Na Munir Shemweta, WANMM KASULU

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt. Leonard Akwilapo, ameendelea na ukaguzi wa maeneo ya uwekezaji ambapo ametembelea eneo la mradi wa kilimo cha miwa na uzalishaji sukari la Kasulu Sugar, wilayani Kasulu mkoani Kigoma na kusisitiza umuhimu wa ardhi iliyotolewa kwa uwekezaji kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa.

Amesema, Serikali inataka kuona maeneo yote yaliyotolewa kwa wawekezaji yakiendelezwa na kuleta tija kwa mujibu wa makubaliano na mipango iliyowekwa.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ndiyo mwenye dhamana ya kuunda Kamati ya Kitaifa ya Kugawa Ardhi ya uwekezaji ambapo mbali na jukumu hilo pia kamati inamshauri Kamishna wa Ardhi katika kushughulikia maombi ya umilikishaji ardhi.

Dkt. Akwilapo amefanya ziara hiyo mwishoni mwa wiki katika eneo la mradi huo linalomilikiwa na kampuni ya Mufindi Papers Mills Co. Limited, maarufu kama Kasulu Sugar, lenye ukubwa wa hekta 37,662.

Katika ziara hiyo, Dkt Akwilapo alijionea shughuli za uwekezaji zinazofanyika na kutoa msisitizo kwa uongozi wa kampuni kuhakikisha ardhi hiyo inaendelezwa na kutumika kwa shughuli za kilimo cha miwa na uzalishaji wa sukari.

"Wizara haitarajii kuona ardhi inayotolewa kwa ajili ya uwekezaji ikiendelea kubaki bila kuendelezwa".amesema Mhe Dkt Akwilapo.

Ameupongeza uongozi wa Kasulu Sugar kwa uwekezaji uliofanyika na kuutaka kuongeza kasi ya utekelezaji wa mradi huo ili uweze kuchangia uzalishaji wa sukari nchini.

"Kuendelezwa kwa eneo hili kutasaidia kuongeza uzalishaji miwa na sukari, kupanua upatikanaji wa bidhaa hiyo sokoni na kuwa na mchango katika kupunguza changamoto ya bei ya sukari nchini". Ameeleza.

Ziara hiyo ni utekelezaji wa maelekezo ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii iliyotaka maeneo yaliyotolewa kwa shughuli za uwekezaji kukaguliwa kwa lengo la kubaini maeneo yasiyoendelezwa ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa.

Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni Mufindi Papers Mills Co. Limited Bw. Satya Narayana amemueleza Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuwa, mradi unaotekelezwa na kampuni yake unatumia teknolojia ya hali ya juu na ya kisasa katika uzalishaji sukari.

"Mradi wa kilimo cha miwa na uzalishaji sukari katika kiwanda hiki unagharimu dola 320 milioni na unatarajia kuchangia uchumi wa Tanzania na jamii kwa ujumla". Amesma.

Eneo la mradi wa Kasulu Sugar wilayani Kasulu mkoa wa Kigoma linahusisha vijiji saba vya Nyarugusu, Kiyungwe, Kitanga, Kamtundu, Nyamidaho, Kigadye na Heru Ushingo, vilivyotoa ardhi kwa ajili ya uwekezaji wa mradi huo.

Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi inaendelea na jitihada za kufuatilia matumizi ya ardhi kwenye maeneo ya uwekezaji kwa lengo la kuhakikisha rasilimali hiyo inatumika kwa tija, kwa kuzingatia mipango ya matumizi ya ardhi na masharti yaliyowekwa.

Hatua hiyo inalenga kuimarisha usimamizi wa ardhi, kuhakikisha wawekezaji wanatimiza wajibu wao na kuongeza mchango wa uwekezaji katika kukuza uchumi na kuboresha maisha ya wananchi.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Akwilapo akioneshwa sehemu ya eneo la uwekezaji kutoka kwa Meneja Mradi wa eneo la uwekezaji kilimo cha miwa na uzalishaji sukari la kampuni ya Mufindi Papers Mills Co. Limited, maarufu kama Kasulu Sugar Bw. Niket Pande wakati wa ziara ya kutembelea eneo la mradi huo wilayani Kasulu mkoa wa Kigoma mwishoni mwa wiki. Wa pili kulia ni mbunge wa jimbo la Kasulu Vijijini Mhe. Edibily Kazala
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Akwilapo akipata maelezo kutoka kwa Meneja Usalama, Afya na Mazingira wa kampuni ya Mufindi Papers Mills Co. Limited, maarufu kama Kasulu Sugar Bw. Ahned Shaban (Kushoto) wakati alipotembelea eneo la mradi huo wilayani Kasulu mkoa wa Kigoma mwishoni mwa wiki.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Akwilapo akipata maelezo ya maendeleo ya ujenzi wa kiwanda cha sukari cha Mufindi Papers Mills Co. Limited, maarufu kama Kasulu Sugar kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa kiwanda hicho Bw. Satya Vekanta (wa pili kulia) alipotembelea eneo hilo la uwekezaji wilayani Kasulu mkoa wa Kigoma mwishoni nwa wiki. Wa pili kushoto ni mbunge wa jimbo la Kasulu Vijijini Mhe. Edibily Kazala.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Akwilapo akipanda mti wa kumbukumbu alipotembelea eneo la uwekezaji mradi wa kilimo cha miwa na uzalishaji sukari la kampuni ya Mufindi Papers Mills Co. Limited, maarufu kama Kasulu Sugar tarehe 2 Oktoba 2026.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Akwilapo akingumza na uongozi wa kampuni ya uwekezaji mradi wa kilimo cha miwa na uzalishaji Sukari wa kampuni ya Mufindi Papers Mills Co. Limited, maarufu kama Kasulu Sugar alipofanya ziara kwenye eneo la mradi huo wilayani Kasulu mkoani Kigoma tarehe 2 Oktoba 2026.
Meneja Mradi eneo la uwekezaji kilimo cha miwa na uzalishaji sukari la kampuni ya kampuni ya Mufindi Papers Mills Co. Limited, maarufu kama Kasulu Sugar tarehe 2 Oktoba 2026. Bw. Niket Pande akielezea namna mradi wa kiwanda cha sukari unavyofanyika wakati wa ziara ya Waziri wa ardhi tarehe 2 Oktoba 2026

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Akwilapo akitembelea moja ya maeneo ya uwekezaji mradi wa kilimo cha miwa na uzalishaji sukari la kampuni ya kampuni ya Mufindi Papers Mills Co. Limited, maarufu kama Kasulu Sugar mwishoni mwa wiki.

Meneja Mradi eneo la uwekezaji kilimo cha miwa na uzalishaji sukari la Kasulu Sugar Bw. Niket Pande (kushoto) akimuelezea Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo namna pampu ya maji inavyofanya kazi wakati alipotembelea eneo hilo la uwekezaji wilayani Kasulu mkoani Kigoma mwishoni mwa wiki. Katikati ni Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Mufindi Papers Mills Co. Limited Bw. Satya Narayana.

Munonekano wa eneo la shamba la miwa katika eneo la uwekezaji mradi wa kilimo cha miwa na uzalishaji sukari la kampuni ya kampuni ya Mufindi Papers Mills Co. Limited, maarufu kama Kasulu Sugar. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...