Na Mwandishi Wetu
WANANCHI wa Kitongoji cha Saburi, Kata ya Makuyuni, wametoa taarifa ya dharura kuomba ulinzi na uingiliaji kati wa haraka kutoka kwa viongozi wao wa serikali dhidi ya vitendo vya kinyama na uvunjifu wa amani vinavyofanywa na mwekezaji Akram Aziz.
Wamesema mwekezaji huyo leo amefika kwenye kitongoji chao akiwa na tingatinga kubwa (bulldozer) kwa lengo la kubomoa nyumba zote zaidi ya 600, pamoja na kuharibu misikiti, kanisa, shule, na zahanati.
Kwa mujibu wa wananchi hao wameeleza kwamba kitendo hicho kimesababisha taharuki kubwa, simanzi, na kuzuka kwa vurugu kati ya vibaraka wake na wananchi wenye hasira waliokuwa wakitetea haki na mali zao za maisha yote, jambo ambalo lililazimu upande wa mwekezaji kukimbia ili kunusuru maisha yao kutokana na ghadhabu za wananchi.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari leo Oktoba 3,2026 na wananchi wa kitongoji hicho kuhusu kinachoendelea katika kijiji hicho wamesema wameishi katika Kitongoji cha Saburi kwa zaidi ya miaka 30.
Wamesema kuwa eneo hilo walipewa kihalali na mwekezaji aliyetangulia, na baadaye Halmashauri ilipima na kuweka alama (beacons) kutenga eneo hilo kutoka katika Shamba la mwekezaji na wananchi hao pia waliuza vipande vya maeneo ilikupata pesa kwaajili ya kujenga makazi na kujiendeleza katika eneo lao.
“Kwa sasa eneo hili limetambuliwa na kusajiliwa rasmi na TAMISEMI kama Kitongoji kinachojitegemea, chenye miundombinu kamili ikiwemo shule,Zahanati, Miskiti na Kanisa, Miundombinu ya Umeme wa REA na Visima vya Maji.Pia kuna makazi ya wananchi zaidi ya 600
Wakieleza zaidi wamesema mwaka 2025 halmashauri ilimuandikia barua rasmi mwekezaji huyo ikimtaka aachie ekari 400 ili kupisha makazi ya wananchi hawa waliowekeza maisha yao hapo zaidi ya miaka 30.
Hata hivyo, mwekezaji huyo amegoma kabisa kutii agizo hilo, akionyesha wazi kiburi cha kupambana na maamuzi ya Serikali za Mitaa.
Kuhusu tukio la mwekezaji kwenda na tingatinga wananchi hao wamesema hali hiyo inaweza kuhatarisha amani ya eneo lao wakati wowote.”Tunaiomba Serikali kupitia ofisi za Mkuu wa Wilaya na Mkuu wa Mkoa kuchukua hatua za dharura ikiwemo kumzuia mara moja Akram Aziz kufanya jaribio lolote la kubomoa makazi na taasisi za kijamii katika Kitongoji cha Saburi.
Hatua nyingine ni kufanya uchunguzi wa dharura kuhusu hati anazozitumia kujitwalia ardhi ya wananchi waliokaa kihalali kwa zaidi ya miongo mitatu pamoja na kulinda usalama wa maisha na mali zao kwa kupeleka vyombo vya ulinzi kuzuia mwekezaji huyu kujichukulia sheria mkononi.
“Haiwezekani wananchi wa Kitongoji cha Saburi tuwe wakimbizi ndani ya nchi yetu wenyewe baada ya kuishi kwa zaidi ya miaka 30. Tunaomba msaada wa haraka, “wamesema wananchi wa Kitongoji cha Saburi, Makuyuni.









Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...