▪️︎ Asema mikataba itasaidia kuzuia migogoro

▪️︎ Asilimia 10 ya makusanyo ya madini kuelekezwa kwenye utafiti


WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, amesisitiza umuhimu wa kurasimisha taratibu za ushirikiano katika shughuli za uchimbaji wa madini kwa kutumia mikataba rasmi, akisema hatua hiyo itasaidia kuweka wazi makubaliano ya pande zinazohusika na kuzuia migogoro.

Dkt. Mwigulu ametoa kauli hiyo leo, Jumamosi, Oktoba 3, 2026, wakati akizungumza katika hafla ya kufunga Maonesho ya Tisa ya Teknolojia ya Madini yaliyofanyika mkoani Geita.

“Twende tuanze kuhamia huku tukiendelea kuaminiana, lakini tuanze kurasimisha taratibu zetu za ushirikiano tunapofanya shughuli hizi za uchimbaji. Wizara imejitahidi mpaka sasa kuweka mikataba, twendeni tutumie mikataba na masharti ya mikataba yale yaliyowekwa,” amesema.

Amesema katika shughuli za uchimbaji zinazohusisha wawekezaji, wenye leseni na wamiliki wa maeneo, makubaliano ya ushirikiano yanapaswa kuwekwa katika mikataba ili kuweka utaratibu wa wazi wa namna pande hizo zitakavyoshirikiana.

Dkt. Mwigulu amesema Serikali itaendelea kusimamia sekta ya madini kwa ushirikiano wa wadau mbalimbali, akisisitiza umuhimu wa kuhakikisha rasilimali za madini zinawanufaisha Watanzania na jamii zinazozunguka maeneo ambako shughuli za uchimbaji zinafanyika.

Amesema Serikali imeweka utaratibu wa kuelekeza asilimia 10 ya makusanyo yatokanayo na madini kwenye utafiti wa kina wa rasilimali madini, akisisitiza umuhimu wa kuongeza utafiti ili Taifa liwe na uelewa mpana wa rasilimali zilizopo.

Dkt. Mwigulu amesema amepokea hoja na maoni mbalimbali yaliyotolewa na wadau katika maonesho hayo, ikiwemo masuala yanayohusu uwajibikaji kwa jamii na miradi ya maendeleo, na kwamba atayafikisha Serikalini kwa ajili ya kufanyiwa kazi kwa mujibu wa taratibu.

Awali, Waziri wa Madini, Antony Mavunde, amesema sekta ya madini inachangia asilimia 10.3 ya Pato la Taifa, huku wachimbaji wadogo wakichangia asilimia 40 ya uzalishaji wa madini nchini.

Mavunde amesema Tanzania Geological Survey imefanya utafiti wa kijiolojia katika asilimia 16 pekee ya eneo la nchi, hivyo Serikali imeelekeza sehemu ya mapato ya sekta ya madini kutumika kuongeza utafiti wa rasilimali zilizopo nchini.

Amesema mwaka uliopita Serikali ilikusanya Sh. trilioni 1.39 kutoka kwenye sekta ya madini na kwamba kwa mwaka huu lengo ni kukusanya Sh. trilioni 1.40. Katika robo ya kwanza ya mwaka, amesema Serikali ililenga kukusanya Sh. bilioni 351 na imekusanya Sh. bilioni 411, sawa na asilimia 117 ya lengo.

Mavunde pia amesema Serikali imeanza kupitia leseni kubwa za madini ambazo hazijaendelezwa, na kwamba hatua za kuzifuta zitaanza kuchukuliwa. Amesema eneo la Sitarike mkoani Katavi ni miongoni mwa maeneo yaliyoanza kushughulikiwa, ambapo maeneo yatakayoachwa yatapelekwa kwa wachimbaji wadogo.

Kwa upande wake, Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji wa Madini Tanzania (FEMATA), John Bina, ameipongeza Serikali kwa hatua mbalimbali inazochukua katika kuwawezesha wachimbaji wadogo na kuimarisha sekta ya madini.

