Na Farida Mangube Morogoro
Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kinatarajia kuadhimisha miaka 50 tangu kuanzishwa kwa mafunzo ya udaktari wa mifugo chuoni hapo, kwa kufanya shughuli mbalimbali zitakazohusisha mbio za marathoni, utoaji wa huduma za uchunguzi na matibabu ya wanyama bila malipo, pamoja na uzinduzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Akizungumza na waandishi wa habari chuoni hapo, Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Rafael Chibunda, amesema tangu kuanzishwa kwa mafunzo hayo, zaidi ya madaktari wa mifugo 1,580 kutoka ndani na nje ya Tanzania wamehitimu katika chuo hicho.
Profesa Chibunda amesema kuwa miongoni mwa shughuli zitakazofanyika katika maadhimisho hayo ni mbio za marathoni, utoaji wa huduma za uchunguzi na matibabu kwa wanyama, uwekaji wa jiwe la msingi katika jengo linalojengwa kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Maendeleo ya Kiuchumi (HEET), pamoja na uzinduzi wa mnara utakaokuwa na majina ya wahitimu wa udaktari wa mifugo wa SUA.
Amesema Makamu wa Rais, Mheshimiwa Deogratius Ndejembi, anatarajiwa kuweka jiwe la msingi katika jengo, kuzindua mnara na baadaye kuhutubia jumuiya ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo pamoja na wakazi wa Morogoro.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Michezo SUA na msimamizi wa VET MARATHON, Charles Lymo, amesema kuwa mbio hizo zitahusisha umbali wa kilomita tano, 10 na 21, huku mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Waziri wa Kilimo na Mifugo, Dkt. Bashiru Ali.
Ameeleza kuwa makundi mbalimbali ya wananchi yatashiriki katika mbio hizo na washindi watapata zawadi mbalimbali zikiwemo medali. Aidha, amewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki katika mbio hizo kwa lengo la kuimarisha afya zao.
Naye Mkuu wa Ndaki ya Tiba ya Wanyama na Sayansi za Afya wa SUA, Profesa Esron Karimuribo, amesema kuwa katika maadhimisho hayo kutakuwa na huduma za uchunguzi na matibabu ya bure kwa wanyama wa kufugwa pamoja na wanyamapori.
Amesema huduma hizo zitatolewa katika halmashauri zote za Mkoa wa Morogoro, huku akiwahimiza wananchi kujitokeza na kupeleka mifugo yao ili inufaike na huduma hizo. Ameeleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya chuo kurudisha shukrani kwa jamii kutokana na ushirikiano unaoendelea kutolewa na wananchi.



Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...