
jk na mwenyeji wake rais pierre nkurunzinza wakipiga ngoma ya kirundi wakati wa tafrija maalum kwa heshima ya jk bujumbura jana usiku wakati wa kilele cha ziara yake ya kiserikali nchini humo. ifuatayo ni hotuba ya jk kwenye dhifa ya kitaifa aloandaliwa na mwenyeji wake
HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA , MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE, KWENYE DHIFA YA KITAIFA ILIYOANDALIWA NA MWENYEJI WAKE, RAIS PIERRE NKURUNZIZA WA BURUNDI, BUJUMBURA , TAREHE 19 JUNI, 2007
Mheshimiwa Pierre Nkurunziza
Rais wa Jamhuri ya Burundi ;
Mheshimiwa Mama Denise Nkurunziza;
Mheshimiwa Martin Nduwimana
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Burundi ;
Waheshimiwa Mawaziri;
Waheshimiwa Mabalozi;
Wageni Waalikwa;
Mabibi na Mabwana.
Awali ya yote napenda kuelezea furaha kubwa tuliyonayo mimi na wenzangu niliofuatana nao kwa mapokezi makubwa na mazuri tuliyoyapata leo. Wakazi wa Bujumbura wametupokea kwa furaha, ukarimu na upendo usio kifani kiasi kwamba nakosa neno zuri la kuelezea shukrani zetu kwenu. Ninachoweza kusema ni asanteni sana . Murakoze chaane.
Ukarimu mliotuonyesha leo Mheshimiwa Rais, umetudhihirishia wazi jinsi gani wananchi wa Burundi mlivyo na moyo wa upendo kwa wageni. Aidha, ni ushahidi tosha wa jinsi mnavyojali na kuthamini udugu na urafiki uliopo baina ya nchi zetu mbili. Jambo hili limetufariji sana mimi na wenzangu na kutufanya tujione kweli tupo nyumbani. Kwa mara nyingine tena nasema murakoze chaane.
Mheshimiwa Rais;
Napenda kutumia fursa hii kukushukuru wewe binafsi kwa kunialika na kwa maneno mazuri uliyoyasema kwenye
hotuba yako kunihusu mimi na nchi yangu ya Tanzania . Naamini maneno hayo yametoka rohoni mwako. Kwa niaba ya wananchi wote wa Tanzania nakushukuru sana .
Hata hivyo, napenda kusema kuwa kama kuna jambo jema Watanzania tumelifanya kwa nchi yenu, basi tumefanya hivyo kama wajibu wetu na wajibu wa nchi yetu. Watanzania na wananchi wa Burundi ni watu wamoja na ni ndugu. Tunao wajibu wa kusaidiana na hasa pale mmoja wetu anapokuwa katika matatizo. Ndiyo maana Watanzania tusingeweza kukaa kimya wakati ndugu zetu wa Burundi mko hatarani. Tungefanya hivyo naamini msingetuelewa na tusingeeleweka kwa watu wengine.
Mheshimiwa Rais;
Wajibu wetu kwenu pia ulitokana na ukweli kwamba sisi ni majirani. Na kwa mila na desturi za Kiafrika, majirani daima husaidiana. Na jirani mwema ni yule anayemsaidia
mwenzake wakati anapokuwa katika matatizo. Ndio maana sisi Watanzania siku zote tumekuwa tukisukumwa na dhamira ya kuwa majirani wema wa Burundi . Tumekuwa tukifanya hivyo licha ya uwezo wetu mdogo na wakati mwingine mazingira magumu.
Tutaendelea kuwa majirani zenu wema na tutakuwa tayari kusaidia wakati wote kwa kadri ya uwezo wetu. Na katika hili napenda kuwahakikishia kuwa hatutachoka, labda mtuchoke nyie!
Mheshimiwa Rais;
Naomba sasa uniruhusu kuelezea lengo la ziara yangu hapa nchini. Ziara yangu ina madhumuni makubwa matatu. Kwanza nimekuja kujitambulisha rasmi kwenu kama
kiongozi mpya wa nchi yangu; pili nimeleta salamu za pongezi kwenu kutoka kwa Watanzania na tatu nimekuja kubadilishana mawazo nanyi kuhusu namna ya kuimarisha ushirikiano baina ya nchi zetu mbili.
Kama mjuavyo mimi ni kiongozi mpya sawa na ulivyo wewe Mheshimiwa Rais. Nina miezi 18 tu tangu nipewe heshima ya kuiongoza nchi yetu. Kwa kuzingatia utamaduni wetu wa Kiafrika, nimeonelea ni jambo jema nije kujitambulisha rasmi kwenu kama Rais wa Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania . Aidha, nimekuja kuwahakikishia kuwa serikali yangu itaendelea kushirikiana na serikali yako katika kuimarisha mahusiano mazuri yaliyopo baina ya nchi zetu na wananchi wa pande zetu mbili.
