Na Janeth Raphael - MichuziTv Bungeni 

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, amesema Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kulipa uzito mkubwa suala la Katiba Mpya, huku akisisitiza kuwa dhamira ya kufufua mchakato huo ipo.

Dkt. Mwigulu amesema tayari Serikali imeweka wazi msimamo wake kuhusu umuhimu wa mchakato huo na mwongozo wa kuendeleza suala la Katiba Mpya umetolewa.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo Bungeni wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Tunduru Kaskazini, Mhe. Ado Shaibu, aliyetaka kufahamu ni lini mchakato wa kupata Katiba Mpya utaanza na utakuwa na sura gani.

Akijibu hoja hiyo, Dkt. Mwigulu amesema suala la Katiba Mpya ni miongoni mwa masuala yenye umuhimu mkubwa kwa Watanzania, hivyo Serikali inalichukulia kwa uzito unaostahili.

Amesema dhamira ya Serikali katika kufufua mchakato huo pia imeainishwa katika Ilani ya Uchaguzi, jambo linaloonesha msimamo wa Serikali wa kuhakikisha suala hilo linapatiwa kipaumbele.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, Serikali inaendelea kufanyia kazi mwelekeo uliowekwa ili kuhakikisha mchakato huo unapoendelea unazingatia maslahi mapana ya Watanzania na matarajio yao kuhusu mustakabali wa Taifa.

Kauli hiyo ya Waziri Mkuu imeweka msisitizo mpya kuhusu dhamira ya Serikali ya kuendeleza mchakato wa Katiba Mpya, huku Watanzania wakisubiri hatua na maelekezo zaidi kuhusu namna na muda wa utekelezaji wa mchakato huo.



Kampuni ya Mawasiliano - Yas Tanzania imeahidi kuendelea kushirikiana na Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation (ZMBF) ili kuhakikisha wananchi wengi zaidi visiwani humo wanapata huduma za kibingwa kupitia kambi za afya zinazoratibiwa na taasisi ya ZMBF.

Ahadi hiyo ilitolewa wakati wa ufunguzi wa kambi ya matibabu ya Afya Bora, Maisha Bora kwa kushirikiana na Wizara ya Afya Zanzibar huko Kinduni, Wilaya ya Kaskazini B chini ya udhamini wa Kampuni ya Mawasiliano ya Yas Tanzania. Kupitia kambi zake za afya, taasisi hiyo imefanikiwa kuwafikia zaidi ya watu 30,400 mpaka sasa.

Wakazi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja wanaweza kufanyiwa uchunguzi wa saratani ya matiti na ya shingo ya kizazi katika kambi hiyo, pamoja na kupata huduma za macho, kinywa, masikio, pua na koo. Pia wana fursa ya kuchangia damu kwa hiari.

Akifungua kambi hiyo, Waziri wa Afya Zanzibar, Mhe. Nassor Ahmed Mazrui, alisema kuwaleta wataalamu karibu na wananchi kunapunguza gharama ambazo familia zingetumia kusafiri kutafuta matibabu. Alisema kambi hizo pia zinawapa wananchi fursa ya kujua hali zao za afya na kupata ushauri wa kitaalam kwa wakati.

Mazrui alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kuboresha majengo ya kutolea huduma za afya, vifaa tiba na mazingira ya kazi ya watumishi wa afya. Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Zanzibar, Dkt. Mngereza Mzee Miraji, alisema uwekezaji wa Serikali katika kipindi cha kwanza cha uongozi wa Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi ulihusisha hospitali kumi za wilaya.

Naye, Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora, Bi. Rehema Tukai, alisema Afya Bora, Maisha Bora ni kampeni endelevu na akiwahimiza wananchi kutumia huduma za kinga na tiba zinazotolewa kupitia kambi hizo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Yas Zanzibar, Ndugu Waqid Mohamed Waqid alisema, ni faraja kwa Kampuni ya Mawasiliano ya Yas kushiriki katika masuala ya kijamii nje ya kusogeza huduma za mawasiliano karibu kwa wakazi wa Zanzibar. "Tutaendelea kushirikiana na Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation ili wananchi wengi zaidi waweze kuonana na madaktari bingwa na kupata msaada wa kitaalam."

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Galos Casian Nyimbo, aliwahimiza wakazi wa mkoa huo kujitokeza kwa wingi ili wafanyiwe uchunguzi na kupata ushauri wa madaktari bingwa.
Waziri wa Afya Zanzibar, Mhe. Nassor Ahmed Mazrui, akizungumza wakati wa ufunguzi wa kambi ya matibabu ya Afya Bora, Maisha Bora huko Kinduni, Wilaya ya Kaskazini B, Unguja. Anayeshuhudia kushoto ni Mkuu wa Yas Zanzibar, Bw. Mohamed Waqid. Yas Tanzania imeahidi kuendelea kusaidia kambi za afya zinazoandaliwa na Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation ili wakazi wengi zaidi Zanzibar wapate huduma za madaktari bingwa karibu na maeneo wanayoishi.

