Na Seif Mangwangi, Michuzi TV, Arusha

TANZANIA imezindua Ajenda ya Kitaifa ya Maendeleo ya Mafundi na Uchumi wa Ubunifu, inayolenga kuweka mazingira bora kwa mafundi na wasanii kukuza shughuli zao, kufungua masoko mapya na kuchangia zaidi katika uchumi wa taifa.

Aidha kupitia ajenda hiyo, Tanzania inalenga kutengeneza zaidi ya ajira 600,000 na kuzalisha mapato ya dola za Marekani milioni 500 kwa mwaka ifikapo 2032.

Akizungumza katika uzinduzi wa ajenda hiyo jijini Arusha,Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzania International Tourism Festival, Ibrahim Othman Jama, amesema ajenda hiyo ya miaka mitano inalenga kuunganisha sekta ya sanaa, utamaduni, biashara na utalii ili kuhakikisha kazi za mafundi na wasanii zinakuwa sehemu muhimu ya uchumi wa Tanzania.

Amesema ajenda hiyo imejengwa juu ya nguzo sita, ikiwemo kurasimisha, kusajili na kuweka mfumo wa kutambua mafundi na wasanii nchini, pamoja na kutumia teknolojia na mifumo ya kidijitali katika kukuza uchumi wa sekta hiyo.

Kwa mujibu wa Jama, nguzo nyingine ni kufungua masoko mapya ndani na nje ya Tanzania, kulinda haki miliki za mafundi na wasanii pamoja na kuendeleza urithi wa vitendo na ubunifu unaotokana na tamaduni mbalimbali za Watanzania.

Amesema ajenda hiyo pia inalenga kuunganisha kikamilifu kazi za mafundi na wasanii katika uchumi wa utalii wa Tanzania, akisisitiza kuwa hadithi ya utalii wa Tanzania haiwezi kutenganishwa na hadithi ya ubunifu, sanaa na utamaduni wa Watanzania.

Jama amesema kupitia ajenda hiyo, Tanzania inalenga kusajili takribani mafundi 50,000, kuzalisha mapato ya dola za Marekani milioni 500 kila mwaka kutoka katika sekta hiyo na kutengeneza ajira 600,000 katika uchumi wa ubunifu ifikapo mwaka 2032.

Amesema malengo hayo pia yamezingatia usawa wa kijinsia na kuongeza nafasi za vijana kushiriki katika uchumi wa ubunifu, akieleza kuwa kundi hilo limekuwa likihitaji fursa zaidi za kuonyesha vipaji, kupata masoko na kujenga maisha kupitia kazi zao.

Ameeleza kuwa Tanzania International Tourism Festival ilianzishwa kwa lengo la kujenga majukwaa yanayokutanisha utamaduni, biashara na jamii, huku tamasha hilo likiwa sehemu ya utekelezaji wa dhamira hiyo kwa kuwaunganisha mafundi na wasanii kutoka maeneo mbalimbali nchini na wanunuzi, wawekezaji na wadau wengine.

Jama amesema zaidi ya wasanii na mafundi 100 wamepata nafasi ya kushiriki katika tamasha hilo, akibainisha kuwa thamani kubwa ya tukio hilo haiishii kwa washiriki waliopo Arusha bali inapaswa kuonekana katika mabadiliko ya maisha ya mafundi walioko vijijini na kwenye warsha mbalimbali nchini.

Amesema mafundi kama washonaji, wachongaji, wachoraji, wasusi na wanaofanya kazi za vyuma wamekuwa wakibeba historia na utamaduni wa Tanzania kupitia kazi zao, lakini mara nyingi hawapati kutambuliwa wala kulipwa kulingana na thamani ya kazi wanazozifanya.

Katika hatua nyingine, Jama ameiomba Serikali na wadau wa sanaa kuweka mifumo itakayowawezesha wasanii na mafundi kushiriki katika matukio ya kimataifa ili kupata fursa za kuonyesha kazi zao, kujenga mitandao ya kibiashara na kutafuta masoko nje ya Tanzania.

Amesema mabalozi na balozi za Tanzania katika nchi mbalimbali zinaweza kuwa sehemu muhimu ya kufungua fursa hizo kwa kuwaunganisha wasanii na mafundi wa Tanzania na masoko ya kimataifa, huku akisisitiza umuhimu wa BASATA na taasisi nyingine za sanaa katika kuratibu fursa hizo.

Ameishukuru Serikali, Serikali ya Mkoa wa Arusha, viongozi wa Wilaya, Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), COSOTA, Bodi ya Filamu, BRELA, taasisi za fedha, washirika wa maendeleo na wadau mbalimbali kwa kushirikiana katika kufanikisha tamasha hilo na ajenda hiyo.

Amesema katika kipindi cha siku tano za tamasha hilo, Arusha itakuwa mwenyeji wa maonesho ya sanaa, biashara, warsha, mikutano ya kibiashara kati ya wafanyabiashara na wawekezaji (B2B), pamoja na filamu na shughuli zinazolenga kuonyesha utamaduni wa Tanzania.

Jama ametoa wito wa kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi, wasanii, mafundi, taasisi za fedha na wadau wa utalii ili ajenda hiyo iweze kutekelezwa na kutoa fursa kwa Watanzania wengi zaidi, hasa vijana, wanawake na jamii zinazotegemea kazi za ubunifu kama chanzo cha kipato.

Mgeni rasmi katika uzinduzi wa tamasha hilo, Mkurugenzi Msaidizi wa Sanaa za Ufundi kutoka Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Bona Leoni Masenge, amewataka vijana na wanawake nchini kutumia vipaji vyao katika sanaa na ubunifu kama fursa ya kujiajiri na kuongeza kipato, badala ya kuuchukulia ubunifu kama njia ya burudani pekee.

Masenge amesema sanaa na ubunifu vina uwezo wa kuzalisha ajira na kujenga biashara, hivyo vijana wanapaswa kutumia vipaji walivyonavyo kuanzisha shughuli zinazoweza kuwapatia kipato na kuchangia maendeleo ya familia na jamii.

Amesema mtu anayeshona nguo, kufuma, kuchonga, kuchora, kupaka rangi, kutengeneza bidhaa za ngozi, kufua chuma, kubuni mavazi au kuhifadhi mbinu za jadi za sanaa siyo fundi pekee, bali ni mjasiriamali, mbunifu na mtunzi wa utamaduni wa Tanzania.







Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...