Wakala ya Taifa ya Huduma za Ugani (NAESA), kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo, umejipanga kutoa mafunzo kwa maafisa ugani katika mikoa 14 inayopata misimu miwili ya mvua, yakilenga kuwajengea uwezo wa kutafsiri taarifa za utabiri wa mvua na kuzitumia katika kutoa ushauri kwa wakulima.
Akizungumza Oktoba 12, mara baada ya Naibu Waziri wa Kilimo David Silinde kutembelea Banda la NAESA katika Maonesho ya Siku ya Chakula Duniani yanayofanyika kuanzia Oktoba 10 hadi 16, 2026, mkoani Tanga, Kaimu Meneja wa Sehemu ya Masoko na Uongezaji Thamani, Esther Mwaisango, amesema mafunzo hayo yanalenga kuimarisha uwezo wa maafisa ugani kuelewa taarifa za hali ya hewa na kuwafikishia wakulima elimu itakayowasaidia kupanga shughuli zao za kilimo.
Amesema maafisa ugani wana nafasi muhimu katika kuwaunganisha wakulima na taarifa za kitaalamu zinazohitajika katika uzalishaji, huku NAESA ikiendelea kuratibu na kusimamia huduma za ugani nchini kwa kutoa mafunzo kwa maafisa ugani, kuratibu mafunzo katika vyuo vya kilimo na kuandaa miongozo ya utoaji wa elimu ya ugani.
Aidha, Mwaisango amesema NAESA imeshirikisha wawakilishi wa vyuo vya kilimo katika maonesho hayo ili kuonesha teknolojia mbalimbali zinazofundishwa kwa maafisa ugani, zikiwemo mbinu za uchakataji na uongezaji thamani wa mazao, ameongeza kuwa zaidi ya wakulima 5,000 wamesajiliwa katika mfumo wa usajili wa wakulima, huku zoezi hilo likiendelea.
Kwa upande wake, Nyagesera, mkufunzi kutoka Chuo cha Kilimo Uyole, amesema wakulima wanapaswa kuachana na mtazamo wa kuuza mazao ghafi pekee na badala yake kuangalia fursa za kuyachakata na kutengeneza bidhaa zinazoweza kuwaongezea kipato.
Amesema bidhaa zinazooneshwa katika banda la NAESA zimetokana na mazao ya kilimo na zinalenga kuwapa wakulima mifano ya namna wanavyoweza kutumia mazao yao kutengeneza bidhaa mbalimbali, ikiwemo bidhaa za lishe.
Nyagesera ametoa mfano wa parachichi ambayo baadhi yake yanapotokidhi vigezo vya soko huishia kutupwa, akieleza kuwa wakulima wanapaswa kuona fursa ya kutumia mazao hayo kutengeneza bidhaa zenye thamani badala ya kuyaacha bila matumizi.
Ameongeza kuwa mazao ya kilimo yanaweza kutumika kutengeneza bidhaa mbalimbali, ikiwemo mafuta yanayotokana na nta ya nyuki, akisisitiza umuhimu wa wakulima kutambua fursa za uongezaji thamani ili kunufaika zaidi na shughuli za kilimo.


.jpeg)
.jpeg)
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...