Mheshimiwa Rais;
Madhumuni ya pili ya ziara yangu ni kuwasilisha salamu. Watanzania wenzangu wamenituma nilete pongezi zao za dhati kwako wewe Mheshimiwa Rais na wananchi wote wa Burundi kwa mafanikio makubwa mliyoyapata hadi sasa. Mimi na Watanzania wote tumefurahishwa na kuridhishwa na mafanikio mliyoyapata hivi karibuni chini ya uongozi wako shupavu. Katika kipindi kifupi cha uongozi wako sote tumeshuhudia Burundi ikijengeka na kuwa nchi nzuri ya amani na utulivu kinyume na ilivyokuwa siku za nyuma.
Tunakupongeza sana Mheshimiwa Rais kwa ujasiri na moyo wako wa uzalendo ambao umesaidia sana katika kuwaunganisha wananchi wa Burundi chini ya serikali yako na kuwafanya wawe kitu kimoja. Aidha, tunawapongeza wananchi wa Burundi kwa jumla kwa kukubali kujenga umoja na mshikamano wa kitaifa ambao umewezesha kupatikana kwa utulivu na amani ya kudumu nchini mwenu. Tunawasihi nyote mtumie utulivu na amani iliyopo sasa katika kuijenga upya Burundi ili iwe nchi yenye neema kwa kila mmoja wenu.
Ni matarajio yetu kuwa kila raia wa Burundi ataweka pembeni tofauti zake za kisiasa na kuungana nawe Mheshimiwa Rais katika kazi ngumu na nzito ya kuijenga upya Burundi . Kwa msingi huo, tunawaombeni mhahakikishe kuwa makubaliano yenu na PALIPEHUTU-FNL yanafuatiliwa kwa karibu na kutekelezwa. Wananchi wa Burundi waliweka matumaini makubwa kwenye mkataba wa amani uliotiwa saini mjini Dar es Salaam mwezi Septemba mwaka jana baina yako na Bwana Agathon Rwasa, Kiongozi wa PALIPEHUTU-FNL kwa kuwa yanafungua pazia la migogoro nchini Burundi na kufungua ukurasa mpya wa maridhiano na ujenzi mpya wa taifa. Kusuasua kwa utekelezaji kumechelewesha kutimia kwa matumaini. Ni matumaini yangu kuwa mazungumzo yenu ya juzi Mjini Dar Es Salaam yameondoa vikwazo vya mwisho na kwamba sasa utekelezaji utakwenda kwa kasi iliyotarajiwa. Nakuahidi, nawaahidi wananchi wa Burundi kuwa Tanzania itaendelea kuwa nanyi bega kwa bega mpaka hatua ya mwisho.
Mheshimiwa Rais;
Kuhusu wakimbizi wa Burundi walioko nchini mwetu, napenda kukuahidi kuwa tutaendelea kushirikiana na serikali yako pamoja na Shirika la Kuhudumia Wakimbizi Duniani (UNHCR) katika kuhakikisha kwamba wakimbizi hao wanarejea hapa nyumbani kwao mapema iwezekanavyo.
Kama wewe mwenyewe ulivyotanabahisha kwenye hotuba yako, hali ya kisiasa na kiusalama sasa ni nzuri hapa Burundi . Wananchi wote wanaishi kwa amani na kwa raha mstarehe bila matatizo. Kwa hiyo hakuna sababu tena ya wananchi wenzenu wengine kuendelea kuwa wakimbizi hasa ikizingatiwa kuwa sababu zilizowafanya waikimbie nchi yao sasa hazipo tena. Watu hao wana haki ya kurudi kwao ili kuungana na wananchi wenzao kuijenga nchi yao .
Mheshimiwa Rais;
Mbali na kujitambulisha na kuwaletea salamu za pongezi za ndugu zenu wa Tanzania , nimekuja pia kubadilishana mawazo kuhusu haja ya kuimarisha ushirikiano wetu wa kibiashara na kiuchumi. Watanzania
tunatambua kuwa nchi zetu mbili zinategemeana kwa mambo mengi. Kwa bahati mbaya huko nyuma kwa sababu ya hali ya vita nchini Burundi mashirikiano yetu yalidhoofika. Hali hiyo sasa haipo. Kwa maana hiyo huu ni muda mzuri wa kujenga upya na kuimarisha ushirikiano wetu kwa faida ya watu wetu wote.
Nafurahi kwamba nchi zetu mbili tayari zimefufua Tume ya Pamoja ya Ushirikiano. Aidha, Tume hiyo imeweza kuainisha maeneo mbalimbali ya ushirikiano. Hata hivyo, jambo muhimu ni kwa Tume hiyo kufuatilia kwa karibu na kuratibu utekelezaji wa mambo yote yaliyokubaliwa na pande zetu mbili . Lengo liwe ni kutoa msukumo mpya katika ushirikiano wetu ili kuharakisha maendeleo ya nchi zetu mbili.
