo, lakini Rais Samia amekuja kutafsiri na kuonekana kilimo kweli ni uti wa mgongo. Hii miradi ya umwagiliaji inaenda kugusa wakulima na wananchi moja kwa moja na hatutasita kuwasemea pale inapofanya vizuri,” amesema.
Mwanyika amesema Mradi wa Umwagiliaji Mwamkulu wenye thamani ya Sh bilioni 33.9 unaotekelezwa katika Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda unatarajiwa kubadilisha maisha ya wakulima wa eneo hilo kwa kuwaondolea changamoto walizokabiliana nazo kwa miaka mingi.
Kwa mujibu wa Mwanyika, utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 83, huku mfereji mkuu wa maji wenye urefu wa kilomita 7.7 ukikamilika kwa asilimia 100.
Amesema mifereji mingine mikuu mitatu yenye jumla ya kilomita 14 imekamilika, pamoja na barabara za mashambani zenye urefu wa kilomita 35 na mifereji ya kurudisha maji katika Mto Katuma yenye urefu wa kilomita 18.
Aidha, amesema ujenzi wa ghala la kuhifadhi nafaka lenye uwezo wa tani 4,000 umefikia zaidi ya asilimia 90, hatua inayolenga kupunguza upotevu wa mazao baada ya kuvuna.
Mwanyika amesema wakati Tanzania ikiweka lengo la kulisha dunia, Katavi ni mkoa wa kimkakati katika uzalishaji wa mazao, hususan mpunga na mahindi, hivyo amewataka wananchi kutumia fursa hiyo na kutunza miundombinu inayojengwa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mhe. Mwanamvua Mrindoko, amesema mkoa huo ambao zaidi ya asilimia 95 ya wananchi wake wanategemea kilimo, umepokea takriban Sh trilioni 1.4 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi katika sekta mbalimbali, huku Sh bilioni 70 zikitengwa kwa ajili ya umwagiliaji.
Amesema Mradi wa Mwamkulu ni hatua kubwa katika kukuza kilimo cha umwagiliaji mkoani humo, huku akiomba mabonde mengine nayo yaendelezwe ili kuongeza uzalishaji na tija kwa wakulima.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Mhe. Jamila Yusuph, amesema mradi huo umeleta matumaini makubwa kwa wananchi na unatarajiwa kuongeza mapato ya Halmashauri.
Amesema Wilaya imewashirikisha viongozi wa dini, wazee, vijana wa bodaboda pamoja na vyama vya siasa kutembelea na kujionea uwekezaji huo wa Serikali, huku akiomba kukamilishwa kwa bwawa la kuhifadhi maji ili kuwawezesha wananchi kulima mara mbili kwa mwaka.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo anayeshughulikia Umwagiliaji na Zana za Kilimo, Eng. Athuman Kilundumya, ameahidi kuwa Tume itaendelea kushirikiana na jamii katika kuhakikisha miradi hiyo inaleta matokeo chanya, huku Wizara ikiendelea kuiwezesha taasisi hiyo kufikia malengo ya Serikali.
Kuhusu upatikanaji wa mbegu, Kilundumya ameitaka Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC) na Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) kuweka kambi katika eneo la Mradi wa Umwagiliaji Mwamkulu ili kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wakulima.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Raymond Mndolwa, amesema mikataba ya Tume hiyo haina gharama za riba, hatua ambayo imeiwezesha Serikali kuokoa zaidi ya Sh bilioni 28 ambazo zingetumika kulipa riba.
Mndolwa amesema kutokana na athari za El Niño zinazotarajiwa, Tume imemuelekeza mkandarasi wa mradi huo kuhakikisha anakamilisha kwa wakati na kwa ubora kazi za mashambani kabla ya kukamilisha majengo ya utawala, ili kuwalinda wakulima dhidi ya madhara yanayoweza kujitokeza.
Amesema Tume ipo katika mchakato wa kupata mashine zitakazofungwa katika ghala la mpunga lililojengwa katika mradi huo, ili kuwawezesha wananchi kuchakata mazao yao katika eneo hilo.
Aidha, ameupongeza uongozi wa mkoa na wilaya kwa ushirikiano wanaoutoa katika kutoa elimu kwa wakulima na kusimamia ukusanyaji wa tozo za ada za umwagiliaji.
Kwa niaba ya Mwenyekiti wa skimu na wakulima wa eneo hilo, Mzee Boniphace Chidesela, amesema mradi huo umebadilisha maisha ya wakulima, akieleza kuwa kabla ya mradi walitumia kati ya saa nne na tano kufika mashambani na walilipa Sh10,000 kusafirisha gunia moja la mazao.
“Hivi sasa magari yanafika hadi shambani, gharama imeshuka hadi Sh1,000 na safari inachukua dakika 15 tu,” amesema.
Uwekezaji huo unatarajiwa kuongeza uzalishaji wa mpunga kutoka wastani wa magunia 20 hadi 35–40 kwa ekari, huku idadi ya wanufaika ikitarajiwa kuongezeka kutoka wakulima 300 hadi 1,500.
Akihitimisha ziara hiyo, Mwanyika amempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka nguvu kubwa katika sekta ya kilimo, akisema Mradi wa Umwagiliaji Mwamkulu unaonyesha thamani halisi ya fedha za umma (Value for Money).


.jpeg)

.jpeg)




.jpeg)
.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...