Bina amesema Benki Kuu ya Tanzania imeendelea kununua dhahabu kutoka nchini na kwamba hadi sasa imekusanya zaidi ya tani 35 za dhahabu. Ameomba benki ziendelee kutoa mikopo kwa wachimbaji ili kuwawezesha kuongeza uzalishaji.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha taarifa za kijiolojia na kuchukua hatua dhidi ya taarifa za uongo za kijiolojia zinazoweza kuwapotosha wachimbaji, pamoja na kuendelea kulinda madini ya Tanzanite.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa AngloGold Ashanti–Geita Gold Mining (GGML), Ashraf Suryaningrat, amesema kampuni hiyo itaendelea kushirikiana na Serikali katika kuendeleza ujuzi na vipaji vya Watanzania, biashara na mnyororo wa ugavi wa ndani, teknolojia, ubunifu na maendeleo ya jamii zinazozunguka mgodi.

Maonesho ya Tisa ya Teknolojia ya Madini yamefanyika mkoani Geita yakiwa na kaulimbiu “Madini ni Utajiri, Tuwajibike kwa Pamoja Kufikia Dira ya Taifa 2050.”

Katika maonesho hayo, jumla ya washiriki 1,052 walishiriki, ikilinganishwa na washiriki 400 katika maonesho yaliyopita.











Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, amesema Afrika ina sera, mikakati na makubaliano mazuri ya maendeleo, lakini sasa inapaswa kuongeza kasi ya utekelezaji ili rasilimali na fursa za bara hilo ziwanufaishe wananchi moja kwa moja.

Akizungumza kwa niaba ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Alamein–Africa Business Forum nchini Misri, Makamu wa Rais amesema Afrika inahitaji kuongeza uzalishaji, kujenga uchumi unaostahimili misukosuko ya nje na kuwekeza zaidi katika nishati na miundombinu.

Akitolea mfano Tanzania, ametaja Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) wenye uwezo wa MW 2,115, pamoja na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayoweka mkazo katika nishati, gesi asilia, nishati jadidifu na miundombinu ya kiuchumi.

Makamu wa Rais pia amesisitiza ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi, uwekezaji unaovuka mipaka na kuunganisha uchumi wa nchi za Afrika ili kuongeza uzalishaji, ajira, thamani ya rasilimali na biashara ndani ya bara.

Amesema Tanzania inaendelea kushirikiana na nchi za Afrika Mashariki katika miradi ya kimkakati ya reli, mafuta, nishati na bandari, inayochochea biashara na mtangamano wa kikanda.

Katika jukwaa hilo lililofunguliwa na Rais wa Misri, Mhe. Abdel Fattah El-Sisi, Mwenyekiti wa AU na Rais wa Burundi, Mhe. Évariste Ndayishimiye, ametoa wito wa kugeuza utajiri na fursa za Afrika kuwa matokeo halisi ya kiuchumi ili kufanikisha Agenda 2063.

Mwenyekiti wa Dangote Group, Aliko Dangote, amesisitiza pia umuhimu wa Afrika kuharakisha ukuaji wa viwanda na kuongeza thamani ya rasilimali zake ndani ya bara badala ya kuuza malighafi na kuagiza bidhaa zilizotengenezwa kutokana na malighafi hizo.





Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius John Ndejembi, amewasili Jijini New Alamein nchini Misri kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika Mkutano wa Nane wa Uratibu wa Katikati ya Mwaka wa Umoja wa Afrika (8th African Union Mid-Year Coordination Summit) pamoja na mikutano mingine ya ngazi ya Juu ya Jumuiya za Kiuchumi za Kikanda.

Mkutano huo unafanyika katika mji wa New Alamein, nchini Misri kuanzia tarehe 02 Oktoba 2026, chini ya kaulimbiu “Africa on the Land of El Alamein.”

Katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Al Alamein, Makamu wa Rais amepokelewa na Waziri wa Michezo na Vijana wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri Mhe. Gohar Nabil, Balozi wa Tanzania nchini Misri Mhe. Meja Jenerali Richard Makanzo, pamoja na maafisa mbalimbali wa Serikali ya Misri na Tanzania.

Mara baada ya kuwasili, Mhe. Makamu wa Rais amepokea taarifa kuhusu maandalizi ya Tanzania kushiriki mkutano huo, ambao unawakutanisha viongozi wa juu wa nchi 15 wanachama wa Umoja wa Afrika na Taasisi mbalimbali za Kimataifa na Kikanda kwa lengo la kujadili na kuratibu masuala muhimu yanayohusu maendeleo na ushirikiano wa Bara la Afrika.

