-Asema mradi wa Sh trilioni 2 utafungua fursa za uwekezaji na ajira kwa vijana
Na Jane Mwakyoma, Rukwa.
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Deogratius Ndejembi, ametembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 400 kutoka Tagamenda, Iringa, hadi Sumbawanga mkoani Rukwa, pamoja na kituo cha kupokea, kupoza na kusambaza umeme cha kilovoti 400/220/66/33 kilichopo Malangali.
Mradi huo wa Tanzania na Zambia (TAZA) unatekelezwa kwa lengo la kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika na kuunganisha maeneo mbalimbali katika gridi ya taifa.
Akizungumza na wananchi baada ya kukagua mradi huo, Ndejembi alisema kukamilika kwake kutaiwezesha Rukwa kuunganishwa na gridi ya taifa, hatua itakayochochea uwekezaji katika viwanda na kuongeza fursa za ajira kwa vijana.
Alisema upatikanaji wa umeme wa uhakika utatoa fursa mpya za kiuchumi kwa wananchi na wawekezaji, hivyo kuwataka kutumia fursa zitakazojitokeza kutokana na kukamilika kwa mradi huo.
“Nimeelezwa hapa mnapokea kilovoti 66, wakati kinajengwa kituo cha kilovoti 400. Umeme huu utasafirisha megawati 600 na utaunganisha vituo saba, huku mikoa ya Kigoma na Katavi nayo ikiunganishwa na gridi hii ya taifa. Tuchangamkie fursa za uwekezaji, umeme huu utamgusa kila mtu,” alisema Ndejembi.
Aidha, aliwataka wananchi kulinda na kutunza miundombinu inayotekelezwa na Serikali ili iweze kuwanufaisha kizazi cha sasa na vijavyo.
“Niwaombe wananchi tutimize wajibu wetu wa kulinda miundombinu hii inayotekelezwa na Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, na tujiandae kupokea uwekezaji mkubwa utakaofanyika mkoani hapa,” alisema.
Awali, akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Lazaro Twange, alisema mradi huo unagharimu Sh trilioni mbili na umefikia asilimia 90 ya utekelezaji.
Alisema ujenzi wake ulianza Novemba 2023 na unatarajiwa kukamilika Desemba mwaka huu.
Twange alibainisha kuwa kwa sasa mkoa wa Rukwa unapata umeme wa megawati 16, wakati mahitaji yake ni megawati 30, hali inayoonesha umuhimu wa kuimarisha miundombinu ya usambazaji wa umeme mkoani humo.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Salome Makamba, alisema licha ya miradi hiyo kutekelezwa na kampuni za kigeni, asilimia 90 ya vijana wa Kitanzania ndio wanaofanya kazi katika miradi inayotekelezwa na TANESCO.
Aliongeza kuwa katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Wizara ya Nishati imetangaza nafasi za ajira 1,400 kwa vijana, ambazo zinapatikana kupitia mfumo wa Ajira Portal.
Akizungumza kwa niaba ya wakazi wa Kata ya Malangali, Diwani wa kata hiyo, Andrew Matanila, aliishukuru Serikali kwa kutekeleza mradi huo, akisema umesaidia vijana wengi wa eneo hilo kupata ajira na kipato cha kukidhi mahitaji yao.
Pia aliishukuru Serikali kwa kuwalipa fidia wananchi waliopisha maeneo yao kwa ajili ya ujenzi wa mradi huo.

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...