Na Janeth Raphael - MichuziTv

Serikali imeitaka CRDB Bank kuongeza zaidi fursa za kiuchumi kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, kwa kuwawezesha kupata mitaji, mikopo na huduma za kifedha zitakazowasaidia kujikwamua kiuchumi na kukuza shughuli zao za uzalishaji.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, ametoa rai hiyo wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja, ambapo amesisitiza umuhimu wa taasisi za kifedha kuendelea kuboresha huduma zao na kwenda hatua ya ziada ili kukidhi mahitaji ya wananchi.

Senyamule amesema taasisi za kifedha zina nafasi kubwa katika kuchochea maendeleo ya wananchi, hususan vijana na wanawake, kwa kuwawezesha kupata rasilimali zitakazowawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi, ikiwamo kilimo na sekta nyingine za uzalishaji.

Amesema utoaji wa huduma bora haupaswi kuishia katika kuongeza idadi ya bidhaa au huduma, bali unapaswa kuzingatia namna taasisi zinavyoweza kurahisisha maisha ya wateja na kuwapatia suluhisho linaloendana na mahitaji yao.

“Ni muhimu kila mmoja wenu kuwa sehemu ya taswira na sifa ya taasisi hii. Jiulizeni ni huduma gani mpya inaweza kuanzishwa ili kwenda hatua ya ziada katika kuwahudumia wateja,” amesema Senyamule.

Ameongeza kuwa Wiki ya Huduma kwa Wateja inapaswa kuwa fursa kwa watumishi wa CRDB kujitathmini, kubaini maeneo yenye changamoto na kuweka mikakati ya kuboresha huduma ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma kwa ufanisi na kwa wakati.

Kwa upande wake, Meneja Biashara CRDB Kanda ya Kati, Andrew Kihenzia, amesema benki hiyo inaendelea kufanya maboresho ya huduma, mifumo na bidhaa zake kwa lengo la kuwafikia wateja kwa urahisi zaidi na kuwapatia suluhisho zinazokidhi mahitaji yao.

Kihenzia amesema CRDB imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa vikundi vya wajasiriamali, wanawake na vijana kupata mikopo inayolenga kuwawezesha kuanzisha, kuendeleza na kupanua shughuli zao za kiuchumi.

“Tunatoa fursa kwa vijana na wanawake kuhakikisha wanainuka kiuchumi kupitia mikopo ya vikundi. Tunapoendelea kusherehekea Wiki ya Huduma kwa Wateja, tunaendelea kuboresha huduma zetu kila siku,” amesema.

Amesema CRDB pia inaendelea kushirikiana na Serikali katika kuboresha mifumo inayowawezesha wafanyakazi kupata huduma za kifedha na mikopo kwa urahisi, huku ikiendelea kupanua wigo wa huduma zake kupitia matawi na vituo mbalimbali ili kuwafikia wananchi wengi zaidi.

Kihenzia amesema kwa mwaka huu CRDB imetenga Shilingi bilioni 6.5 kwa ajili ya makundi maalum, akisisitiza kuwa fursa hizo zinapaswa kutolewa kwa uwazi na kuhakikisha zinawafikia walengwa wanaokusudiwa.

Amesema hatua hiyo ni sehemu ya dhamira ya benki hiyo ya kuhakikisha huduma za kifedha zinakuwa chachu ya uwezeshaji wa wananchi na kuongeza ushiriki wa makundi mbalimbali katika shughuli za kiuchumi.

Aidha, amesema kaulimbiu ya Wiki ya Huduma kwa Wateja ya mwaka huu, “Piga Hatua Mbele,” inaendana na dhamira ya CRDB ya kuendelea kuboresha huduma, mifumo na bidhaa zake ili kuongeza ufanisi na kuhakikisha wateja wanapata huduma zinazokidhi mahitaji yao.











Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...