Ushiriki wa Tanzania katika mkutano huo ni sehemu ya kuendeleza ushirikiano wake ndani ya Umoja wa Afrika na kuchangia katika mijadala kuhusu utekelezaji wa vipaumbele vya maendeleo ya Bara la Afrika, ikiwemo uchumi, amani, usalama na ushirikiano miongoni mwa mataifa ya Afrika.

Makamu wa Rais anamwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika mkutano huo, ikiwa ni mwendelezo wa Tanzania kushiriki katika majukwaa ya kikanda na kimataifa yanayojadili masuala yenye maslahi kwa Tanzania na Bara la Afrika kwa ujumla.







-Yawataka wananchi kuchangia ada za huduma, yaahidi kuibana Serikali kuhakikisha miradi inakamilika


NA MWANDISHI WETU

KASI ya ujenzi wa miradi ya umwagiliaji imeiridhisha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, huku kamati hiyo ikiahidi kurejea Bungeni kuishinikiza Serikali kuhakikisha inatoa fedha kwa wakati ili miradi hiyo ikamilike kwa wakati.

Akizungumza wakati wa kuhitimisha ziara ya kamati hiyo katika skimu za umwagiliaji za Masimba na Msingi mkoani Singida, Mwenyekiti wa Kamati hiyo ambaye pia ni Mbunge wa Njombe Mjini, Deodatus Philip Mwanyika, amesema kamati imeridhishwa na kasi ya ujenzi wa miundombinu ya miradi hiyo.

Mwanyika amesema kutokana na maendeleo ya ujenzi wa miundombinu hiyo, kamati itaeleza Bunge kuhusu hali halisi ya miradi na kutoa msukumo kwa Serikali ili iweze kutenga na kutoa fedha zinazohitajika kwa wakati.

“Hatuna la kusema, tumeridhika na ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji. Tutaenda kuwapigania Bungeni. Tumepata nguvu ya kwenda kuwaombea fedha ili miradi hii mizuri inayogusa maisha ya mkulima mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla iweze kukamilika,” amesema.

Aidha, amewataka wananchi wanaonufaika na miradi hiyo kuhakikisha wanaitunza na kuchangia ada za huduma za umwagiliaji ili kuhakikisha miundombinu hiyo inadumu na kuendelea kutoa huduma kwa muda mrefu.

“Wananchi, huu mradi ni wetu. Uendelevu wa fedha kuja hapa ni wa kudumu. Kwa mujibu wa miongozo ya Wizara chini ya sheria zinazosimamiwa na Bunge, ada hii ni muhimu sana tulipe ili maboresho ya kazi yaliyofanyika, ikiwemo mifereji, yaweze kuwa ya kudumu,” amesema.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo anayeshughulikia Umwagiliaji na Zana za Kilimo, Athuman Kilundumya, amesema ziara hiyo imekuwa na tija, huku Wizara ikitambua nia ya kamati hiyo ya kufahamu maendeleo ya miradi ya umwagiliaji nchini.

Amesema Serikali ipo tayari kutekeleza na kusimamia maelekezo yatakayotolewa na Bunge kuhusu miradi hiyo.

“Mmeona ubora wa kazi zilizofanyika na miradi mliyotembelea. Baadhi inatekelezwa na wakandarasi wa ndani na Tume imekuwa ikiisimamia ipasavyo kwa kushirikiana na Wizara ili kuweza kupata thamani ya fedha,” amesema.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Raymond Mndolwa, ameihakikishia kamati hiyo kuwa ujenzi wa miradi ya umwagiliaji unaendelea kwa kasi na utaendelea kuleta manufaa na tabasamu kwa wananchi.

“Miradi ya umwagiliaji inakwenda kwa kasi na itaacha tabasamu kwa wananchi kama Rais alivyoelekeza. Tume tumefarijika na ujio wenu na tutahakikisha mnatembelea miradi mingine,” amesema.

Mndolwa amesema kwa sasa kuna zaidi ya miradi 146 ya umwagiliaji inayotekelezwa, ambapo asilimia 70 ya wakandarasi wanaotekeleza miradi hiyo ni wazawa.

Amesema hatua hiyo inaendana na azma ya Serikali ya kuwawezesha wakandarasi wazawa kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama, Hajjat Asia Messos, amewataka wananchi wanaonufaika na miradi ya umwagiliaji kuacha kuuza maeneo yao ili kuhakikisha malengo ya Serikali ya kuendeleza kilimo cha umwagiliaji yanafikiwa.

