Na. Vero Ignatus,Michizi TV- ARUSHA.
Tanzania imeendelea kuimarisha nafasi yake katika juhudi za kikanda na kimataifa za usalama wa nyuklia baada ya Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC) kwa kushirikiana na Wakala wa Kimataifa wa Nguvu za Atomu (IAEA) kuwakutanisha wataalamu na washiriki kutoka nchi 18 katika warsha ya kikanda inayolenga kuimarisha uwezo wa rasilimali watu katika masuala ya usalama wa nyuklia.
Akifungua warsha hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa TAEC ambaye pia ni Mratibu wa Kitaifa wa Tanzania na IAEA (National Liaison Officer – NLO), Prof. Najat Kassim Mohamed, amesema mkutano huo unalenga kujadili namna Vituo vya Usaidizi wa Usalama wa Nyuklia (Nuclear Security Support Centres – NSSCs) vinavyoweza kusaidia nchi kujenga na kudumisha wataalamu wenye uwezo wa kusimamia masuala ya usalama wa nyuklia.
Prof. Najat amesema maendeleo ya rasilimali watu ni jukumu endelevu linalohitaji nchi kutambua ujuzi unaohitajika na mahitaji ya mafunzo, ili kuwa na uwezo wa kuendesha na kudumisha mifumo ya usalama wa nyuklia, pamoja na kuzuia, kugundua na kukabiliana na matukio yanayohusiana na usalama huo.
Aidha, amesema washiriki wa warsha hiyo wanajadili mipango ya maendeleo ya wataalamu katika mazingira ya usalama wa nyuklia duniani, mifumo ya kitaifa ya ulinzi, utambuzi na mwitikio, pamoja na usimamizi wa maarifa ili kuhakikisha taarifa na uzoefu muhimu vinakusanywa, vinahifadhiwa na kushirikishwa kwa wakati unaofaa.
Prof. Najat amesema Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazotumia teknolojia ya nyuklia katika sekta mbalimbali, ikiwemo afya, kilimo, utafiti na uchunguzi, huku akieleza kuwa baadhi ya nchi za Afrika Mashariki, ikiwemo Kenya, Rwanda, Uganda na Tanzania, zimeonesha nia ya kuendeleza matumizi ya teknolojia ya nyuklia kwa ajili ya uzalishaji wa umeme. Amesema Afrika Kusini ina uzoefu wa muda mrefu katika uzalishaji wa umeme wa nyuklia, huku Misri ikiendelea na mradi wake wa kuzalisha umeme wa nyuklia.
Kwa upande wake, Judith Aloch Okor, Mkaguzi wa Nyuklia kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Nyuklia ya Kenya (KNRA), amesema ameshiriki mafunzo hayo kwa lengo la kujifunza mbinu za kutambua mapungufu ya umahiri na kutathmini mahitaji ya mafunzo, pamoja na kupata maarifa na uzoefu utakaosaidia kuimarisha maendeleo ya rasilimali watu katika eneo la usalama wa nyuklia.
Akizungumzia hofu kuhusu madhara yanayoweza kutokana na matumizi ya teknolojia ya nyuklia, ikiwemo silaha za nyuklia, Judith amesema nchi za Afrika zimejikita katika matumizi ya teknolojia hiyo kwa madhumuni ya amani na usalama, akieleza kuwa sayansi na teknolojia ya nyuklia inatumika katika maeneo mbalimbali ikiwemo utafiti wa kisayansi, kilimo, viwanda na tiba.



.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...