Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
SHULE ya Sekondari Kibasila, Manispaa ya Temeke, Dar es Salaam, imeendelea kufanya vizuri katika mitihani ya kitaifa baada ya kufanikiwa kuondoa kabisa wanafunzi waliopata daraja sifuri (0) na kupunguza idadi ya wanafunzi wanaopata daraja la nne.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Shule hiyo, Dkt. Juma Boniface Orenda, wakati wa Mahafali ya 67 ya Kidato cha Nne ya shule hiyo yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Dkt. Orenda alisema shule hiyo imeweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha inaondokana na daraja sifuri katika mitihani ya kitaifa, hatua ambayo imekuwa ikiongeza morali kwa walimu na wanafunzi katika kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji.

“Na hapa tutakubaliana wote kuwa kwa punguzo hili ni dhahiri kwamba walimu wote wa shule hii wanaunga mkono kauli mbiu ya Dkt. Samia Suluhu Hassan ya ‘Kazi na Utu Tunasonga Mbele’,” alisema.
Alisema mwaka 2024, matokeo ya Kidato cha Pili yalikuwa na ufaulu wa asilimia 100, huku Kidato cha Nne kikiwa na asilimia 100 na Kidato cha Sita asilimia 99.3.
“Kwa mwaka 2025, Kidato cha Pili, Kidato cha Nne na Kidato cha Sita yote yalikuwa na ufaulu wa asilimia 100,” alisema.

Akizungumzia hali ya elimu nchini, Dkt. Orenda alisema idadi ya shule za sekondari imeendelea kuongezeka, ambapo shule zilizosajiliwa kwa ajili ya kufanya Mtihani wa Cheti cha Elimu ya Sekondari (CSEE) mwaka 2025 zilifikia 5,864, ikilinganishwa na shule takribani 4,700 zilizokuwepo mwaka 2015.


Alisema ongezeko hilo linaonesha hatua kubwa iliyopigwa katika kupanua fursa za elimu ya sekondari nchini, huku takribani asilimia 80 ya shule hizo zikiwa za Serikali.

Pamoja na mafanikio hayo, Dkt. Orenda alisema shule hiyo bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwamo ukosefu wa kantini yenye uwezo wa kutoa huduma bora ya chakula kwa wanafunzi wote.


Alisema changamoto hiyo imekuwa kubwa zaidi katika kipindi hiki ambacho wanafunzi wote hupata chakula cha mchana shuleni.

“Changamoto nyingine ni ukosefu wa gari la shule kwa ajili ya wanafunzi wa bweni na shughuli mbalimbali za shule, pamoja na uhaba wa samani katika ofisi za walimu kama vile viti, meza na makabati, hali inayofanya walimu kufanya kazi katika mazingira magumu,” alisema.


Hata hivyo, aliishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kujenga mabweni kwa ajili ya wanafunzi wa kike wa Kidato cha Tano na Sita.


Dkt. Orenda alisema wahitimu wa Kidato cha Nne mwaka huu ni 358, wakiwemo wasichana 157 na wavulana 201, ambao walianza masomo yao Januari 2023 na wote waliosajiliwa walifanya mtihani wa taifa.

Alisema Kibasila ni miongoni mwa shule kongwe nchini, ikiwa imetimiza miaka 75 tangu ilipoanzishwa mwaka 1951 chini ya usimamizi wa Jumuiya ya Magoa, wakati huo ikiwa ikijulikana kama St. Xavier Secondary School.
“Katika kipindi hicho ilikuwa shule ya msingi na sekondari iliyokuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 225.

 Mwaka 1970, baadaye ilibadilishwa rasmi na kuwa shule ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kubadilishwa jina na kuitwa Kibasila Sekondari,” alisema.
Kwa sasa, alisema shule hiyo ina jumla ya mikondo 40 na wanafunzi 1,835, wakiwemo wasichana 859 na wavulana 976.

Alisema shule hiyo ina jumla ya walimu 65, kati yao wanaume 31 na wanawake 34, pamoja na mfanyakazi mmoja asiye mwalimu na walimu wa kujitolea 21, wakiwemo wanawake wanane na wanaume 13.

Kwa upande wake, mgeni rasmi katika mahafali hayo, Diwani Mariam Juma Mtemvu, aliipongeza shule hiyo kwa mafanikio iliyoyapata katika ufaulu na kuahidi kuwasilisha changamoto zilizotajwa kwa uongozi husika ili zipatiwe ufumbuzi.

“Hotuba ya Mkuu wa Shule nimeisikia pamoja na wanafunzi, lakini katika shule zote nilizowahi kuhudhuria, Kibasila ni namba moja. Nawapongeza sana,” alisema.
Mtemvu, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za Jamii, alisema suala la uhaba wa vyoo shuleni ni miongoni mwa changamoto atakazozifanyia kazi.

“Pamoja na mambo mengine, nimeisikia suala la uhaba wa vyoo. Kwa kweli hili pia nitalivalia njuga, kwa sababu kero hii imeniumiza sana,” alisema.

Mahafali hayo yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali, wazazi, walimu, wanafunzi wahitimu pamoja na wanafunzi wengine wa shule hiyo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...