Pili, Burundi sasa ni mwananchama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki jambo ambalo limefungua wazi zaidi milango ya ushirikiano. Napenda kukupongeza tena wewe Mheshimiwa Rais kwa jitihada kubwa uliyoifanya hadi kuiwezesha Burundi kuwa mwanachama kamili wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, kitendo tulichokishuhudia jana pale Kampala . Haya ni mafanikio makubwa kwako, kwa Serikali yako na kwa diplomasia ya Burundi . Hongera sana .
Kujiunga kwa Burundi kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki ni changamoto kwa nchi zetu mbili kutumia nafasi hiyo kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na kiuchumi. Naomba sote tuitumie kwa ukamilifu nafasi hiyo ili nchi zetu ziweze kunufaika kiuchumi.
Nafurahi kwamba kesho nimepangiwa kukutana na wafanyabiashara wa hapa Burundi . Hii ni nafasi niliyokuwa naitafuta kwa siku nyingi. Nitatumia fursa hiyo kubadilishana nao mawazo juu ya njia nzuri zaidi za
kuendeleza na kukuza biashara baina ya nchi zetu mbili. Yale yote tutakayokubaliana kesho sisi tutayatekeleza mapema iwezekanavyo.
Nitapenda kutumia fursa hiyo kuwahakikishia kuwa reli, barabara, maziwa, bandari na anga ya Tanzania iko wazi na huru kwa Burundi kuitumia. Tunayo matatizo kadhaa kwenye reli, barabara na usafiri wa anga ambayo tunaendelea kuyashughulikia. Tunaimarisha uendeshaji wa reli, tunafufua shirika la ndege la Tanzania na usafiri wa ndege wa kuja Bujumbura . Tuna mpango wa kutatua matatizo ya Bandari za Dar Es Salaam na Kigoma. Pia tuna mpango wa kujenga barabara ya lami toka Kigoma hadi Tabora na kutoka Tabora hadi Manyoni. Yote haya yakitimia yatarahisisha sana usafiri na uchukuzi kati ya Burundi na Tanzania .
Mheshimiwa Rais;
Naomba nimalize hotuba yangu kwa kukuhakikishia tena wewe na ndugu zetu wote wa Burundi kuwa Tanzania daima itaheshimu, italinda na itaimarisha haki yenu ya kutumia miundombinu yake ikiwemo barabara, reli na bandari. Tunafanya hivyo kwa vile ni wajibu wetu wa kimataifa. Na siku zote tutautekeleza wajibu wetu huo kikamilifu kwa faida ya nchi zetu mbili na watu wake.
Waheshimiwa Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana;
Baada ya kusema hayo sasa kwa heshima na taadhima naomba nyote mjumuike nami katika:
· Kuwatakia afya njema na maisha marefu Rais Pierre Nkurunziza na Mama Denise Nkurunziza;
· Kuombea amani na ustawi wa watu wa Burundi ; na
· Kwa ajili ya kuendeleza na kuimarisha udugu, urafiki na mshikamano baina ya wananchi wa Burundi na Tanzania .
Tunywe kwa ajili ya ushirikiano.
Asanteni kwa kunisikiliza.
JK YUPO HOME HAPO ...MAANA MAMBO YA NGOMA WAKWAREE NDIO HOME.
ReplyDeleteupigaji ngoma gani huo utasema hajakulia ngomani? kanyoooka!!
ReplyDeletemwenzie kidogo kajitahidi pozi la kingomangoma
JK wakilisha waha na wahangaza hapo.......
ReplyDeleteYeah...Piga ngoma sana lakini at the same time sikiliza sauti za raia wako nyumbani.
ReplyDeleteHatutaki muunganooooooo period
HATUTAKI MUUNGANO
The worse thing you could do to our country is to bring back that East african federation thing
WE VOTE NEGATIVE TO FEDERATION WITH KENYA AND UGANDA
Mheshimiwa Issa PICHA INAELEWEKA HII..JK..KONSETRESHENI YAKE NI YA HALI YA KIPEKEE..MBONA PICHA NUSU HII..MABINTI WANAOKATIKA HATUWAONI..JK.."..UTAMU WA NGOMA UINGIE UCHEZE.."
ReplyDeletehivi Jakaya ataacha lini kujimbulisha? Nani asiyejua yeye ni rais wa Tanzania? Hii si sababu ya yeye kufanya ziara. Ni bora afikirie sababu nyingine. Nawakilisha.
ReplyDeleteHii ya Raisi wetu sasa kali. Ni kama vile mtu anafanya baby shower mtoto anatambaa..Miezi 18 kazini bado unajitambulisha kwa jirani zako...!!!!! Afadhali ingekua umeenda kujitambulisha North Pole hapo kwa mjirani hata watoto wadogo wameshajua raisi wa tanzania ni Kikwete na sio Mkapa tena
ReplyDeleteOfficially, a president in a blue suit... how funny!!
ReplyDelete