DAR ES SALAAM
MAWAZIRI wa Ulinzi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Msumbiji, Dkt. Rhimo Nyansaho na Cristóvão Artur Chume, wamehitimisha rasmi Mkutano wa Saba wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano wa Ulinzi na Usalama kati ya nchi hizo mbili.
Mkutano huo uliofanyika jijini Dar es Salaam, umehitimishwa Oktoba 7, 2026, kwa kusainiwa kwa makubaliano mbalimbali yanayolenga kuimarisha zaidi ushirikiano wa Tanzania na Msumbiji katika masuala ya ulinzi na usalama.
Makubaliano hayo yanatarajiwa kuendelea kuimarisha juhudi za nchi hizo mbili katika kulinda amani, utulivu na usalama wa wananchi, pamoja na kushughulikia kwa pamoja masuala yenye maslahi ya pamoja katika eneo la ulinzi na usalama.
Mkutano huo wa saba wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano wa Ulinzi na Usalama pia ulilenga kuendeleza na kuimarisha maono ya waasisi wa mataifa hayo mawili, Hayati Baba wa Taifa wa Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, na Hayati Samora Moisés Machel wa Msumbiji.
Viongozi hao waliweka msingi imara wa uhusiano wa kihistoria, kidugu na kimkakati kati ya Tanzania na Msumbiji, ambao umeendelea kudumishwa katika vipindi mbalimbali.
Maono hayo yanaendelea kuenziwa na viongozi wa sasa wa nchi hizo mbili, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, na Rais wa Jamhuri ya Msumbiji, Daniel Chapo, kupitia kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa pande mbili katika maeneo yenye maslahi ya pamoja.
Ushirikiano huo unatajwa kuwa sehemu muhimu ya kuendeleza amani, usalama na utulivu katika Tanzania, Msumbiji na ukanda wa kusini mwa Afrika






Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...