Wasanii wa tasnia mbalimbali wakiwemo wa vichekesho, Wanamuziki, Wanamichezo na Watu wenye ushawishi nchini wametajwa kuwa ni nyenzo na nguzo muhimu katika kukuza, kuimarisha na kuenzi misingi ya Muungano.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Richard Muyungi wakati akifungua kikao kati ya Ofisi hiyo na Wadau hao kilicholenga kujadili mpango wa elimu kwa umma kuhusu Muungano kilichofanyika jijini Dar es Salaam Oktoba 19, 2026.

Alisema kuwa wadau hao ni kundi muhimu lenye uwezo wa kujenga ushawishi na kuhamasisha jamii, hivyo Ofisi hiyo imekusudia kutumia majukwaa yao ili kufikisha elimu ya Muungano kwa makundi mbalimbali ikiwemo vijana.

“Vipaji vyenu ni nyenzo muhimu ya kufikisha elimu ya Muungano…Tunapaswa kutambua kuwa Muungano wetu ni historia ambayo jamii hususani vijana inapaswa kutambua tulipo, tulipotoka na tunapokwenda” alisema Dkt. Muyungi.

Alieleza kuwa kwa kutambua umuhimu wa elimu kuhusu historia, misingi na chimbuko la Muungano, Ofisi ya Makamu wa Rais imekusudia kuwatumia wasanii, waigizaji na watu wenye ushawishi ambao wamekuwa na wafuatiliaji wengi hususani vijana katika mitandao ya kijamii.

Aidha, Katibu Mkuu huyo alisema maudhui yanayoandaliwa na kundi hilo yamekuwa yakivuta hisia na hamasa kwa vijana, hivyo Ofisi hiyo imebaini nafasi hiyo kuwa ni nyenzo na nguzo muhimu katika kufikisha elimu ya Muungano kwa jamii.

“Hili ni kundi muhimu katika jamii, vipaji mlivyonavyo tutahakikisha vinatumika vyema kwa ajili ya manufaa endelevu yanayolenga katika kulinda, kuimarisha na kuenzi misingi ya Muungano” alisema Dkt. Muyungi.

Alisema elimu ya Muungano ni agenda ya kudumu inayolenga kutambulisha taifa na jamii kufahamu historia na chimbuko lao, hivyo ushirikishaji wa wasanii, waigizaji, watengezaji wa maudhui ni suala lisiloepukika.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu (Muungano) Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Latifa Mohammed Khamis alisema kuwa ushirikishaji wa wasanii, waigizaji na watengezaji maudhui ni mojawapo ya mikakati iliyoandaliwa na Ofisi hiyo katika kuhakikisha elimu ya Muungano inaifikia jamii.

“Wasanii, waigizaji na Mabalozi hawa wanatoka katika pande zote mbili za Muungano na hii ni moja ya mbinu mahsusi itakayotumika katika kuhakikisha jamii yetu hususani vijana inafahamu historia, chimbuko na misingi ya Muungano” alisema Dkt. Latifa.

Wakichangia mjadala katika kikao hicho, baadhi ya wadau akiwemo mwimbaji maarufu wa taarabu Bi. Hadija Omary Kopa pamoja na kupongeza hatua hiyo ya kuwashirikisha katika suala hilo walionesha nia ya kutoa elimu ya Muungano kupitia mitandao yao ya kijamii.

Walisema kuwa kwa ushirikiano na Ofisi ya Makamu wa Rais wako tayari muda wowote kutumia vipaji vyao kutoa elimu ya Muungano kwa jamii hususan vijana ambao wawafuatilia kupitia akaunti zao za mitandao ya kijamii.

Sanjari na hilo pia walielelezea umuhimu wa wanamuziki mbalimbali kuungana na kuandaa tungo (nyimbo) maalumu za kuhamasisha jamii kuuenzi Muungano huu adhimu ambao unatajwa kuwa ni wa kipekee duniani.

Pia, walishauri uzalendo wa kupenda nchi yao na kutambua umuhimu wa Muungano upandikizwe kuanzia ngazi ya chini hususan kwenye taasisi za elimu ya msingi hadi vyuo kwani kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, Watanzania waliozaliwa baada ya Muungano ni asilimia 77.3, hivyo ni muhimu kuwapa elimu.

Kikao hicho cha siku moja kilishirikisha wasanii na waigizaji mbalimbali wakiwemo wachekeshaji maarufu mtandaoni Victor Victor ‘Nanga’, Mohamed Mwinchande ‘Matofali’, Ester Luckson ‘Mama Chanja’, Amani Nzala “Nzala”, mtengeneza maudhui mtandaoni Vicent Njau ‘Kiredio’, Mwandishi wa habari na mjasiriamali Bw. Fredrick Bundala ‘Sky Walker’, John Rojas ‘Simple the Boy’ na wengine wengi.



Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Richard Muyungi akifungua kikao kati ya Ofisi hiyo na wasanii, waigizaji na watu wenye ushawishi cha kujadili mpango wa elimu kwa umma kuhusu Muungano kilichofanyika Oktoba 19, 2026 jijini Dar es Salaam. Kulia ni Naibu Katibu Mkuu (Muungano) Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Latifa Mohammed Khamis na Mkurugenzi wa Muungano Dkt. Juma Mohammed Salum.

Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Richard Muyungi akimsikiliza Mkurugenzi wa Muungano Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Juma Mohammed Salum kabla ya kuanza kwa kikao cha Ofisi hiyo na Wadau kutoka makundi ya wasanii, waigizaji na watu wenye ushawishi wakiwa katika kikao cha kujadili mpango wa elimu kwa umma kuhusu Muungano kilichofanyika Oktoba 19, 2026 jijini Dar es Salaam.

Naibu Katibu Mkuu (Muungano) Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Latifa Mohammed Khamis akizungumza wakati wa kikao kati ya Ofisi hiyo na wasanii, waigizaji na watu wenye ushawishi cha kujadili mpango wa elimu kwa umma kuhusu Muungano kilichofanyika Oktoba 19, 2026 jijini Dar es Salaam na kufunguliwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Richard Muyungi.

Wadau kutoka makundi ya wasanii, waigizaji na watu wenye ushawishi wakiwa katika kikao cha kujadili mpango wa elimu kwa umma kuhusu Muungano kilichofanyika Oktoba 19, 2026 jijini Dar es Salaam kilichofunguliwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Richard Muyungi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...