Wadau wa sekta ya chakula wameendelea kuhamasisha matumizi ya teknolojia na mbinu bora za uzalishaji ili kuhakikisha wananchi wanapata chakula cha kutosha, bora na salama, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha usalama wa chakula nchini kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050.

Akizungumza Oktoba 11, 2026, wakati wa maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani mkoani Tanga, Theofoch Cosmas Ndunguru, Mfuatiliaji wa Chakula na Usalama wa Chakula kutoka Wizara ya Kilimo, amesema maandalizi yamekamilika na wadau mbalimbali wamejiandaa kushiriki maonesho hayo.

Ndunguru amesema ameshiriki kutembelea banda la Umoja wa Mataifa, linaloonesha shughuli za taasisi mbalimbali, ikiwemo Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), huku akieleza kuwa ufunguzi rasmi wa maadhimisho hayo unatarajiwa kufanywa na Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde.

Amesema Tanzania ina utoshelevu wa chakula wa asilimia 133 kwa mujibu wa tathmini iliyofanyika, kiwango kinachoonesha kuwa uzalishaji wa chakula unazidi mahitaji ya nchi. Ameeleza kuwa ni muhimu kuendelea kuimarisha uzalishaji na matumizi ya teknolojia ili kuhakikisha upatikanaji wa chakula mwaka mzima, licha ya changamoto za mabadiliko ya tabianchi.

Kwa upande wake, Migidius Kasunzu, Katibu Tawala Msaidizi, Sehemu ya Uchumi na Uzalishaji kutoka Mkoa wa Tanga, ameeleza kuwa maonesho hayo yatakuwa na shughuli mbalimbali, zikiwemo maonesho ya bidhaa za chakula na nyama, utoaji wa elimu kuhusu ubora na usalama wa chakula pamoja na mashindano ya mapishi ya vyakula vya asili yatakayowapa wananchi fursa ya kujifunza na kutambua thamani ya vyakula hivyo.

Maonesho hayo yanawakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya chakula kwa lengo la kutoa elimu kwa wananchi kuhusu uzalishaji, uhifadhi, ubora na usalama wa chakula, pamoja na kuonesha bidhaa na mbinu zinazoweza kusaidia kuboresha mifumo ya chakula.

Akizungumza, Afisa Afya ya Mimea kutoka Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), Mushobozi Baitani, amesema pamoja na changamoto zinazokabili sekta hiyo nchini, kupitia maadhimisho hayo, FAO inalenga kutoa elimu na kuhamasisha wadau kushiriki katika kutafuta suluhisho la changamoto za chakula ili kuboresha upatikanaji wa chakula salama na cha kutosha kwa wananchi.

Wakazi wa Tanga na maeneo jirani wamehimizwa kujitokeza kwa wingi kutembelea maonesho hayo ili kupata elimu na kujifunza mbinu bora zinazoweza kusaidia kuimarisha upatikanaji wa chakula cha kutosha na salama kwa wananchi.


]


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...