Na Janeth Raphael -MichuziTv

Tanzania na Uganda zimekubaliana kuharakisha hatua za kuondoa vikwazo vya biashara, kupanua masoko ya bidhaa zinazozalishwa katika nchi hizo na kuboresha miundombinu ya usafirishaji, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kukuza biashara, uwekezaji na ushirikiano wa kiuchumi baina ya mataifa hayo mawili.

Makubaliano hayo yamefikiwa Novemba 18, 2026, wakati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, alipoanza ziara ya kitaifa ya siku mbili nchini Uganda kwa mwaliko wa mwenyeji wake, Rais Yoweri Kaguta Museveni. Rais Samia aliwasili Ikulu ya Entebbe na kupokelewa rasmi na Rais Museveni kabla ya kufanya mazungumzo kuhusu masuala mbalimbali ya ushirikiano baina ya nchi hizo.

Katika mazungumzo hayo, viongozi hao wamejadili namna ya kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na kiuchumi, kuongeza biashara na uwekezaji, kurahisisha upatikanaji wa masoko pamoja na kuondoa vikwazo vinavyoathiri usafirishaji wa bidhaa kati ya Tanzania na Uganda.

Akizungumza katika mazungumzo hayo, Rais Samia amesema nchi hizo zimepiga hatua katika utekelezaji wa makubaliano ya awali yaliyohusu biashara, uwekezaji, nishati, usafiri na miundombinu, huku akisisitiza umuhimu wa kuongeza kasi ya utekelezaji wake ili kuleta matokeo yanayotarajiwa.

Ameeleza kuwa changamoto za usafiri na usafirishaji ni miongoni mwa mambo yanayokwamisha ukuaji wa biashara kati ya nchi hizo, akibainisha kuwa Tanzania inaendelea kuboresha miundombinu ya usafiri ikiwemo reli na bandari. Amesema Tanzania ipo tayari kushirikiana na Uganda katika utekelezaji wa mradi wa reli ya kisasa utakaounganisha Isaka na maeneo ya mpakani mwa Uganda, huku maboresho na upanuzi wa Bandari za Dar es Salaam na Tanga vikilenga kurahisisha usafirishaji wa bidhaa katika ukanda wa Afrika Mashariki.

“Tanzania itaendelea kushirikiana na Uganda kwa moyo wa watu wamoja, hatima moja. Sasa ni wakati wa kuharakisha utekelezaji wa tuliyokubaliana,” amesema Rais Samia. Aidha, ameipongeza Uganda kwa kuanza ujenzi wa ubalozi wake katika Mji wa Serikali Dodoma, ikiwa ni nchi ya kwanza kuanza ujenzi wa ubalozi katika mji huo tangu kuzinduliwa kwake.

Kwa upande wake, Rais Museveni amesema biashara kati ya Tanzania na Uganda inapaswa kuzingatia mahitaji na fursa zilizopo katika kila nchi, akitolea mfano wa mchele unaozalishwa Tanzania ambao una soko kubwa nchini Uganda kutokana na ubora na bei yake, pamoja na sukari inayozalishwa Uganda ambayo ina mahitaji katika soko la Tanzania. Amesema Uganda ina ziada ya sukari, hivyo ni muhimu nchi hizo kuruhusu biashara yenye manufaa kwa pande zote mbili.

Rais Museveni ameonya dhidi ya shinikizo la ndani la kuzuia bidhaa kutoka nchi jirani, akieleza kuwa hatua hizo zinaweza kudhoofisha uzalishaji na kuathiri uhusiano wa kibiashara. Amesisitiza umuhimu wa nchi za Afrika kushirikiana katika usimamizi wa rasilimali, uzalishaji na upatikanaji wa masoko kwa manufaa ya wananchi. Viongozi hao pia wamejadili ushirikiano katika sekta ya nishati, hususan usafishaji wa mafuta na miradi ya viwanda.

Rais Museveni amesema Uganda inapanga kujenga kiwanda kidogo cha kusafisha mafuta Hoima na kuunga mkono ujenzi wa kiwanda kikubwa zaidi jijini Tanga, Tanzania. Kwa pamoja, viongozi hao wamehimiza kuharakishwa kwa utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa ili kuimarisha uchumi na kuongeza manufaa ya ushirikiano kwa wananchi wa nchi hizo mbili.































Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...