Na Seif Mangwangi, Michuzi TV, Arusha

WABUNGE wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) kutoka Tanzania wamempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuanzisha Wizara mahsusi ya kusimamia masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, wakisema hatua hiyo itaongeza ufanisi wa uratibu na utekelezaji wa masuala ya mtangamano wa kikanda.

Wakizungumza leo, Novemba 27, 2026, katika ofisi za Jumuiya hiyo, wabunge hao wamesema uamuzi huo unatekeleza matakwa ya Ibara ya 8(3)(a) ya Mkataba wa Uanzishaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, inayozitaka nchi wanachama kuwa na Wizara yenye jukumu la kuratibu mawasiliano na Katibu Mkuu wa Jumuiya katika utekelezaji wa mkataba huo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa Wabunge wa EALA kutoka Tanzania, Ansar Abubakar Kachwamba, mageuzi hayo ya kitaasisi ni hatua muhimu katika kuimarisha nafasi ya Tanzania ndani ya Jumuiya hiyo na kuongeza manufaa ya mtangamano kwa wananchi.

Amesema uwepo wa Wizara hiyo utasaidia kuimarisha utekelezaji wa sheria, itifaki na makubaliano ya Jumuiya, pamoja na kurahisisha uratibu wa masuala ya kikanda.

Aidha, wabunge hao wamempongeza Angellah Jasmine Kairuki kwa kuteuliwa kuwa Waziri wa Wizara hiyo, James Kinyasi Millya kuwa Naibu Waziri na Charles Ngeveja Kadonya kuwa Katibu Mkuu.

Wameahidi kuwapatia ushirikiano viongozi hao katika kutekeleza majukumu yao, wakieleza kuwa ushirikiano huo utasaidia kuondoa vikwazo vya biashara na uwekezaji, kupanua fursa za ajira na kuimarisha ushindani wa uchumi wa Tanzania.

Kwa upande wake, Mbunge wa EALA, Dkt. Hasnu Makame, amesema awali masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki yalikuwa yakisimamiwa pamoja na majukumu mengine ya Wizara ya Mambo ya Nje, hali iliyokuwa ikisababisha baadhi ya masuala kutopata kipaumbele kinachostahili.

Naye Mbunge Dkt. Gladness Selema amesema kuanzishwa kwa Wizara hiyo hakutaleta ongezeko la gharama za kiutendaji, kwa kuwa watendaji waliokuwa wakishughulikia masuala ya Jumuiya hiyo wataendelea na majukumu yao.

Tanzania inawakilishwa na wabunge tisa katika Bunge la EALA ambao ni Ansar Kachwamba, Dkt. Hasnu Makame, Dkt. Gladness Selema, Kambaragwe Masato Wassira, Cosato Chumi, Mashaka Ngole, Ali Machano, Nadra Mohammed na Fatma Abdallah Kange.




Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...