Habari za kifo cha Mh. Salome Mbatia kimestua na kusikitisha wa-Tanzania wengi, nami nikiwa mmoja wao.


Namkumbuka Mama Mbatia, kama tulivyozoea kumwita, kwa mengi tokea alipokuwa bosi wa Biashara Consumers Services (BCS) yenye makao yake makuu jengo la CRDB mtaa wa Azikiwe, ambapo mara kwa mara alikuwa akiniita na kunipa tenda hizi na zile za kupiga picha aidha za shughuli za BCS ama za familia.


Mara kadhaa yeye na familia yake walikuwa wakinikaribisha nyumbani kwao mtaa wa Uganda kwa ajili ya kupiga picha za familia, iwe za kipa imara ama sherehe zingine, ama za kumbukumbu tu, kiasi nikatokea kuzoeana nao kama ndugu wa karibu. Siwezi kusahau ukarimu wake wa dhati awapo nyumbani ambapo kila mara alishurutisha nipate chai ama soda aliyokoroga ama aliyofungua na kunimiminia glasini yeye mwenyewe kwa mkono wake, japo wadogo zangu na watumishi walikuwepo kuweza kufanya hivyo. Ni kitendo adimu na adhimu kwa mtu kama mimi kuhudumiwa tena kwa unyenyekevu na mtu kama Mama Mbatia ambaye licha ya nyadhifa zake alikuwa mtu wa kawaida ndani na nje ya nyumba yake.


Kila tulipokutana katika enzi za uhai wake alizoea kunipa salamu za wadogo zangu, hasa Junior, ambaye tulitokea kushibana kutokana na mimi kuvutiwa na maswali yake ya mara kwa mara na ya karibu kila kitu, ikiwa ni pamoja na kuhoji namna kamera inavyofanya kazi, ama kwa nini mie huwa sifumbi jicho moja ninapopiga picha tofauti na wapiga picha wengine wengi anaowafahamu.


Ni kweli kwamba mtu akiaga dunia sifa kede kede humwagiwa, ila si uwongo kwamba mie simo kwenye mkumbo huo. Na sisti kumsifia Mama Mbatia kama mmoja wa watu wasio na maringo, makuu, madharau kwa mtu yeyote bila kujali hali ama mali zake. Nilikuwa daima najisikia kama niko nyumbani kwa dada yangu kila ninapokanyaga kwake ama nikutanapo nae kikazi. Daima likuwa haishii kunijulia hali bali pia kutaka kujua naendeleaje na kazi na je nyumbani kwema?


Hapa nilipo nina uchungu moyoni kwa kubakiwa na deni lake, ambalo ni kumsafishia picha aliyopiga siku ya harusi moja ambapo alikuwa kavaa nguzo za kimasai mwaka jana. Hakika alipendeza sana nami jambo la kwanza kunijia akilini baada ya kusikia habari za kifo chake ni hili deni la picha na kujikuta nanyong'onyea kwa kutomtimizia haja yake hiyo. Nikaweka nadhiri ya kuitengeneza na kuiwakilisha hiyo picha kwa familia yake baada ya matanga kwani moyoni deni hilo ni zito hasa ikizingatiwa kwamba ahadi ni deni.


Hivi ninavyoongea nimetumiwa picha nyingi zinazoonesha sehemu ya tukio, moja ikionesha mkono wake wa kushoto ulio na saa ukichungulia katikati ya mabati ya gari lake, ambayo hata kama isingekuwa kuzingatia maudhui ya taaluma ya kutochapisha picha zinazotisha, nisingeweza kuzibandika humu asilani. Hata zile ambazo zimechapwa kwenye baadhi ya magazeti nimejikuta naziangalia kwa moyo mzito na kuangalia pembeni kwa uchungu wa mkuki moyoni.


Naweza kusema mengi na bado nisiwe nimemaliza angalau robo ya ninayotaka kusema juu ya Mama Mbatia ambaye namtaja kama marehemu kwa moyo mzito kwani inaniwia vigumu kuamini kwamba hatunaye tena duniani.


Mungu ailaze mahala pema peponi roho ya Mama Salome Joseph Mbatia na awape familia, ndugu jamaa na marafiki moyo wa uvumilivu katika wakati huu mgumu, na wafarijike kwamba sisi tulimpenda ila Mungu amempenda zaidi


Amina



Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 5 mpaka sasa

  1. Michuzi,

    Kifo chake kimegusa wengi hata tulio nje ya nchi. Hasa tuliyokuwa na bahati ya kumfahamu.

    Na sisitiza chanzo cha hiyo ajali ichunguzwe. Dereva kakimbia. Waligongana uso kwa uso (head on collision) mchana.

    REST IN PEACE ETERNAL DADA ROSE.

    ReplyDelete
  2. umetuelezea vizuri sana kaka michuzi atleast tunapata kumjua kwa undani RIP mama

    ReplyDelete
  3. Chemi, dada Rose, sikujua jina jingine la Mh. Salome Mbatia lilikuwa ni Rose.

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...