Amesema Halmashauri hiyo imeanza kupima maeneo husika kwa lengo la kupata mpango bora wa matumizi ya ardhi na tayari imewafikia zaidi ya wananchi 200, huku jumla ya hati 900 za kilimo zikiwa zimepatikana.








Mtoto wa Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Madaraka Nyerere akizungumza wakati wa hafla ya kuwaaga waendesha baiskeli wa Nyerere Cycling Tour na kutoa salamu za familia ya Mwalimu Nyerere. Hafla hiyo ilifanyika jijini Dar es Salaam kabla ya kuanza safari ya Nyerere Cycling Tour kuelekea Butiama, mkoani Mara, ikiwa na lengo la kumuenzi Mwalimu Nyerere na kuunganisha mchezo wa baiskeli na jitihada za kuleta matokeo chanya katika jamii.

Mama Maria Nyerere (katikati) akizungumza wakati alipokutana na waendesha baiskeli wa msafara wa Nyerere Cycling Tour ambapo Vodacom Tanzania Plc waliokwenda kumuaga na kupata baraka zake kabla ya kufanya mashindano ya Vodacom Coastal Classic pamoja na Nyerere Cycling Tour.

 Safari ya Nyerere Cycling Tour kutoka Dar es Salaam hadi Butiama, mkoani Mara, inalenga kumuenzi Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kwa kuunganisha mchezo wa baiskeli na jitihada za kuleta matokeo chanya katika jamii. 

Kupitia safari hiyo, waandaaji na washirika wanatarajia kutekeleza shughuli mbalimbali zinazogusa elimu, afya, uhifadhi wa mazingira, elimu ya fedha na maendeleo ya jamii zikiwemo utoaji wa madawati 1,000, ujenzi wa madarasa 10, ukarabati wa madarasa 40 na upandaji miti, huku shughuli hizo zikitarajiwa kuwafikia zaidi ya watu 25,000. 

Tukio hilo lilishuhudiwa na Meneja mauzo na mkakati wa biashara wa kanda ya Dar es salaam na Pwani Vodacom Tanzania PLC Caleb Majo(kulia), mtoto wa Mwalimu Nyerere - Madaraka Nyerere (wa pili kushoto) na Wilmot Ishengoma, Mkuu wa Kitengo cha Tahadhari wa Stanbic Bank Tanzania (kushoto) pamoja na wadau wengine wa mchezo wa baiskeli.

Tukio hilo lilifanyika wikendi hii, jijini Dar es salaam.

Meneja Mauzo na mkakati wa biashara wa kanda ya Dar es Salaam na Pwani wa Vodacom Tanzania Plc, Caleb Majo akizungumza na waendesha baiskeli wa Nyerere Cycling Tour wakati wa hafla ya kuwaaga na kupata baraka kutoka kwa Mama Maria Nyerere kabla ya kuanza mashindano ya Vodacom Coastal Classic pamoja na safari ya Nyerere Cycling Tour kutoka Dar es Salaam hadi Butiama, mkoani Mara.

 Safari hiyo inalenga kumuenzi Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kupitia mchezo wa baiskeli na shughuli za maendeleo ya jamii.
Waendesha baiskeli wa msafara wa Nyerere Cycling Tour wakimsikiliza Mama Maria Nyerere akizungumza wakati wa hafla ya kuwaaga na kupata baraka zake kabla ya kuanza mashindano ya Vodacom Coastal Classic pamoja na safari ya Nyerere Cycling Tour kutoka Dar es Salaam hadi Butiama, mkoani Mara. Safari hiyo inalenga kumuenzi Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, huku ikiunganisha mchezo wa baiskeli na jitihada za kuleta matokeo chanya katika jamii.
Waendesha baiskeli wa msafara wa Nyerere Cycling Tour wakisikiliza wazungumzaji wakati wa kikao cha kuwaaga na kupata baraka kutoka kwa Mama Maria Nyerere kabla ya kuanza mashindano ya Vodacom Coastal Classic pamoja na safari ya Nyerere Cycling Tour kutoka Dar es Salaam hadi Butiama, mkoani Mara. Safari hiyo inalenga kumuenzi Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, huku ikiunganisha mchezo wa baiskeli na jitihada za kuleta matokeo chanya katika jamii.
Wafanyakazi wa Vodacom Tanzania Plc wakiwa katika picha ya pamoja na Mama Maria Nyerere, Madaraka Nyerere, Meneja Mauzo na Mkakati wa Biashara wa Kanda ya Dar es Salaam na Pwani wa Vodacom Tanzania Plc Caleb Majo na Mkuu wa kitengo cha tahadhari wa Stanbic Bank, Wilmot Ishengoma, baada ya hafla ya kuwaaga na kupata baraka kwa waendesha baiskeli wa Nyerere Cycling Tour jijini Dar es Salaam.

