Tanzania imeyatolea wito mataifa ya ukanda wa Magharibi mwa Bahari ya Hindi kuimarisha ushirikiano wa kisiasa, kiuchumi na kimazingira ili kulinda rasilimali za bahari zenye thamani ya zaidi ya dola bilioni 300 za Marekani dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi, uchafuzi wa mazingira na matumizi yasiyo endelevu.

Wito huo umetolewa na Makamu wa Rais, Mhe. Deogratius Ndejembi, wakati akimwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika ufunguzi wa Mkutano wa 12 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Nairobi (COP12), unaofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere, Dar es Salaam.

Makamu wa Rais amezitaka nchi wanachama kutafsiri makubaliano ya kimazingira katika hatua madhubuti za kisera, kisheria na kibajeti, huku akisisitiza kuwa ukuaji wa uchumi wa buluu lazima uende sambamba na uhifadhi wa mazingira, uzalishaji wa ajira na mgawanyo wa haki wa manufaa kwa wananchi.

Ameeleza kuwa zaidi ya watu milioni 65 wanategemea bahari moja kwa moja kwa maisha yao, huku ukanda huo ukizalisha takribani dola bilioni 20.8 kila mwaka na huduma za mifumo ya ikolojia zikiwa na thamani ya dola bilioni 25 kwa mwaka.

Aidha, ameainisha vipaumbele sita vya kuimarisha usimamizi wa bahari, vikiwemo kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kudhibiti uchafuzi, kuhifadhi bioanuai, kuwekeza katika sayansi na teknolojia pamoja na kuongeza ushiriki wa sekta binafsi, wanawake na vijana katika uchumi wa buluu.

Kwa upande wake, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP, Bi. Elizabeth Maruma Mrema, amesisitiza umuhimu wa mshikamano wa kikanda na ushirikishwaji wa taasisi za fedha katika uwekezaji wa uchumi endelevu wa buluu, huku Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Masauni, akieleza kuwa Tanzania imenufaika na msaada wa kitaalamu, udhibiti wa uchafuzi na ushirikiano wa kimazingira kupitia Mkataba wa Nairobi.

Mkutano wa COP12, unaoadhimisha miaka 40 ya Mkataba wa Nairobi, unawakutanisha washiriki zaidi ya 1,500 kutoka nchi mbalimbali duniani, zikiwemo nchi 10 wanachama, kuanzia Oktoba 6 hadi 9, 2026.










Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...