Ujenzi wa Ghala Jipya la Bohari ya Dawa (MSD) Kanda ya Kagera lililopo Chato, mkoani Geita, umefikia asilimia 97 ya utekelezaji, hatua inayotarajiwa kuongeza uwezo wa taasisi hiyo kuhifadhi bidhaa za afya kwa ufanisi zaidi katika mikoa ya Kagera, Geita na maeneo jirani pindi litakapoanza kutumika.

Ghala hilo lenye ukubwa wa mita za mraba 4,800 na kugharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 19 linatarajiwa kuwa kitovu muhimu cha kuhifadhi na kusambaza bidhaa za afya, huku likiongeza wigo wa huduma kutoka halmashauri 11 zinazohudumiwa sasa hadi Halmashauri 17.

Meneja wa MSD Kanda ya Kagera, Kalendero Masatu, amesema kukamilika kwa ghala hilo kutawawezesha kuongeza uwezo wa kuhifadhi bidhaa nyingi zaidi katika ubora unaohitajika na kupanua huduma kwa wateja wake.

“Tunatoa huduma kutokea ofisi zetu zilizopo Wilaya ya  Muleba, Mkoa wa Kagera katika mazingira magumu kutokana na ufinyu wa nafasi ya kuhifadhi bidhaa pamoja na changamoto za hali ya hewa, hususan mvua nyingi zinazonyesha katika eneo hilo” amesema Masatu.

Ameeleza kuwa kupitia ghala jipya la Chato, Kanda hiyo itaongeza maeneo ya huduma kwa kujumuisha halmashauri zilizokuwa zikihudumiwa na Kanda ya Mwanza, pamoja na kuongeza halmashauri nyingine mbili kutoka Mkoa wa Kigoma, zilizokuwa zikihudumiwa na Kanda ya Tabora.

“Kwa uwepo wa ghala hili sasa tunaenda kutunza mzigo mkubwa na hivyo tutaweza kuwahudumia wateja wetu kwa upana zaidi. Pia, maeneo haya yako karibu nasi, hivyo tutarahisisha usambazaji na kupunguza gharama ambazo taasisi ilikuwa ikitumia,” amesema Masatu.

Kwa upande wa utekelezaji wa mradi, Mhandisi wa Kampuni ya HAINAN International Ltd, Patrick Laibo, amesema ujenzi ulianza Agosti 20, 2025 na ulipangwa kutekelezwa kwa kipindi cha miezi 14.

Amesema kwa sasa jengo la ofisi limefikia asilimia 99 ya utekelezaji, ghala kuu likiwa katika asilimia 96 kutokana na kazi za mwisho za ufungaji na ukamilishaji wa mfumo wa viyoyozi (AC), huku miundombinu ya nje ikiwa karibu kukamilika kwa asilimia 100.

Ameongeza kuwa kwa ujumla mradi umefikia asilimia 97 na kazi zilizobaki ni za ukamilishaji wa mifumo na maeneo machache ya mradi.

Mbali na kuimarisha miundombinu ya MSD, mradi huo umekuwa chanzo cha ajira kwa wananchi wa Chato, ambapo zaidi ya vijana 100 wamepata fursa za ajira kupitia utekelezaji wake. Mhandisi Laibo amesema mradi huo umechangia pia kuwajengea vijana uwezo na uzoefu wa kitaalamu kupitia ushiriki wao katika shughuli mbalimbali za ujenzi.

Akizungumzia mazingira ya kazi katika ghala hilo, Afisa Huduma kwa Wateja wa MSD Kagera, Julieth Msele, amesema jengo hilo lina nafasi kubwa na mazingira mazuri yatakayorahisisha utoaji wa huduma kwa wateja pamoja na uhifadhi wa bidhaa mbalimbali za afya.

Naye Fundi wa Mifumo ya Njia ya Hewa, Joseph Mwatoine, amesema mradi huo umekuwa fursa muhimu kwa vijana kupata ajira, kujiongezea kipato na kupata uzoefu wa kitaalamu kupitia ushiriki wao katika utekelezaji wa kazi mbalimbali za ujenzi.

Bi. Hellen Juma, mkazi wa Chato ameishukuru Serikali kwa kuleta mradi huo katika eneo hilo, akieleza kuwa mbali na kutoa ajira kwa wananchi, uwepo wa ghala hilo utarahisisha upatikanaji wa dawa kwa vituo vya kutolea huduma za afya vilivyopo maeneo ya jirani.










Mratibu wa Mradi wa Tuinuke Pamoja kutoka Shirika la Aga Khan Foundation, Magreth Lushakuzi, amewahimiza wajasiriamali na vikundi vya wanufaika wa mradi huo katika Halmashauri zote nane za Mkoa wa Dodoma, kutumia maonesho ya biashara yanayofanyika katika maeneo mbalimbali nchini kama fursa ya kutafuta masoko, kujifunza teknolojia mpya na kupanua shughuli zao za biashara.

