NAIBU Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia Masuala ya Afrika Mashariki, James Kinyasi Millya, ametoa wito wa kuimarishwa kwa uangalizi wa uchaguzi unaozingatia weledi, kutokuwa na upendeleo na ushahidi ili kuimarisha demokrasia, amani na utulivu barani Afrika.

Millya ametoa wito huo leo, Oktoba 11, 2026, wakati wa ufunguzi wa pamoja wa mafunzo ya rejea ya Umoja wa Afrika (AU) kwa wataalamu wa timu kuu na timu saidizi pamoja na waangalizi wa muda mfupi wa uchaguzi, wakiwemo wanawake na vijana, yanayofanyika jijini Dar es Salaam.

Amesema mafunzo hayo ni uwekezaji muhimu katika kuimarisha demokrasia barani Afrika, akisisitiza kuwa waangalizi wa uchaguzi wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia uadilifu, uhuru na weledi, huku wakitegemea ukweli na ushahidi wa kuaminika katika tathmini zao.

Ameeleza kuwa maendeleo ya teknolojia, akili unde na matumizi ya mitandao ya kijamii yanaendelea kubadilisha michakato ya uchaguzi, huku kuenea kwa taarifa potofu na za kupotosha pamoja na kuongezeka kwa mgawanyiko wa kisiasa kukileta changamoto mpya zinazohitaji kuboreshwa kwa ujuzi na mbinu za uangalizi wa uchaguzi.

Aidha, Millya amesisitiza umuhimu wa kuongeza ushiriki wa wanawake na vijana katika utawala wa kidemokrasia, akieleza kuwa mpango huo wa Umoja wa Afrika ni hatua muhimu katika kujenga kundi la waangalizi wa uchaguzi la Kiafrika lenye uwakilishi mpana na shirikishi.

Amesema ushiriki wa makundi hayo ni muhimu katika kuimarisha michakato ya kidemokrasia na kuhakikisha uangalizi wa uchaguzi unazingatia mitazamo na mahitaji ya watu kutoka makundi mbalimbali ya jamii.

Katika hatua nyingine, Millya amesisitiza dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuendeleza ushiriki wa wanawake na vijana katika ajenda ya kuunganisha Afrika, amani na usalama, pamoja na kukuza biashara kupitia Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA).

Ameeleza kuwa Tanzania itaendelea kuunga mkono utawala bora wa kidemokrasia na ushirikiano wa Afrika, huku akiwahimiza washiriki wa mafunzo hayo kutumia maarifa na ujuzi watakaoupata kuendeleza michakato ya uchaguzi yenye amani, inayoaminika na inayoshirikisha wananchi wote barani humo.


































Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...