Na Mwandishi Wetu, Mirerani

MKURUGENZI wa Shule ya Awali na Msingi ya Glisten, iliyopo Mirerani, Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, Justin Nyari, amewaasa wahitimu wa darasa la saba kutambua kuwa kuhitimu elimu ya msingi si mwisho wa safari yao ya elimu, bali ni mwanzo wa hatua mpya ya maisha.

Nyari alitoa rai hiyo katika mahafali ya sita ya shule hiyo yaliyofanyika hivi karibuni, ambapo ujumbe wake kwa wahitimu ulisomwa na mwalimu Diana Akama.

Alisema wahitimu hao wanapojiandaa kuanza elimu ya sekondari, wanapaswa kujiandaa kukabiliana na mazingira mapya, marafiki wapya na majukumu makubwa zaidi, huku wakizingatia nidhamu na maadili mema.

“Leo ni siku ya furaha na fahari, lakini kumbukeni kuhitimu darasa la saba siyo mwisho wa elimu yenu, ni mwanzo wa sura mpya,” alisema Nyari.

Aliwataka wanafunzi hao kufanya maamuzi ya busara, kuchagua marafiki wenye maadili mema, kuwasikiliza wazazi na walimu wao, pamoja na kuweka elimu mbele katika maisha yao.

Aidha, aliwaonya dhidi ya kujiingiza katika makundi mabaya, utoro, udanganyifu, matumizi mabaya ya pombe na dawa za kulevya, mahusiano yasiyofaa na tabia nyingine zinazoweza kuhatarisha maisha yao ya baadaye.

Alisisitiza kuwa wanapaswa kuwa na msimamo na kutokubali kushawishiwa na marafiki kufanya mambo yanayopingana na maadili na malengo yao.

Katika hatua nyingine, Nyari aliipongeza Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa uwekezaji katika sekta ya elimu na juhudi za kupanua fursa za elimu kwa watoto wa Kitanzania.

“Tunaishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na watangulizi wake kwa kupanua fursa za elimu kupitia elimu bila malipo na nafasi za kujiunga na shule za sekondari,” alisema.

Aliongeza kuwa wanaendelea kumuomba Mungu aibariki Tanzania, viongozi wake na wananchi ili amani, umoja na maendeleo viendelee kudumishwa nchini.

Nyari aliwatakia wahitimu hao mafanikio katika masomo yao ya sekondari na shughuli zao za baadaye, akiwahimiza kuondoka shuleni hapo wakiwa na shukrani, nidhamu, uadilifu na azma ya kutimiza malengo yao.

Alisema shule hiyo inatarajia kuwaona wahitimu hao wakifanya vizuri katika masomo yao na kukua kuwa raia wawajibikaji, wenye heshima na mchango chanya katika jamii.

Vilevile, aliwashukuru wazazi na walezi kwa kuiamini shule hiyo na kushirikiana na walimu katika malezi na makuzi ya watoto wao.

Pia, aliwapongeza walimu na wafanyakazi wa shule hiyo kwa kujitolea, uvumilivu na mchango wao katika kukuza uwezo wa kitaaluma na maadili mema kwa wanafunzi.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...