Na Janeth Raphael – MichuziTv Bungeni 

Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Esther Matiko, amehoji hatima ya Shilingi Bilioni 13.88 zilizotengwa kwa ajili ya mikopo ya asilimia 10 ya Halmashauri, akitaka Serikali kueleza fedha hizo zilipoelekezwa baada ya kubainika kuwa hazikuwafikia walengwa waliokusudiwa.

Matiko ameeleza kuwa fedha hizo zilipaswa kuwanufaisha makundi maalumu ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kupitia mfumo wa mikopo inayotolewa na Halmashauri, lakini ripoti ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) imeibua hoja kuhusu kutofikishwa kwa fedha hizo kwa walengwa.

Akichangia hoja bungeni jijini Dodoma leo, Novemba 4, 2026, Matiko amesema hali hiyo inahitaji maelezo ya kina kutoka Serikalini, kwa kuwa fedha hizo zilitengwa kwa lengo maalumu la kuwawezesha wananchi kiuchumi na kuwasaidia kuanzisha au kuendeleza shughuli za uzalishaji mali.

Amesisitiza kuwa sheria inayosimamia Mamlaka za Serikali za Mitaa inaelekeza Halmashauri kutenga asilimia 10 ya mapato yake kwa ajili ya makundi hayo, hivyo ni muhimu kuhakikisha matakwa ya sheria yanafuatwa na fedha zinawafikia walengwa bila kugeuzwa matumizi mengine.

Katika kauli yake, Matiko amekosoa utaratibu wa kuelekeza fedha hizo kwenye matumizi mengine kupitia mabadiliko ya bajeti (reallocation), akisisitiza kuwa fedha zilizotengwa kwa ajili ya mikopo ya makundi maalumu hazipaswi kuhamishiwa kwenye shughuli zisizokuwa na uhusiano na madhumuni yake.

Amesema Serikali inapaswa kuweka wazi sababu zilizosababisha Shilingi Bilioni 13.88 kutowafikia wanufaika, pamoja na kuchukua hatua kuhakikisha fedha za mikopo zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na kuwafikia vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.

Hoja ya Matiko inalenga kuimarisha uwajibikaji katika usimamizi wa fedha za umma, hususan mikopo ya asilimia 10 inayotarajiwa kuwa chachu ya kuwawezesha wananchi kiuchumi na kuongeza fursa za kujiajiri kupitia shughuli mbalimbali za maendeleo. 



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...