 Safari hiyo kutoka Dar es Salaam hadi Butiama, mkoani Mara, inalenga kumuenzi Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, kupitia mchezo wa baiskeli na shughuli za maendeleo ya jamii.

Na MWANDISHI WETU

WANANCHI, wadau, taasisi, mashirika, kampuni na watu binafsi wameombwa kujitokeza kuchangia harambee yenye lengo la kukusanya Sh milioni 105 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa muhimu vya afya wilayani Kigamboni, Dar es Salaam.

Wito huo umetolewa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Kigamboni, Pendo Abdallah Mahalu, aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya hiyo katika mbio za Afya ya Mama Kigamboni City Marathon, zilizoandaliwa na Taasisi ya Afya ya Mama Foundation kwa lengo la kuchangisha fedha hizo.

Mbio hizo zilizoanzia katika Viwanja vya Tungi Madani, karibu na Daraja la Nyerere, wilayani Kigamboni, zilishirikisha wakimbiaji kutoka klabu mbalimbali za marathon nchini, waliokimbia umbali wa kilomita tano na kilomita 21.

Pendo amesema fedha hizo zitasaidia kununua vifaa tiba muhimu, vikiwemo mashine za kupima na kufuatilia ishara muhimu za uhai wa watoto, vifaa vya kusaidia upumuaji wa watoto wachanga pamoja na zana za kupima kiwango cha oksijeni katika damu.

“Pia zinahitajika seti maalumu za vifaa safi na salama vya kujifungulia kwa ajili ya wajawazito, vitanda vya kujifungulia pamoja na vifaa vya wodi ya uzazi,” amesema Pendo.

Amesema Serikali chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuwekeza kwa kasi katika sekta ya afya kwa kujenga zahanati, vituo vya afya na hospitali za wilaya kote nchini, ingawa ushiriki wa wadau bado unahitajika.

“Ninaipongeza taasisi hii isiyo ya kiserikali ya Afya ya Mama Foundation kwa kuandaa mbio hizi ili kukamilisha pale penye mapungufu na kuhakikisha huduma zinawafikia walengwa,” amesema Pendo.

Aidha, amewaomba wadau zaidi kujitokeza kuchangia na kufanikisha harambee hiyo, yenye lengo la kuboresha huduma za afya wilayani Kigamboni.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Afya ya Mama Foundation, Felister Bwana, amesema taasisi hiyo ilianzishwa kwa lengo kuu la kuhakikisha hakuna mama anayepoteza maisha wakati wa kujifungua.

“Katika kufuatilia huduma za afya ya uzazi Wilaya ya Kigamboni, taasisi ilibaini kuwa vituo vyetu vya afya na zahanati bado vinakabiliwa na uhaba wa vifaa tiba na miundombinu katika kutoa huduma za msingi kwa mama na watoto wachanga,” amesema Felister.

Ameongeza kuwa changamoto hizo ndizo zilizoifanya taasisi hiyo kuandaa mbio hizo zenye kaulimbiu ‘Mama Imara, Taifa Imara’, kwa lengo la kufanya harambee ya kukusanya Sh milioni 105 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba.

Mkurugenzi wa Biashara wa Azania Bank, Yahaya Mbanka, amesema benki hiyo imeahidi kuchangia Sh milioni 5 katika kufanikisha mpango huo.









▪️︎ Aagiza wahusika kuwajibishwa iwapo uzembe utathibitika

▪️︎ Aelekeza kodi ya klinka iondolewe ili kupunguza bei ya saruji


WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, ameagiza kupatiwa taarifa za uchunguzi kuhusu majengo ya Hospitali ya Wilaya ya Bunda yaliyotitia, akitaka hatua zichukuliwe dhidi ya waliohusika iwapo itathibitika kuwa kulikuwa na uzembe.

