Na Mwandishi Wetu, Simanjiro
NAIBU Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, James Ole Millya, ameahidi kupambania shule za Wilaya ya Simanjiro, mkoani Manyara, kupata usajili wa shule za bweni ili ziweze kunufaika na huduma ya chakula inayotolewa na Serikali.
Ole Millya ametoa ahadi hiyo wakati akizungumza katika mahafali ya Kidato cha Nne ya Shule ya Sekondari Emboreet, ambapo amesema atawashirikisha wazee 10 wa kimila maarufu kama Malaigwani pamoja na wazee wengine wenye ushawishi katika eneo hilo kufikisha changamoto hiyo kwa Serikali.
Amesema atawaalika wazee hao kwenda Dodoma kwa ajili ya kukutana na Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, ili kujadili namna ya kutatua changamoto ya upatikanaji wa chakula kwa wanafunzi wa shule za Simanjiro.
Kwa mujibu wa Ole Millya, takribani asilimia 80 hadi 90 ya wanafunzi wa wilaya hiyo wanatoka katika jamii ya wafugaji, hivyo kuna umuhimu wa shule zao kupata usajili wa bweni ili kuwawezesha wanafunzi kupata mahitaji muhimu wanapokuwa shuleni.
“Shule nyingi za msingi na sekondari zipo mbali na makazi ya jamii, hivyo zinapaswa kupata usajili wa bweni ili wanafunzi walale huko huko na kupata chakula,” amesema Ole Millya.
Akizungumzia changamoto hiyo, Mkuu wa Shule ya Sekondari Emboreet, Aziza Rajabu Msengesi, amesema kutosajiliwa kwa shule hiyo kuwa ya bweni kwa wanafunzi wa Kidato cha Kwanza hadi cha Nne kunasababisha wazazi wengi kushindwa kumudu gharama za uchangiaji wa chakula.
Amesema hali hiyo imekuwa ikiwalazimu baadhi ya wazazi kuwahamishia watoto wao katika Wilaya ya Monduli, ambako shule zinapata ruzuku ya chakula kutoka Serikalini.
“Jambo hilo linasababisha wazazi wengine kuwahamisha watoto wao na kuwapeleka wilaya jirani ya Monduli, ambako shule zote zinapata ruzuku ya chakula kutoka Serikalini,” amesema Msengesi.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Emboreet, Yohana Shinini, amemshukuru Ole Millya kwa mchango wa Mfuko wa Jimbo katika kuchochea maendeleo ya eneo hilo.
Amesema kupitia mfuko huo, Shule ya Sekondari Emboreet ilipata Sh milioni 83 kwa ajili ya kuboresha madarasa, huku vikundi anavyovisimamia vikifanikiwa kupata mikopo yenye thamani ya Sh milioni 80 kupitia mapato ya ndani ya asilimia 10 yanayotengwa kwa ajili ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Hata hivyo, Shinini ameiomba Serikali kuangalia changamoto ya miundombinu ya barabara ya Laitunyo, akieleza kuwa kuna korongo linaloweza kuathiri usafiri na mawasiliano hasa mvua za El NiƱo zitakapoanza.
Amesema hali hiyo inaweza kuwaletea wakazi wa eneo hilo usumbufu wanapohitaji kufika Emboreet, makao makuu ya kata, hivyo kuhitajika hatua za haraka kuboresha miundombinu hiyo.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...