Na Mwandishi Wetu.

  Dar es Salaam, Oktoba 7, 2026 

Shirika la Dawa Asilia na Ulinzi wa Mazingira Tanzania (TRAMEPRO) limeungana na Watanzania na jamii ya kimataifa kumkumbuka Askofu Mkuu Desmond Mpilo Tutu, aliyezaliwa Oktoba 7, 1931 nchini Afrika Kusini na kufariki dunia Desemba 26, 2021 akiwa na miaka 90.

Tutu, aliyekuwa kiongozi wa dini na mtetezi wa haki za binadamu, amani na maridhiano, alitunukiwa Tuzo ya Nobel ya Amani mwaka 1984 kutokana na mchango wake katika mapambano dhidi ya Apartheid nchini Afrika Kusini.

Katika kumbukizi hiyo, TRAMEPRO imesema urithi wa Tutu unapaswa kuwa somo kwa jamii kuhusu umuhimu wa kutumia nafasi na taaluma walizonazo kuleta mabadiliko na kuacha alama kwa vizazi vijavyo.

Shirika hilo limetumia pia kumbukizi hiyo kuhimiza Tanzania kutumia nafasi yake katika majukwaa ya kimataifa, ikiwemo Mkutano wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), kutangaza fursa zilizopo katika afya, mazingira, utafiti na Tiba Asili.

TRAMEPRO imesema Tanzania ina utajiri wa mimea tiba na maarifa ya jadi ambayo yanaweza kuchangia katika afya, utafiti, uhifadhi wa mazingira na uchumi, lakini maendeleo ya sekta hiyo yanapaswa kuzingatia usalama wa watumiaji, utafiti, ushahidi, ubora wa bidhaa, maadili ya kitaaluma na uhifadhi wa bioanuwai.

Aidha, shirika hilo limewataka wataalamu wa Tiba Asili kuwa waaminifu kwa wagonjwa, kuepuka madai yasiyothibitishwa na kushirikiana na watafiti pamoja na wataalamu wengine wa afya.

TRAMEPRO pia imewataka viongozi wa dini kuendelea kuwa sauti ya amani, utu na maridhiano, huku vyombo vya habari vikihimizwa kuelimisha jamii kuhusu afya, mazingira na matumizi salama ya Tiba Asili.

Kwa upande wa wananchi, shirika hilo limesisitiza umuhimu wa kutambua kuwa afya ya binadamu inahusiana moja kwa moja na afya ya mazingira, hivyo kulinda misitu, maji, udongo na mimea tiba ni kulinda maisha ya kizazi cha sasa na kijacho.

TRAMEPRO imesema kumbukizi ya Desmond Tutu inapaswa kuwa changamoto kwa kila mtu kufanya jambo litakalobaki kuwa na thamani katika jamii.

“Umoja wetu ndiyo nguvu yetu. Huduma yetu ndiyo alama yetu. Matendo yetu ndiyo historia yetu.”

BONIVENTURA  MWALONGO. Katibu Mkuu & Mtaalamu wa Tiba Asili TRAMEPRO

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...