Dkt. Mwigulu ametoa agizo hilo leo, Jumamosi, Oktoba 3, 2026, wakati akizungumza na wananchi katika Mkutano wa Hadhara uliofanyika Nyamuswa, Wilaya ya Bunda, mkoani Mara, baada ya kukagua ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Bunda.

“Nimeambiwa Waziri wa Afya alishatengeneza timu na ikafanya kazi na TAKUKURU ameshafanyia kazi. Nizipate hizo taarifa ili hawa waliofanya makosa haya wawajibike kule kule walipo. Lazima wawajibike. Hii kuharibu wilaya hii na kuhamishiwa ukaharibu na wilaya nyingine, hii haikubaliki,” amesema.

Amesema wakati wa ukaguzi huo amekuta majengo mawili yakiwa yametitia na kupewa maelezo kuwa hali hiyo imesababishwa na uwepo wa maji katika eneo la mradi pamoja na udongo wa mfinyanzi.

“Namuuliza kwa nini majengo yametitia? Wanasema kwa sababu yamejengwa karibu na chanzo cha maji. Chanzo cha maji kile kimekuja baada ya kujenga msingi? Si kilikuwepo pale pale? ... Wanasema udongo huu ni wa mfinyanzi,” amesema.

Dkt. Mwigulu amesema Serikali itaendelea kufuatilia suala hilo ili kubaini ukweli wa kilichosababisha majengo hayo kutitia na kuhakikisha wananchi hawapati adhabu kutokana na uzembe katika utekelezaji wa miradi ya Serikali.

Amesema Serikali pia inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kukamilisha maeneo yaliyobaki ya ujenzi wa hospitali hiyo ili wananchi waendelee kupata huduma za afya katika eneo lao.

Katika hatua nyingine, Dkt. Mwigulu amesema Serikali imechukua hatua mbalimbali kukabiliana na kupanda kwa bei ya saruji, ikiwemo kuelekeza kuondolewa kwa kodi kwenye klinka, malighafi inayotumika katika uzalishaji wa saruji.

“Nimewaelekeza Mamlaka ya Mapato waondoe kodi kwenye klinka, malighafi inayotumika kwenye uzalishaji wa saruji ili upatikanaji wa saruji uwe wa uhakika na bei iweze kuwa bei himilivu,” amesema.

Amesema Serikali inalenga kuhakikisha upatikanaji wa saruji unaendelea kuwa wa uhakika na bei yake inakuwa himilivu kwa wananchi, akibainisha kuwa katika baadhi ya maeneo bei imekuwa ikipanda hadi kufikia zaidi ya Sh. 25,000, Sh. 27,000 na katika baadhi ya mikoa kufikia Sh. 32,000 kwa mfuko.

Kuhusu huduma za afya, Dkt. Mwigulu amesisitiza kuwa wananchi hawapaswi kuchangishwa fedha za mafuta kwa ajili ya magari ya Serikali, hususan magari ya wagonjwa yanayotumika kuokoa maisha.

“Hatuwezi tukawa na magari ya Serikali yana mafuta, halafu ambulance ya kunusuru maisha ya wagonjwa tuchangishane mafuta. Haya ni mambo ya mazoea ambayo hatutaki kuwa utaratibu wa Serikali,” amesema.

Amesema mwananchi yeyote atakayeombwa fedha za mafuta kwa ajili ya gari la wagonjwa anatakiwa kutoa taarifa kwa mamlaka husika ili hatua zichukuliwe.

Dkt. Mwigulu pia amesisitiza umuhimu wa wagonjwa walio katika hali mbaya kupewa huduma ya dharura mara moja kabla ya kukamilisha taratibu nyingine za kiutawala.

“Mgonjwa aliyezidiwa amefika, hatua ya kwanza apelekwe moja kwa moja kwenye kitanda apate huduma. Hata kumwandikisha mtamwandikisha akiwa ameshapata huduma ya kwanza. Kanusuru kwanza maisha yake. Usifanye itifaki kwenye maisha,” amesema.

Kuhusu upatikanaji wa dawa, amesema Serikali imeendelea kutoa fedha kwa ajili ya ununuzi wa dawa na vifaa tiba, hivyo amewataka viongozi na watendaji wa afya kuhakikisha dawa zinawafikia wananchi waliokusudiwa na matumizi yake yanafuatiliwa ipasavyo.