Akizungumza Novemba 4, 2026, jijini Dodoma, amesema ushiriki wa vikundi hivyo katika Maonesho ya Bidhaa za Viwanda na Biashara umeviwezesha kukutana na wajasiriamali wengine, viongozi wa Serikali na kampuni zinazotengeneza mashine na vifaa vya uzalishaji, hivyo kupata maarifa na fursa za kuboresha bidhaa na kuongeza uwezo wa uzalishaji.

Amesema kupitia Mradi wa Tuinuke Pamoja unaofadhiliwa na Ubalozi wa Ireland nchini Tanzania, Aga Khan Foundation inalenga kuwawezesha wanawake kiuchumi katika ngazi ya jamii kupitia kuwajengea uwezo na kuimarisha shughuli zao za kiuchumi, huku akiwataka wanufaika kutumia elimu na mitandao waliyoipata kukuza biashara zao na kujenga ujasiriamali endelevu.

Kwa upande wake, mnufaika wa Mradi wa Tuinuke Pamoja na mwakilishi wa Kikundi cha Kondoa Women Group mkoani Dodoma, Haruna Makunga, amesema ushiriki wao katika maonesho hayo umewapa fursa ya kutangaza bidhaa zao, kujifunza mbinu za kuboresha uzalishaji na kufahamu taratibu za usajili na viwango vya ubora ili kuongeza ushindani na kupanua wigo wa biashara zao.

Naye mnufaika wa mradi huo kutoka Kikundi cha JUWACHA kilichopo Chamwino Ikulu, amesema mafunzo waliyopata kupitia mradi huo yamewawezesha kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, ikiwemo kujifunza uzalishaji wa mafuta ya mimea. Ameishukuru Serikali kwa kuwapa wakulima wadogo fursa ya kuonesha bidhaa zao na kujifunza kutoka kwa wajasiriamali wengine.

Aidha, Halima Salim Fundi, mwanakikundi wa Tujikomboe Makamaka Women Group, ameishukuru Aga Khan Foundation kwa kuwawezesha kushiriki maonesho hayo, akisema yamewapa fursa ya kujifunza mbinu mpya za kukuza biashara na kuboresha bidhaa zao ili ziweze kushindana katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

Maonesho hayo yamefanyika sambamba na uzinduzi wa Sera ya Maendeleo Endelevu ya Viwanda ya Mwaka 2025 na Sera ya Maendeleo ya Wajasiriamali Ndogo na wa Kati ya Mwaka 2003 (Toleo la Mwaka 2025), ambazo zimezinduliwa rasmi Novemba 4, 2026, jijini Dodoma na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba.

Sera hizo zinalenga kuimarisha uzalishaji, kuongeza thamani ya malighafi za ndani, kuboresha upatikanaji wa mitaji na masoko pamoja na kukuza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya ndani na nje ya nchi.



 

Na. WMA - DODOMA,

Wakala wa Vipimo (WMA) imesema matumizi ya vipimo sahihi ni msingi muhimu wa kuimarisha uzalishaji viwandani, kulinda haki za wafanyabiashara na walaji, na kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya ndani na nje.

Kauli hiyo imetolewa wakati wa uzinduzi wa Sera ya Maendeleo Endelevu ya Viwanda ya Mwaka 2025 na Sera ya Maendeleo ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati ya Mwaka 2003 (Toleo la 2025), uliofanywa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete (JKCC), jijini Dodoma.

Akizungumza katika tukio hilo, Afisa Mtendaji Mkuu wa WMA, Bw. Alban Kihulla, amesema vipimo sahihi vinajenga uaminifu katika biashara kwa kuhakikisha wanunuzi wanapata kiasi cha bidhaa kinacholingana na thamani ya fedha wanazolipa.

Amesema WMA inatekeleza jukumu hilo kwa kukagua bidhaa zilizofungashwa zinazozalishwa nchini pamoja na zinazoagizwa kutoka nje ya nchi kupitia bandari na vituo vya mipakani, ili kuhakikisha kuwa uzito au ujazo ulioainishwa kwenye vifungashio unalingana na kiasi halisi cha bidhaa kilichomo.

“Mnunuzi wa ndani au wa nje ya nchi anapochukua bidhaa yenye nembo ya Made in Tanzania, anatakiwa kupata kile hasa kilichoandikwa kwenye kifungashio. Hiyo ndiyo kazi yetu, na ndiyo sababu tunaziona sera hizi kama fursa ya kuimarisha imani kwa bidhaa za Kitanzania,” amesema Bw. Kihulla.

Ameeleza kuwa WMA pia hushirikiana na taasisi na mashirika ya vipimo ya kikanda na kimataifa katika kuimarisha ulinganifu wa vipimo na kusaidia kupunguza vikwazo vya biashara vinavyohusiana na vipimo.

Akizungumzia biashara ya mazao, amesema WMA inaendelea kuhakiki mizani inayotumika katika vituo vya ununuzi na viwanda vya usindikaji ili kuhakikisha wakulima wanapimiwa kwa usahihi na kulipwa kulingana na uzito halisi wa mazao yao.

