Na Oscar Assenga, TANGA

Mkandarasi Dimetoclasa Realhope Ltd, chini ya usimamizi wa mshauri elekezi Mekon Arch Consultant Ltd wamekabidhi majengo ya Chuo Kikuu cha Mzumbe, Tawi la Tanga, kilichopo eneo la Gombero, Wilaya ya Mkinga, Mkoa wa Tanga.

Makabidhiano hayo yaliyofanyika Novemba 26, 2026, ni hatua muhimu katika kukamilisha mradi huo na kuweka mazingira ya chuo kuanza shughuli za udahili wa wanafunzi kwa ajili ya mwaka wa masomo 2027/2028.



Akikabidhi funguo za majengo hayo kwa uongozi wa chuo, Meneja Mshauri Elekezi kutoka Kampuni ya Mekon Arch Consultant Ltd, Dkt. Moses Mkony, alisema kuwa mradi huo uliokuwa umepangwa kutekelezwa kwa kipindi cha miezi 18 uliongezewa muda kutokana na changamoto za miundombinu katika eneo la mradi.





Alisema kuwa licha ya changamoto hizo, wamejitahidi kuhakikisha ujenzi unafikia hatua iliyopo sasa, huku baadhi ya maeneo yakiendelea kufanyiwa kazi za mwisho.

"Ujenzi huu ulianza mwaka 2024, na ulipangwa kukamilika ndani ya miezi 18, lakini muda uliongezeka kutokana na mazingira ya miundombinu ya eneo hili. Hata hivyo, tumejitahidi sana kuendana na kasi ya utekelezaji na leo hii tunayo furaha kubwa kukabidhi funguo za majengo ya chuo hiki kwa uongozi wa chuo kwa ajili ya kuendelea na hatua nyingine," alisema Dkt. Mkony.




Dkt. Mkony alisema mradi huo wenye thamani ya shilingi bilioni 12 unajumuisha pia ujenzi wa kituo cha afya kitakachotoa huduma kwa wanafunzi wa chuo hicho pamoja na wakazi wa Kata ya Gombero.



Alisema awali kulikuwa na mpango wa kujenga zahanati, lakini baada ya kufanya tathmini alishauri kujengwa kituo cha afya ili kuongeza wigo wa huduma kwa jamii inayozunguka chuo hicho.



"Awali ilikuwa tujenge zahanati, lakini nilishauri tujenge kituo cha afya kwa ajili ya kuhudumia jamii ya wakazi wa Kata ya Gombero. Hivyo, tumewajengea kituo cha afya chenye viwango vya juu ambapo wakazi wa Gombero watapata huduma hapa hapa na kupunguza safari za kufuata huduma za afya," aliongeza Dkt. Mkony.



Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Prof. William Mwegoha, aliwashukuru wadau wote waliofanikisha ujenzi wa chuo hicho, akisema kuwa utekelezaji wa mradi huo haukuwa rahisi kutokana na mazingira ya eneo husika.



Alisema kuwa walipofika katika eneo la Gombero walikuta pori, lakini kwa ushirikiano wa wadau mbalimbali, wamefanikiwa kufikia hatua hiyo muhimu.



"Tulifika hapa Gombero tulikuta pori, lakini tunawashukuru wadau wote waliofanikisha ujenzi huu. Tumepewa ardhi yenye ukubwa wa ekari 300 bure. Watu wa Tanga ni wakarimu sana. Haikuwa kazi rahisi, lakini tumeshirikiana kwa pamoja mpaka tumefikia hatua hii," alisema Prof. Mwegoha.

Alisema kuwa matarajio ya chuo hicho ni kuanza udahili wa wanafunzi mwaka 2027 kwa ajili ya kujiunga na kampasi hiyo, huku lengo likiwa kufikia jumla ya wanafunzi 10,000 ndani ya kipindi cha miaka 10.



Aliongeza kuwa idadi ya wanafunzi itaongezeka kila mwaka kadiri chuo kitakavyoendelea kupanua shughuli zake za kitaaluma.



Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Gombero, Zuberi Mohamed Zuberi, aliishukuru Serikali kwa uamuzi wa kupeleka mradi huo katika kijiji hicho, akisema kuwa tayari mradi umeanza kuleta manufaa kwa wananchi kupitia fursa za ajira na biashara.



Alisema uwepo wa mradi huo umeongeza mzunguko wa fedha na shughuli za kiuchumi katika eneo hilo, huku akitarajia hali hiyo kuongezeka zaidi mara chuo kitakapoanza kupokea wanafunzi.

"Tunaishukuru sana Serikali kwa kuleta mradi huu kwenye kijiji chetu. Wakazi wa Gombero wamepata fursa nyingi za kazi na biashara. Kata yetu kwa sasa ina mzunguko mkubwa wa fedha na biashara, na tunategemea wakija wanafunzi kutakuwa na mzunguko mkubwa zaidi wa fedha," alisema



Aidha, aliwataka wakazi wa Gombero kuongeza uwekezaji katika biashara na huduma mbalimbali ili kunufaika na fursa zitakazotokana na uwepo wa chuo hicho badala ya kusubiri wageni kutoka maeneo mengine kuja kutumia fursa zilizopo.

Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...