Hospitali ya Wilaya ya Bunda ilianza kutekelezwa tarehe 8 Mei, 2019, ikiwa ni miongoni mwa hospitali 67 za awamu ya kwanza za halmashauri zilizolenga kusogeza huduma za afya za ngazi ya hospitali karibu na wananchi. Hadi sasa, Serikali imetoa jumla ya Sh. bilioni 5.39 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.

Hospitali hiyo imeanza kutoa huduma mbalimbali, ikiwemo huduma za wagonjwa wa nje, maabara, afya ya uzazi na mtoto, kujifungua, radiolojia, kulaza wagonjwa, huduma za macho, meno na huduma za dharura.











Na Janeth Raphael - MichuziTv

Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imefungua Awamu ya Tatu na ya mwisho ya udahili wa wanafunzi wa Shahada ya Kwanza kwa mwaka wa masomo 2026/2027, huku waombaji ambao hawakupata nafasi katika awamu zilizopita wakipewa fursa nyingine ya kutuma maombi katika programu ambazo bado zina nafasi.

Katibu Mtendaji wa TCU, Prof. Charles Kihampa ametoa TAARIFA hiyo katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dodoma Leo ambapo amesema, dirisha la kutuma maombi katika awamu hiyo litakuwa wazi kuanzia leo Oktoba 3 hadi Oktoba 9, 2026, baada ya Tume kupokea maombi kutoka kwa baadhi ya waombaji ambao hawakufanikiwa kupata udahili katika awamu zilizopita pamoja na vyuo ambavyo bado vina nafasi za udahili.

Tume imeviagiza vyuo vya elimu ya juu nchini kuendelea kutangaza programu ambazo bado zina nafasi ili kuwawezesha waombaji kufanya uchaguzi na kutuma maombi kwa wakati.

TCU imesema hatua hiyo imechukuliwa baada ya kukamilika kwa awamu mbili za awali za udahili, huku ikiwasihi waombaji ambao hawakutuma maombi au hawakupata nafasi katika Awamu ya Pili kutumia fursa hiyo kutuma maombi katika vyuo na programu wanazozipenda.

Awamu ya Tatu itafuata ratiba maalum ambapo vyuo vitawasilisha TCU majina ya wanafunzi waliodahiliwa kati ya Oktoba 13 na 14, 2026, kabla ya majina hayo kutangazwa na vyuo husika Oktoba 17, 2026.

Aidha, TCU imesema waombaji waliodahiliwa katika chuo zaidi ya kimoja katika Awamu ya Pili, pamoja na wale ambao hawakuthibitisha udahili wao katika Awamu ya Kwanza, wanatakiwa kuthibitisha udahili katika chuo kimojawapo kuanzia Oktoba 3 hadi 19, 2026.

Uthibitisho huo utafanyika kwa kutumia namba maalum ya siri iliyotumwa kwa ujumbe mfupi wa simu au kupitia barua pepe ambayo mwombaji alitumia wakati wa kutuma maombi ya udahili.

TCU imeeleza kuwa waombaji ambao hawajapokea namba hiyo wanapaswa kuingia kwenye mifumo ya udahili ya vyuo walivyodahiliwa na kuomba kutumiwa ujumbe wenye namba maalum ya siri ili kukamilisha mchakato wa kuthibitisha udahili.

Pia, waombaji wameelekezwa kufanya uthibitisho kupitia akaunti walizotumia wakati wa kuomba udahili. Orodha ya waombaji waliodahiliwa katika zaidi ya chuo kimoja inapatikana kupitia tovuti ya TCU.

Kwa upande mwingine, TCU imekumbusha kuwa masuala yote yanayohusu udahili au uthibitisho wa udahili yanapaswa kuwasilishwa moja kwa moja kwenye vyuo husika.

Vyuo vyote vimeelekezwa kupokea taarifa za waombaji wanaokumbana na changamoto wakati wa kuthibitisha udahili na kutafuta ufumbuzi wa haraka kwa kuzingatia miongozo na taratibu zilizowekwa.

Kwa ratiba ya Awamu ya Tatu, maombi ya udahili yatafanyika Oktoba 3 hadi 9, vyuo kuwasilisha majina TCU Oktoba 13 hadi 14, kutangaza majina Oktoba 17, huku uthibitisho wa udahili kwa waliodahiliwa zaidi ya chuo kimoja ukifanyika Oktoba 17 hadi 19, 2026.