
kalala junior, mwana wa mwanamuziki mkongwe hamza kalala 'komando wa shida', akiongoza kikosi cha mchinga generation kwenye tamasha la sauti za busara. Soma zaidi..
MCHINGA GENERATION BADO WAMO
SIKU chache baada ya kukimbiwa na mwimbaji Ali Choki “Mzee wa Farasi” aliyetimkia African Stars, bendi ya Mchinga Generation imeendelea kuonesha umahiri kwa kufanya vitu vikubwa kwenye tamasha la Sauti za Busara linaloendelea visiwani hapa kwenye ukumbi wa Ngome Kongwe usiku wa jana.
Kinyume na matarajio ya wengi kwamba Mchinga ingepwaya baada ya ‘Mzee wa Farasi’ kuingia mitini, vijana hao waliinua mamia ya washabiki waliohudhuria tamasha hilo kwa kumwaga mtindo wao wa ‘Timbatimba’ ikiwa ni pamoja na staili yao mpya ya ‘Kizunguzungu’ kwa ustadi wa hali ya juu jukwaani.
Wakiongozwa na mtunzi na mwimbaji mahiri Roget Hegga ‘Caterpillar’, huku akisaidiana na Rashidi Mwenzingo, Bashiri Uhadi, Hadija Mnoga ‘Kimobitel’ na rapa Kalala Junior, hakuna kilichoharibika.
Wanenguaji wake pia, hawakubaki nyuma kwa kulisakata sebene wakiwa pamoja na akina Bonzo Kwembe na wenzie kwa pozi na mbwembwe zilizoongozwa na mnenguaji Aaliya aliyehamia Mchinga toka African Revolution.
Mchinga ambao walipanda jukwaani majira ya saa sita kasoro usiku , walipagawisha na kibao chao cha nguzo tano za upendo huku wakilishambulia jukwaa bila kupumzika hadi majira ya saa nane usiku.
Mamia ya mashabiki, wengi wao wakiwa ni watalii toka sehemu mbalimbali za dunia, walipagawishwa kwa miondoko ya ‘Timbatimba’ kiasi hata ya kuomba muda uongezwe ili wafaidi zaidi.
Hiyo ilikuwa ni mojawapo ya shamra shamra za siku ya pili ya tamash hili la kila mwaka, ambalo linazidi kujiongezea umaarufu kwa msisimko na ustadi wa wasanii walioalikwa kutoka ndani na nje ya nchi.
Kabla ya Mchinga kupanda jukwaani, kundi la Black Roses toka nchini Swaziland liliacha gumzo kwenye visiwa hivi vya karafuu kwa muziki wao ulio katika mahadhi ya reggae na bongo muffin.
Bi. Kidude naye na kundi lake na ngoma ya unyago aliacha mashabiki hoi kwa kupiga ngoma na kuimba huku kinamama kama sita hivi wakikata mauno jukwaani, na kuonesha namna gani mwali hufundwa.
Kikundi cha Culture Club kilipanda jukwaani pia na kuonesha namna taarabu asilia inavyopigwa. Kabla ya hapo alipanda msanii Atongo Zimba toka Ghana na gita lake la asili, baada ya kundi la Zemkala kutumbuiza.
Usiku wa kuamkia leo, vijana wa mchiriku, Jagwa Music, watapanda jukwaani kuonesha nini walikifanya nchini Uingereza walikoalikwa mwaka jana.Mbali na Jangwa Music Wagosi wa Kaya pia wakutakuwepo kuzikonga nyoyo za mashabiki wa muziki visiwani hapa.
Wengine ni Salome Kiwaya na Sakis Stars toka Dodoma, hali kadhalika Mandojo na Domo Kaya, Ukoo Flani Maumau, News Sound band, Black Roots, The Shrine Synchrosystem na Taffetas.
kha ilikuwa tamu hiyo! nimehudhuria mara (miaka - miwili)...naelewa mnavokula raha mida hii...asante kwa brief!
ReplyDeleteUnajua kama ipo documented on tape, vcd, dvd? I would sincerely like to get a copy of this event. Huku ughaibuni vitu kama hivi ninavimiss sana tu!!!
ReplyDelete