“Mkulima anapouza korosho, kahawa au pamba, mizani inayotumika lazima iwe sahihi ili alipwe kwa uzito halisi wa mazao yake. Tunaendelea kuhakiki mizani katika vituo vya ununuzi na viwanda vya usindikaji, na kupambana na ufungashaji wa lumbesa unaomnyima mkulima haki yake,” amesema.

Kwa upande wa wajasiriamali wadogo na wa kati, amesema matumizi ya vipimo sahihi huwasaidia kufungasha bidhaa kwa kiasi kilichoainishwa, kudhibiti upotevu na kujenga uaminifu kwa wateja.

Amesema WMA inaendelea kutoa elimu kupitia njia mbalimbali, zikiwemo redio na televisheni, ili kuwawezesha wajasiriamali na wafanyabiashara kuelewa na kuzingatia matakwa ya vipimo katika shughuli zao. Wakala pia hutumia klabu za vipimo mashuleni kujenga uelewa wa matumizi ya vipimo sahihi tangu umri mdogo.

Aidha, amesema ukuaji wa viwanda na uwekezaji unaongeza mahitaji ya huduma za vipimo, ikiwemo uhakiki wa mizani, mita za umeme na mita za gesi asilia, pamoja na idhini za miundo ya vipimo vinavyokusudiwa kutumika katika shughuli zinazodhibitiwa kisheria.

Ameongeza kuwa WMA inaendelea kuboresha mifumo ya kidijitali ili kurahisisha upatikanaji wa huduma, sambamba na kuimarisha ukaguzi wa bidhaa zinazozalishwa nchini na zinazoagizwa kutoka nje, pamoja na uhakiki wa vipimo vinavyotumika viwandani na katika biashara.

“Tunawaomba wananchi wahakikishe mizani na vipimo wanavyotumia vina alama ya uhakiki ya WMA, na watoe taarifa pale wanapoona kipimo kisicho sahihi. Kipimo sahihi ni haki ya kila mwananchi,” amesisitiza.

WMA ni miongoni mwa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara zilizoshiriki maonesho na kongamano lililoambatana na uzinduzi huo. Wananchi na wafanyabiashara waliotembelea banda la Wakala walipata elimu kuhusu matumizi ya vipimo sahihi na huduma zinazotolewa na WMA.

Sera hizo zinalenga kuimarisha maendeleo ya viwanda na ujasiriamali kwa kuongeza uzalishaji, thamani ya malighafi za ndani, fursa za ajira na upatikanaji wa mitaji na masoko kwa wajasiriamali, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.




Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa, Bw. Ally Akida (Wapili kushoto), Meneja wa Mfuko wa PSSSF Kanda ya Kati, Bw. Lulyalya Sayi (Wanne kushoto), na Mkuu wa Shule ya Sekondari Kimaghai A, Bi. Eudia Medaa (Watano kushoto) na baadhi ya viongozi wa wilaya na walimu wa shule hiyo, wakiungana kuzindua, mradi wa maji uliofadhiliwa na Mfuko wa PSSSF katika hafla ya uzinduzi iliyofanyika shuleni hapo Novemba 4, 2026.
Meneja wa Mfuko wa PSSSF Kanda ya Kati, Bw. Lulyaya Sayi (Aliyesimama) akizungumza katika hafla ya kukabidhi mradi wa kisima Cha maji katika Shule ya Sekondari Kimaghai A, Wilayani Mpwapwa jijini Dodoma Novemba 4, 2026.


Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa, Bw, Ally Akida (Aliyesimama) akizungumza katika hafla ya kukabidhi mradi wa kisima Cha maji uliofadhiliwa na Mfuko wa PSSSF katika Shule ya Sekondari Kimaghai A, jijini Dodoma. Hafla hiyo imefanyika Novemba 4, 2026.
Meneja wa PSSSF Kanda ya Kati, Bw, Lulyaya Sayi, Kaimu Afisa Elimu wa Halmashauri ya mji Dodoma Bw, Yasin Mponda, Mkuu wa Shule ya Msingi Uhuru wakishuhudia uwepo wa maji kwa uhakika baada ya kukamilika kwa mradi huo katika Shule ya Msingi Uhuru.
Picha ya pamoja ikionyesha Meneja wa PSSSF Kanda ya Kati, Bw. Lulyaya Sayi, Kaimu Afisa Elimu wa Halmashauri ya Mji wa Dodoma, Bw. Yassin Mponda, Mkuu wa Shule ya Msingi Uhuru, Bi. Agatha Mosha, pamoja na watumishi, wazazi, na wanafunzi waliohudhuria katika uzinduzi wa mradi wa maji katika Shule ya Msingi Uhuru.
Kaimu Afsa Elimu wa Halmashauri ya Mji wa Dodoma, Bw, Yasin Mponda akizungumza katika hafla ya kukabidhi mradi mradi wa kisima Cha maji katika Shule ya Msingi Uhuru, Dodoma.



