Na Ashura Mohamed, Arusha

Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limesema litaendelea kuimarisha uwekezaji katika miundombinu ya mawasiliano na huduma za kidijitali,kama nyenzo muhimu ya kukuza uchumi wa kidijitali na kufanikisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Akizungumza Jana Jijini Arusha kwenye Kongamano la Wenyeviti wa Bodi na Maofisa Watendaji Wakuu (C-CEOs) wa taasisi za umma, Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Moremi Marwa, alisema shirika hilo lina jukumu kubwa la kujenga msingi imara wa mageuzi ya kidijitali nchini.

Marwa alisema uwekezaji unaofanywa na TTCL, ikiwemo Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, vituo vya kuhifadhi data na minara ya mawasiliano, unalenga kuhakikisha huduma za kidijitali zinapatikana kwa uhakika kote nchini.

"Miundombinu ya mawasiliano yenye uhakika ndiyo msingi wa uchumi wa kidijitali. Bila mawasiliano ya uhakika, hatuwezi kufikia malengo tuliyojiwekea kama taifa,"alisema Marwa.

Alifafanua kuwa Dira ya Maendeleo ya 2050 inalenga kuhakikisha asilimia 80 ya huduma za Serikali zinatolewa kidijitali na asilimia 70 ya Watanzania wanatumia huduma hizo ifikapo mwaka 2050, jambo linalohitaji uwekezaji endelevu katika sekta ya mawasiliano.

"TTCL kama taasisi ya kitaifa ina jukumu la kuwezesha utekelezaji wa Dira 2050. Jukumu letu limejikita katika kuhakikisha mawasiliano yanakuwa kiungo muhimu kinachounganisha taasisi za Serikali, wafanyabiashara na wananchi," aliongeza.

Aidha, Marwa alisema miundombinu hiyo itasaidia kujenga mazingira wezeshi kwa taasisi za umma na sekta binafsi kuboresha utoaji wa huduma, kuongeza tija na kupanua wigo wa matumizi ya majukwaa ya kidijitali.

Alisisitiza kuwa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ni uti wa mgongo wa huduma za kidijitali nchini, huku vituo vya data vikiwa na mchango mkubwa katika kuhifadhi, kusimamia na kuhakikisha usalama wa taarifa.

"Kufikia malengo ya Dira 2050 kunahitaji ushirikiano wa dhati miongoni mwa taasisi za umma na uelewa wa pamoja wa wajibu wetu katika mageuzi ya uchumi wa kidijitali," alisema.

Marwa alihitimisha kwa kusema TTCL itaendelea kuwekeza kwa kasi katika miundombinu ya kisasa ili kuhakikisha Tanzania inakuwa na msingi imara wa kidijitali utakaowezesha taifa kufikia maendeleo endelevu yanayolengwa.





Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...