Na Mwandishi Wetu, Rukwa

SERIKALI imewahamasisha vijana mkoani Rukwa kushiriki kikamilifu katika Wiki ya Vijana Kitaifa 2026, ili kupata maarifa, kujifunza na kufanya maamuzi sahihi ya kutumia fursa zilizopo katika maeneo yao kwa ajili ya kujikwamua kiuchumi na kushiriki katika maendeleo ya Taifa, badala ya kusubiri ajira pekee.

Kauli hiyo imetolewa leo, Oktoba 5, 2026, na Katibu Tawala wa Mkoa wa Rukwa, Msalika Makungu, kwa niaba ya Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais–Maendeleo ya Vijana, Jenifa Christian Omolo, wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusu maandalizi ya Wiki ya Vijana Kitaifa 2026.

Makungu amesema kuanzia Oktoba 8 hadi 14, 2026, kutakuwa na maonyesho katika viwanja vya Shule ya Msingi Ndua, Manispaa ya Sumbawanga, yatakayoshirikisha taasisi za Serikali, sekta binafsi, washirika wa maendeleo, mashirika ya vijana, wabunifu, wajasiriamali na watoa huduma mbalimbali.

Amesema ufunguzi rasmi wa kongamano hilo utafanyika Oktoba 10, 2026, ambapo Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.

Aidha, amesema Oktoba 11 na 12, 2026, kutakuwa na Kongamano la Vijana litakalowakutanisha vijana 1,500 kila siku kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.

Kwa mujibu wa Makungu, kongamano hilo litatoa fursa kwa vijana kujadili masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo yao, kupata taarifa kutoka kwa wataalamu, taasisi za Serikali, sekta binafsi na washirika wa maendeleo, pamoja na kutoa maoni na mapendekezo kuhusu masuala yanayowahusu.

Amesema maonyesho hayo pia yatahusisha shughuli mbalimbali, ikiwemo kongamano la vijana, maonesho ya bidhaa na huduma, pamoja na utoaji wa taarifa kuhusu fursa na huduma zinazowahusu vijana.

“Kongamano hili linatarajiwa kuwapa vijana nafasi ya kujifunza, kubadilishana uzoefu na kukutana na wadau mbalimbali wa maendeleo,” amesema.

Aidha, Makungu amesema kilele cha maadhimisho hayo kitafanyika Oktoba 14, 2026, sambamba na kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru pamoja na kumbukizi ya miaka 27 ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

Amesema shughuli hizo zitafanyika katika Uwanja wa Nelson Mandela, Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga, ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.

Kaulimbiu ya Wiki ya Vijana Kitaifa 2026 ni “Mazingira Tofauti, Fursa Sawa kwa Vijana”, inayolenga kuhamasisha vijana kutoka maeneo mbalimbali kutambua fursa zilizopo, kupata maarifa na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya Taifa.







Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...