Meneja wa PSSSF Kanda ya Kati, Bw, Lulyaya Sayi akizungumza katika hafla ya kukabidhi mradi wa kisima Cha maji katika Shule ya Msingi Uhuru.





*Miradi Kunifaisha zaidi ya Watu 1000

*Wanafunzi Waanzisha Bustani Kuboresha Lishe

Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) umekabidhi miradi miwili ya visima vya maji vyenye thamani ya Shilingi milioni 55 katika Shule ya Sekondari Kimaghai, Mpwapwa, na Shule ya Msingi Uhuru, jijini Dodoma, inayotarajiwa kunufaisha zaidi ya watu 1,000.

Akizungumza wakati wa makabidhiano ya mradi wa Kimaghai A, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa, Bw. Ally Akida, aliishukuru PSSSF kwa kutatua changamoto ya muda mrefu ya maji, akieleza kuwa mradi huo utanufaisha zaidi ya watu 600.

Naye Kaimu Afisa Elimu wa Jiji la Dodoma, Bw. Yasin Mponda, aliipongeza PSSSF kwa kukubali ombi la Shule ya Msingi Uhuru, akieleza kuwa Mfuko umeifanya shule hiyo kujiona inathaminiwa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Msingi Uhuru, Bi. Agatha Mosha, aliishukuru PSSSF kwa mradi huo ambao umewezesha kuanzishwa kwa kilimo cha mbogamboga kwa ajili ya kuboresha lishe ya wanafunzi na unatarajiwa kunufaisha zaidi ya watu 500.

Makabidhiano ya miradi hiyo yalifanyika tarehe 3 na 4 Novemba 2026, yakiongozwa na Meneja wa PSSSF Kanda ya Kati, Bw. Lulyaya Sayi, aliyewataka wanafunzi, walimu na wananchi kutunza visima na miundombinu yake ili iendelee kutoa huduma kwa muda mrefu.

Jeshi la Polisi Wilaya ya Ulanga limeendelea kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati yake na wananchi kupitia programu ya “Ongea na Kamanda” iliyofanyika katika Kijiji cha Kituti, Kata ya Ruaha, wilayani Ulanga, Mkoa wa Morogoro kwa lengo la kujenga jamii yenye uelewa wa mambo ya amani na usalama pamoja na kuzuia vitendo vya uhalifu.

Akitoa Elimu hiyo, Mkuu wa Polisi Wilaya ya Ulanga, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP) Deogratius Challe, alieleza maana na malengo ya kampeni hiyo, akisisitiza umuhimu wa wananchi kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kudumisha usalama na kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu kwa wakati ili hatua sitahiki ziwezekuchukuliwa kwa wakati.

Katika programu hiyo, wananchi walipatiwa elimu mbalimbali kuhusu utii wa sheria bila shuruti, usalama migodini, utunzaji wa fedha, ukatili wa kijinsia, utunzaji wa eneo la tukio la uhalifu, utoaji wa taarifa za uhalifu.

Aidha Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa Polisi Wilaya akatumia fursa hiyo kuwakumbusha wananchi wanaomiliki silaha kinyume na utaratibu kusalimisha silaha hizo katika vituo vya Polisi na ofisi za serikali za vijiji huku akiwakumbusha na tahadhari dhidi ya mvua za El Niño.

Licha ya ananchi walilipongeza Jeshi la Polisi kwa juhudi zake za kuimarisha usalama na kudumisha amani katika jamii wananchi hao, wameliomba Jeshi hilo kuendelea kutoa elimu ili kuwajengea uelewa Juu ya mambo ya kiusalama.

Kwa ujumla, programu ya “Ongea na Kamanda” imeendelea kuwa jukwaa muhimu la mawasiliano kati ya Jeshi la Polisi na wananchi, likichochea ushirikiano katika kuzuia uhalifu, kutatua changamoto za kiusalama na kujenga jamii yenye amani, utulivu na usalama.







Pamela Mollel,Arusha

Arusha .Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) imehimiza kuimarishwa kwa ushirikiano wa taasisi mbalimbali ili kuondoa vikwazo vinavyochelewesha ulipaji wa fidia za bima na kuhakikisha wananchi wanapata haki zao kwa wakati.

Akizungumza wakati wa kikao kazi cha wadau wa sekta ya bima Kanda ya Kaskazini jijini Arusha, Meneja wa TIRA Kanda ya Kaskazini, Dkt. Emmanuel Lupilya, amesema ulipaji wa fidia ndiyo kipimo muhimu cha imani ya wananchi kwa sekta ya bima.

Amesisitiza kuwa bima haipaswi kuishia katika kukusanya malipo ya awali, bali lazima itimize wajibu wake wa kumlinda mwananchi pale anapokumbwa na janga.

Dkt. Lupilya amependekeza kuanzishwa kwa 'Mfumo wa Kitaifa wa Uratibu wa Madai ya Bima (National Insurance Claims Coordination Framework)' utakaounganisha kampuni za bima na taasisi muhimu, ikiwemo Jeshi la Polisi, hospitali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na wadau wengine, ili kurahisisha upatikanaji wa taarifa na kuharakisha maamuzi ya madai.

