Na Mwandishi Wetu,Kondoa


MKURUGENZI wa Halmashauri ya Mji wa Kondoa, Said Majaliwa, amepinga taarifa iliyosambazwa kwenye mtandao wa kijamii wa chombo cha habari cha Mwanahabari, ikidai kuwa Shule ya Msingi Hurumbi, iliyopo Kata ya Selia, ina miundombinu chakavu na vyoo vichafu, akisema taarifa hiyo haiakisi hali halisi ya ubora na upekee wa shule hiyo.

Majaliwa ametoa ufafanuzi huo baada ya taarifa hiyo kusambaa kwenye mitandao ya kijamii, akieleza kuwa mradi wa ujenzi wa miundombinu ya shule hiyo ulikamilika tangu Desemba 2025 kwa fedha zilizotolewa na Serikali Kuu pamoja na mapato ya ndani ya halmashauri na sasa kuwa ma miundombinu mizuri kwa watoto.

Akizungumza akiwa katika eneo la shule hiyo, Majaliwa alisema ameamua kufika mwenyewe na kutoa ufafanuzi ili kuonesha hali halisi ya miundombinu iliyojengwa na kutoa taarifa kwa umma kuwa tumechukizwa mno na taarifa za upotoshaji zilizochapishwa.

“Ndugu zangu wananchi, hapa nilipo ni Hurumbi. Nisingependa kuona nguvu za viongozi zinazotumika kukamilisha miradi ya maendeleo zikapuuzwa, huku waandishi wa habari wakitoa taarifa zinazochafua hali halisi. Nimekuja mwenyewe kuonesha majengo haya na kufafanua kuwa taarifa iliyotolewa si ya kweli,” alisema Majaliwa.

Alieleza kuwa Serikali Kuu ilitoa Sh milioni 154 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa matatu ya elimu ya awali, matundu manne ya vyoo, madarasa matatu ya shule ya msingi na matundu 12 ya vyoo.

Aidha, alisema halmashauri ilitumia Sh milioni nne kutoka mapato ya ndani kwa ajili ya ujenzi wa matundu mawili ya vyoo vya walimu, hatua iliyolenga kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji shuleni hapo.

Kwa mujibu wa Majaliwa, mradi huo ulikamilika toka Desemba 2025, hivyo taarifa iliyosambazwa kuhusu hali ya miundombinu ya shule hiyo inahitaji kuangaliwa kwa kuzingatia hali halisi ya eneo husika na taarifa za utekelezaji wa mradi.

Alisisitiza umuhimu wa waandishi wa habari kufanya uhakiki wa taarifa kabla ya kuzichapisha, akieleza kuwa taarifa zisizothibitishwa zinaweza kupotosha umma kuhusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayofanywa na Serikali na halmashauri.

Majaliwa alisema ni muhimu kwa vyombo vya habari kutembelea maeneo yanayohusika, kuzungumza na mamlaka husika na kuthibitisha taarifa kabla ya kuzisambaza ili wananchi wapate habari sahihi kuhusu huduma na maendeleo katika maeneo yao.

Hata hivyo, aliwataka waandishi wa habari ili kuweka wazi hali ya sasa ya shule hiyo kwa umma, ni muhimu taarifa zilizochapishwa kulinganishwa na ushahidi wa hali ya miundombinu iliyopo, ikiwemo madarasa, vyoo na tarehe ya kukamilika kwa mradi.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...