Na Janeth Raphael - MichuziTv
Mbunge wa Jimbo la Kigoma Mjini, Mhe. Clayton Revocatus Chipando, maarufu kama Baba Levo, ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuendelea kuboresha na kujenga viwanja vya kisasa vya michezo nchini.
Akichangia hoja bungeni, Baba Levo amesema uwekezaji unaofanywa na Serikali katika miundombinu ya michezo ni hatua muhimu itakayoiwezesha Tanzania kuwa mwenyeji wa mashindano mbalimbali ya kimataifa.
Amesema viwanja hivyo vitakuwa na mchango mkubwa katika maandalizi na kufanikisha mashindano yanayotarajiwa kufanyika nchini mwaka 2027, sambamba na matukio mengine makubwa ya michezo yatakayofuata.
Mbunge huyo amesema ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya michezo unaonesha dhamira ya Serikali ya kuikuza sekta hiyo na kuweka mazingira bora kwa wanamichezo kushiriki na kufanya vizuri katika mashindano ya kitaifa na kimataifa.
Katika mchango wake, Baba Levo pia amesisitiza umuhimu wa wabunge kujadili kwa kina hoja na mapendekezo yanayotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Amesema mjadala wa hoja hizo utawasaidia wananchi kufahamu namna wawakilishi wao wanavyosimamia matumizi ya fedha za umma, pamoja na kufuatilia utekelezaji wa mapendekezo yanayotolewa katika taarifa za ukaguzi.
Baba Levo ameongeza kuwa wabunge wana wajibu mkubwa wa kuhakikisha hoja zinazobainishwa na CAG zinapatiwa ufumbuzi na hatua stahiki zinachukuliwa, ili kuimarisha uwajibikaji na kuhakikisha fedha za umma zinatumika kwa ufanisi na kwa manufaa ya wananchi.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...