Ameeleza kuwa mfumo huo utasaidia pia kuboresha takwimu za madai yaliyolipwa, yaliyocheleweshwa na yale yenye viashiria vya udanganyifu, huku akisisitiza umuhimu wa kila taasisi kutekeleza wajibu wake na kutoa taarifa kwa wakati.

Dkt. Lupilya amesisitiza kuwa mafanikio ya sekta ya bima hayapimwi kwa idadi ya watu wanaokata bima pekee, bali pia kwa kasi, uwazi na haki katika kulipa fidia pale wanapohitaji huduma hiyo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa TIRA, Ponziano Rusiano Lukosi, amebainisha changamoto zinazochangia migogoro ya madai, zikiwemo magari kuwekewa bima bila ukaguzi wa kutosha, makadirio yasiyo halisi ya gharama za matengenezo na ucheleweshaji wa taarifa za uchunguzi wa ajali.

Naye Mchunguzi Mwandamizi wa TAKUKURU Arusha, Julieth Mwambola, amewataka wananchi kuripoti vitendo vya rushwa vinavyohusiana na ufuatiliaji wa madai ya bima kupitia namba ya bure 113, huku akizihimiza kampuni za bima kutoa taarifa za viashiria vya udanganyifu.

Kikao kazi hicho kimewakutanisha kampuni za bima, Jeshi la Polisi, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, LATRA, NHIF, wawakilishi wa gereji, mawakala wa bima na taasisi nyingine zinazoshiriki katika mnyororo wa kushughulikia madai ya fidia.

Meneja wa TIRA Kanda ya Kaskazini, Dkt. Emmanuel Lupilya,akizungumza kwenye kikao kazi hicho kilichofanyika jijini Arusha.





Na Mwandishi Wetu, Morogoro
WAWEKEZAJI wafanyabiashara na wasafirishaji wa mizigo mkoani Morogoro wameitaka Serikali kupitia Shirika la Reli Tanzania (TRC), kuongeza kasi na ufanisi wa usafirishaji wa mizigo kwa kutumia Reli ya Kisasa ya SGR ili kupunguza gharama za biashara na kuchochea ukuaji wa uchumi.

Wamesema pamoja na kuongezeka kwa mahitaji ya usafirishaji wa mizigo kwa njia ya reli, bado kuna umuhimu wa kuboresha miundombinu na huduma zinazotolewa ili kuhakikisha wafanyabiashara na wawekezaji wanapata huduma kwa wakati na kwa uhakika.

wamesema hatua hiyo itasaidia kupunguza muda wa kusafirisha mizigo kutoka eneo moja kwenda jingine, kupunguza gharama za uendeshaji wa biashara na kuongeza ushindani katika sekta ya usafirishaji nchini.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Katibu Tawala wa Mkoa huo, Dkt. Mussa Ali Mussa, kwa kushirikiana na Katibu Tawala Msaidizi anayeshughulikia masuala ya biashara, Beatrice Njau, wameeleza changamoto zinazokabili miundombinu ya reli na kusisitiza umuhimu wa kuzitatua ili kuongeza ufanisi wa huduma.

Mwakilishi wa Bandari Kavu ya Free Zone Mkoa Morogoro Mansoor Hilari Hilari amesema kuboreshwa kwa miundombinu hiyo kutakuwa na mchango mkubwa katika kurahisisha shughuli za kiuchumi, hususan kwa wafanyabiashara na wawekezaji wanaotegemea usafiri wa reli kusafirisha bidhaa zao.

Kwa upande wake, mwakilishi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Raphael Bwire, amesema shirika hilo linaendelea na juhudi za kupanua na kuboresha miundombinu ya reli ili kuongeza uwezo wa kuhudumia mahitaji ya usafirishaji wa mizigo yanayoendelea kukua.

Amesema hatua hizo ni sehemu ya jitihada za kuimarisha huduma za reli na kuhakikisha zinakidhi mahitaji ya wananchi, wafanyabiashara na sekta mbalimbali za kiuchumi.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Nahodha Mussa Mandia, amesema bodi hiyo itaendelea kuishauri Serikali kuhusu umuhimu wa kuboresha miundombinu ya reli ili kuimarisha mfumo mzima wa usafirishaji hasa katika usafirishaji wa makasha kutoka Bandari ya Dar es Salaam na kuweka kwenye Bandari ya Free Zone mkoani Morogoro.

Amesema uwekezaji katika miundombinu ya usafirishaji ni muhimu katika kuchochea biashara, kuongeza ufanisi wa usafirishaji wa mizigo na kuvutia wawekezaji zaidi.








Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
WANAFUNZI wa vyuo vikuu nchini wametakiwa kutumia teknolojia ya akili bandia (AI) kama nyenzo ya kuboresha ujifunzaji na tafiti zao badala ya kuitegemea kuwaandikia kazi za kitaaluma, hali inayoweza kudhoofisha uwezo wao wa kufikiri kwa kina na kufanya tafiti huru.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), Profesa Eliamani Mathew Sedoyeka, aliyesema matumizi sahihi ya AI yanaweza kuongeza ufanisi wa tafiti kwa kuwasaidia wanafunzi kubaini mapungufu, kupata taarifa na kuboresha ubora wa kazi zao za kitaaluma.

Hata hivyo, amesema kumekuwa na tabia ya baadhi ya wanafunzi, hususan wa masomo ya uzamili, kutumia teknolojia hiyo kuwaandikia tasnifu na makala za kitaaluma badala ya kufanya utafiti na kuandaa kazi hizo wenyewe.

Amesema mwenendo huo unaweza kuathiri ubora, uhalisia na uaminifu wa tafiti za kitaaluma, huku akisisitiza umuhimu wa wanafunzi kuitumia AI kama nyenzo ya kuwaongezea maarifa badala ya kuchukua nafasi ya uwezo wao wa kufikiri na kuchambua mambo.

Ameongeza kuwa mifumo ya uchunguzi wa kazi za kitaaluma kama Turnitin inaweza kusaidia katika kukagua uhalisia wa kazi hizo na kubaini masuala yanayohitaji uchunguzi zaidi.

Profesa Sedoyeka amewataka wanafunzi na wahadhiri kujifunza matumizi sahihi ya teknolojia hiyo ili kunufaika na maendeleo ya kidijitali bila kupoteza misingi ya utafiti, ubunifu na fikra huru.

Kwa upande wake, mwanafunzi wa Shahada ya Uzamili ya Uongozi, Sharfani Zuberi, amesema matumizi yasiyo sahihi ya AI yanaweza kuwafanya wanafunzi kuwa tegemezi kwa teknolojia hiyo na kushindwa kutumia uwezo wao binafsi katika kutatua changamoto za kitaaluma.

Amesema ni muhimu wanafunzi kuitumia kama nyenzo ya kuongeza uelewa na kurahisisha mchakato wa kujifunza na kufanya tafiti, badala ya kuifanya kuwa mbadala wa maarifa na uwezo wao.

Naye mwanafunzi wa Shahada ya Uzamili ya Mipango na Usimamizi wa Miradi, Imtihal Salum Taufiq, amesema katika utafiti wake unaohusu miundombinu ya barabara na mchango wake katika kuboresha mtiririko wa magari na usalama barabarani, amekutana na changamoto mbalimbali.

Amezitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni pamoja na kupata ushirikiano kutoka kwa baadhi ya wadau wa Serikali na jamii, pamoja na changamoto za kiteknolojia zinazoweza kuathiri utekelezaji wa utafiti wake.


Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA) umeeleza kuwa unaendelea kuimarisha usimamizi na ukaguzi wa vipimo vinavyotumika viwandani na katika shughuli za biashara ili kuhakikisha wazalishaji na wafanyabiashara wanazingatia matakwa ya Sheria ya Vipimo, hatua inayolenga kulinda haki za wanunuzi na wauzaji pamoja na kujenga mazingira ya biashara yenye usawa.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Sera ya Maendeleo ya Viwanda ya mwaka 2025 na sera ya jasiriamali ndogo na za kati Jijini Dodoma, Afisa Mtendaji Mkuu wa WMA, Alban Kihulla, amesema wakala huo unashirikiana na viwanda na wajasiriamali kuhakikisha mizani ya kupimia inavyotumika katika shughuli zao inakaguliwa na kuhakikiwa kwa mujibu wa Sheria ya Vipimo, Sura ya 340.

Amesema katika shughuli za viwandani, WMA itasimamia matumizi sahihi ya mizani mikubwa inayotumika kupimia malighafi, vifaa vya kupimia mafuta na pampu za mafuta ili kuhakikisha kiasi kinachopimwa kinaendana na kiwango halisi kinachotakiwa katika miamala ya kibiashara.

Aidha, amesema wakala huo utaendelea kukagua bidhaa zilizofungashwa kwa kuzingatia matakwa ya kisheria kuhusu vipimo, ikiwemo kuhakikisha kiasi cha bidhaa kinachotajwa kwenye kifungashio kinaendana na uzito au ujazo halisi uliomo, pamoja na kusimamia vipimo vya urefu na vipimo vingine vinavyotumika katika biashara.

Kwa upande wa wajasiriamali wadogo na wa kati, Kihulla amesema WMA imeongeza utoaji wa elimu kuhusu umuhimu wa kutumia mizani na vifaa vingine vya kupimia vilivyohakikiwa kisheria, akibainisha kuwa matumizi ya vipimo visivyo sahihi yanaweza kusababisha mmoja wa wahusika katika biashara kupata hasara na kuathiri uaminifu baina ya wafanyabiashara na wateja.

Ameongeza kuwa matumizi ya vipimo sahihi ni muhimu katika kuweka mazingira ya ushindani wa haki, kulinda maslahi ya watumiaji na kuhakikisha wafanyabiashara wanapata stahiki zao kulingana na kiasi cha bidhaa wanachouza au kununua.

