Na Mwandishi Wetu, Simanjiro
Wahitimu wa kidato cha nne wa Shule ya Sekondari Loiborsiret, wilayani Simanjiro, mkoani Manyara, wameaswa kutumia muda uliobaki kujisomea kwa bidii na kujiandaa kikamilifu kwa mitihani yao ya mwisho ili waweze kufanya vizuri na kufikia malengo yao ya kielimu.
Wito huo umetolewa na Afisa Mtendaji wa Kata ya Loiborsiret, Charles Msangya, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mahafali ya 13 ya kidato cha nne ya shule hiyo.
Msangya amewataka wahitimu 56 wa mwaka 2026 kutumia siku zilizobaki kabla ya kuanza kwa mitihani kujikumbusha masomo waliyofundishwa na kuimarisha maandalizi yao ili kupata matokeo mazuri.
“Hatua mliyofikia kielimu hampaswi kuridhika nayo, safari bado ni ndefu. Nawaasa msisikilize maneno ya mitaani kwamba watu wasiosoma wana fedha. Hiyo ni mipango ya Mungu, lakini mtu mwenye elimu huwezi kumfananisha na ambaye hajasoma,” amesema Msangya.
Aidha, amelizipongeza shirika lisilo la kiserikali la Namayana Foundation kwa kuahidi kununua mashine ya fotokopi kwa ajili ya shule hiyo, akieleza kuwa msaada huo utasaidia kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji.
Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Sekondari Loiborsiret, Mwalimu Fabian Amsi Doriye, amesema shule hiyo imeendelea kufanya vizuri katika mitihani ya kitaifa, ambapo kwa miaka miwili mfululizo wanafunzi wa kidato cha pili na cha nne wamepata ufaulu wa asilimia 100.
Amesema wanafunzi 56 wanaotarajia kufanya mtihani wa kuhitimu kidato cha nne mwaka huu wameandaliwa ipasavyo, huku matarajio ya shule yakiwa ni kupata ufaulu wa madaraja ya kwanza na ya pili.
Doriye, ambaye amekuwa mkuu wa shule hiyo tangu mwaka 2024, amesema mafanikio hayo yametokana na ushirikiano kati ya walimu, wanafunzi, wazazi na walezi katika kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu bora.
Amesema shule hiyo imeendelea kuimarika pia kupitia miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali, ikiwemo ujenzi wa majengo mawili ya maabara yenye thamani ya shilingi milioni 30 kupitia fedha za mpango wa EP4R, pamoja na upatikanaji wa madarasa na nyumba za walimu.
Ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwekeza katika miradi ya elimu inayolenga kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.
Naye mmoja wa wahitimu hao, Lena Nebuti, amesema ndoto yake ni kuwa mwanasheria, akieleza kuwa ana matumaini ya kufaulu mtihani wa kidato cha nne ili kuendelea na masomo na kutimiza azma hiyo.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...