.jpeg)
Na Karama Kenyunko, Michuzi TV
UPANDE wa mashtaka katika kesi ya uchochezi inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Tundu Lissu, umeiomba Mahakama Kuu ya Tanzania imhukumu kifungo cha miaka mitano jela au faini kubwa, ukidai kuwa kauli zake zimesababisha athari kubwa kiuchumi na kuleta hofu ya uvunjifu wa amani nchini.
Ombi hilo limewasilishwa mbele ya Jaji Dustan Ndunguru leo Novemba 6, 2026, baada ya Mahakama kumtia hatiani Lissu kwa kosa la uchochezi kinyume na Kifungu cha 390 cha Kanuni ya Adhabu.
Wakili wa Jamhuri, Katuga, akitumia mamlaka ya Kifungu cha 339 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), ameiomba Mahakama izingatie kuwa licha ya mshtakiwa kutokuwa na kumbukumbu za makosa ya awali, vitendo vya uchochezi vimekuwa vikiathiri kwa kiasi kikubwa amani na uchumi wa nchi.
Jamhuri imesema vitendo hivyo vimekuwa vikisababisha uharibifu wa mali za umma na binafsi, huku wananchi wakiwa na hofu inayowazuia kufanya shughuli zao za kiuchumi.
Katika kuimarisha hoja hiyo, upande wa mashtaka umeiomba Mahakama izingatie hotuba na taarifa rasmi ya Tume ya Jaji Chande, ambayo imeonyesha kuwa vurugu na changamoto zilizojitokeza wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 zilisababishwa na kauli za baadhi ya wanasiasa.
Kutokana na athari hizo, Jamhuri imeiomba Mahakama itumie Kifungu cha 35 kinachoruhusu adhabu ya jumla ya kifungo cha miaka mitano jela, ili iwe fundisho na onyo kwa watu wengine wenye nia ya kutenda makosa yanayoweza kuhatarisha amani ya nchi.
Baada ya kuwasilishwa kwa ombi hilo la adhabu, Jaji Ndunguru amempa mshtakiwa fursa ya kujitetea kabla ya kutolewa kwa hukumu ya adhabu.
Lissu ameiomba Mahakama impe muda wa dakika tano ili kufanya mashauriano na mawakili wake kabla ya kuwasilisha maelezo yake ya kuomba nafuu ya adhabu (mitigation).
Jaji Ndunguru amekubali ombi hilo na kutoa nafasi ya mapumziko mafupi kabla ya mchakato huo kuendelea.


Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...