Katika hatua nyingine, amesema WMA itaendelea kushirikiana na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kuwawezesha vijana kutumia ujuzi wao kubuni na kutengeneza vifaa vya vipimo nchini, badala ya kutegemea kwa kiwango kikubwa vifaa vinavyoagizwa kutoka nje.



GENEVA, Uswisi: Tanzania kesho, Novemba 5, 2026, itakuwa katika jukwaa la kimataifa la haki za binadamu jijini Geneva, itakapowasilisha mafanikio, mageuzi na hatua zilizotekelezwa katika kuimarisha utawala wa sheria, upatikanaji wa haki na ustawi wa wananchi, katika Mapitio ya Nne ya Hali ya Haki za Binadamu (Universal Periodic Review – UPR) ya Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa.

Ushiriki huo unaipa Tanzania fursa ya kueleza mbele ya jumuiya ya kimataifa utekelezaji wa mapendekezo yaliyotolewa katika mapitio yaliyopita, hatua zilizochukuliwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita na maeneo yanayoendelea kupewa kipaumbele katika kuimarisha mifumo ya ulinzi na utekelezaji wa haki za binadamu nchini.


Akizungumza na waandishi wa habari jijini Geneva kuhusu ushiriki wa Tanzania katika mapitio hayo, Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Abdallah Ulega, amesema Serikali inaendelea kuimarisha diplomasia, utawala bora na ulinzi wa haki za binadamu chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kupitia falsafa ya Maridhiano, Ustahimilivu, Mageuzi na Kujenga Upya (4Rs).

Amesema mapitio hayo ni fursa muhimu kwa Tanzania kueleza mafanikio yaliyopatikana, hatua zilizochukuliwa kutekeleza mapendekezo yaliyokubaliwa katika duru zilizopita, pamoja na kuonesha dhamira ya kuendelea kuimarisha haki za binadamu na ustawi wa wananchi.


Tanzania inashiriki katika duru ya nne ya UPR ikiwa tayari imeshiriki katika mapitio matatu yaliyotangulia mwaka 2011, 2016 na 2021. Katika duru ya tatu, iliyofanyika mwaka 2021, nchi ilipokea mapendekezo 252 kutoka kwa mataifa mbalimbali, ambapo iliridhia mapendekezo 187, yakiwemo 20 yaliyokubaliwa kwa sehemu, huku 65 yakikosa kuridhiwa.


Tangu mapitio hayo, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali katika maeneo yanayogusa ustawi wa wananchi, yakiwemo utawala wa sheria, upatikanaji wa haki, afya, elimu, upatikanaji wa maji na miundombinu. Hatua hizo ni sehemu ya juhudi za kuimarisha mazingira ya haki, usawa wa fursa na maendeleo jumuishi.

Maandalizi ya Taarifa ya Nne ya Kitaifa ya UPR yamehusisha Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kwa kushirikisha Wizara, Idara na Taasisi za Serikali, Mahakama, asasi za kiraia, taasisi za kidini, mashirika ya watu wenye ulemavu na wadau wengine wa haki za binadamu.

Taarifa hiyo inaainisha mafanikio, mageuzi na hatua zilizochukuliwa katika kipindi cha mwaka 2021/22 hadi 2026, ikieleza juhudi za kuimarisha mifumo ya haki za binadamu kama msingi wa Maendeleo endelevu

Ushiriki wa Tanzania katika mapitio hayo unaendana pia na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayolenga kujenga taifa lenye ustawi, haki, ujumuishi na uwezo wa kujitegemea. Dira hiyo inaweka utu wa binadamu, usawa wa fursa na maendeleo ya wananchi katika msingi wa mipango ya maendeleo ya Taifa.

Kwa mantiki hiyo, ushiriki wa Tanzania katika UPR unaunganisha ajenda ya haki za binadamu na malengo mapana ya maendeleo ya Taifa, kwa kuzingatia kuwa upatikanaji wa haki, huduma muhimu na fursa za maendeleo ni mambo yanayochangia ustawi wa wananchi.

UPR ni utaratibu wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa unaozipa nchi zote wanachama fursa ya kupitia hali ya haki za binadamu katika nchi zao kwa misingi ya usawa. Kupitia utaratibu huo, nchi huwasilisha taarifa kuhusu hatua zilizochukuliwa, mafanikio na changamoto zilizopo, huku mataifa mengine yakitoa mapendekezo yanayolenga kuimarisha zaidi utekelezaji wa haki za binadamu.

Mapitio ya Nne ya Tanzania yanafanyika katika Kikao cha 53 cha Kikundi Kazi cha UPR kinachoendelea jijini Geneva kuanzia Novemba 2 hadi 13, 2026. Kupitia ushiriki huo, Tanzania inatarajia kuwasilisha hatua ilizochukua katika kipindi cha miaka mitano iliyopita na kuendeleza ushiriki wake katika juhudi za kimataifa za kukuza na kulinda haki za binadamu.